Na festus pangani, Ludewa-Njombe Yetu
ONGEZEKO la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi wilayani Ludewa katika mkoa mpya wa Njombe kunasababishwa na hali duni ya kipato, wazazi kutokuwajibika, idadi kubwa ya wategemezi na wengine kufiwa wazazi kutokana na ugonjwa wa ukimwi imefahamika.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa huduma za watoto walio katika mazingira hatarishi wilayani Ludewa wakati wa ufunguzi wa semina ya siku moja kwa asasi na wadau mbalimbali Afisa ustawi wa jamii Petro Mahanze alisema tatizo la watoto waishio katika mazingira hatarishi ni kubwa sana wilayani kwake na kwamba waliokwisha tambuliwa ni 8420.
“Tatizo la watoto waishio katika mazingira hatarishi wilayani hapa ni kubwa kutokana na sababu nyingi ikiwemo ugonjwa wa ukimwi, uzembe na ulevi wa wazazi, magonjwa sugu na umaskini wa kipiato” alisema Mahanze
Mahanze alisema hata hivyo watoto waliokwisha kutambuliwa wanaendelea kupata misaada mbalimbali kupitia mfuko wa halmashauri, mfuko wa mbunge na asasi mbalimbali kwa kutoa huduma kama mfuko wa afya wa jamii(CHF) elimu na kutoa vyeti vya kuzaliwa.
Stephen Mtweve Kalinjila ni mratibu wa shirika lisilokuwa la kiserikali la Milo Sayuni Orphanage (Miso) lenye makao yake makuu mjini Ludewa akitoa taarifa ya utekelezaji wa shirika hilo katika mradi wa pamoja tuwalee unaofadhiliwa na Africare alisema watoto zaidi ya 400 wamepatiwa vyeti vya kuzaliwa.
Alitaja kata zilizofikiwa na mradi huo kuwa ni pamoja na kata ya Luana ambayo watoto 365 waishio katika mazingira hatarishi walipewa vyeti vya kuzaliwa, kata ya Manda watoto 42, ikiwa ni pamoja na kupata chakula na lishe, elimu na mafunzo ya ufundi, msaada wa kisaikolojia, kuwajengea uwezo wa kipato walezi wa watoto hao na elimu ya afya ya uzazi kwa vijana.
Jumla ya watoto 1154 wamepatiwa vitambulisho vya bima ya afya kutoka katika kata mbalimbali ikiwemo kata ya Makonde watoto 142, Manda 341, Milo 327 kata ya Mavanga 306, na kata ya Madilu watoto 38.
“Watoto waliopata miradi ya huduma ya miti ya mbao na matunda ni pamoja na kata ya Luana watoto 17, Madilu watoto 286, Milo watoto 140, Manda 54 na Mavanga watoto 250 na sungura 86 kutolewa kwa watoto 43 wa kata za Milo na Luana” Alisema Kalinjila
Blogzamikoa
0 comments:
Post a Comment