Home » » SAKATA LA KUHAMISHWA MTENDAJI IGWACHANYA, WANANCHI WAMTAKA MTENDAJI WAO

SAKATA LA KUHAMISHWA MTENDAJI IGWACHANYA, WANANCHI WAMTAKA MTENDAJI WAO

*RC amtetea DC kuhamia Mdandu
Na Waandishi wetu
Wananchi wa Kata ya Igwachanya wanamlilia aliyekuwa Mtendaji wa Kata yao kwa maelezo kuwa alikuwa mchapakazi.
Taarifa ambazo Kwanza Jamii-Njombe imezipata zinasema Job Fute amehamishwa kutoka katika kata hiyo kimyakimya baada ya kulitaarifu gazeti hili juu ya tetesi zilizopo katika kata hiyo juu ya uamuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe kutokubali nyumba ya mbunge na kuamua kuanzia shughuli zake kata ya Mdandu.
Imefahamika baada ya Fute kuondolewa katika wadhifa wake kama mtendaji wa Kata ya Igwachanya, hivi sasa yupo mapokezi katika idara ya utumishi katika ofisi za Halmashauri kama adhabu.
Hata hivyo, katika mkutano na wananchi, Mkuu wa Mkoa wa Njombe Kepteni (Mstaafu), Assery Msangi aliwaeleza wananchi wa Igwachanya kuwa, kitendo cha kuamua kutumia ofisi za Mdandu ni kuepuka matumizi mabaya ya fedha kwani ingeigharibu wilaya hiyo ya Wanging’ombe kiasi kisichopungua sh. 90 milioni kuikarabati shule waliyokuwa wamepewa na kanisa huko Igwachanya.
Msangi aliyetumia muda mwingi kuelezea kwa nini ofisi ya DC alisema “Maneno yamekuwa mengi, sasa ni wakati wa kufanya kazi…tumeshatengewa sh.2.5 bilioni kwa ajili ya kujenga ofisi.”
Hata hivyo aliwataka wakazi hao kukubali madhara yanayotokana na eneo lao kuwa makao makuu kama kubomolewa nyumba kutokana na upanuzi wa barabara na pamoja kuanza kulipia huduma kama maji.
Akizungumzia uhamisho wa ghafla wa mtendaji wa kata ya Igwachanya kwa kueleza ‘ukweli’, Shukuru Martin, mkazi wa eneo hilo amesema, muda mfupi wa Fute umekuwa na maendeleo ya haraka hasa uhamasishaji wa uchangiaji wa sekondari.
Alikwenda mbele na kuongeza, wakazi wa eneo hilo hawaoni jambo baya aliloeleza kwenye gazeti na kuongeza; “tunashangaa serikali ilivyokuja juu na kumwamisha kiongozi wetu tena bila hata kutuambia lolote. Sasa tutaona itakavyokuwa sababu hatutamkubali mtendaji yoyote atakayeletwa kwenye kata hii.”
Naye Athuman Kilamlya, mkazi wa Igwachanya amesema, uamuzi huo unaonesha pasipo shaka kwamba, serikali haiwapendi viongozi wanaopenda kusema kama taarifa za Fute alizotoa kupitia Kwanza Jamii-Njombe.
Hildegat Mwanyika alilaumu kitendo cha mkurugenzi kumhamisha ghafla mtendaji huyo bila kuangalia upande wa pili ambao ni wa wananchi kwani wanamjua utendaji wake na kumwondoa ni sawa na kuwarudisha wananchi nyuma kimaendeleo.
“Mkuu wa wilaya alibisha hodi hapa na tulimpokea kwa moyo mmoja sasa kwanini aondoke tena bila taarifa yoyote? Mtendaji aliongea kwa niaba yetu sasa kwanini mkurugenzi amwamishe bila hata kusikia lolote kutoka kwetu, kwa maana hiyo mkurugenzi pia hana nia njema na sisi na anakubaliana na yale ambayo yataendelea kuturudisha nyuma,” alisisitiza.
Igwachanya ni eneo lililopo Wanging’ombe na Rais Jakaya Kikwete alitangaza kuwa litakuwa makao makuu ya wilaya. Kutokana na maandalizi duni ya kulifanya eneo hilo kuwa makao makuu, Mkuu wa wilaya hiyo, Esterina Kilasi aliamua kuweka ofisi eneo ya Mdandu kwa muda, jambo lililowatisha wakazi wa Igwachanya kuwa huenda alitaka kuhamia huko moja kwa moja.
Chanzo: Jamii Kwanza Njombe

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa