HABARI PICHA ZA MAZISHI YA ALIYEKUWA MWENYEKITI WA CHAMA CHA MAPINDUZI WILAYA YA NJOMBE MZEE ADAM MSIGWA


 Deo Sanga ambaye ni Mbunge na Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Njombe akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Njombe.


Aliyekuwa  mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Njombe, Adam Ismail Msigwa (pichani) ambaye alijukana kwa jina maarufu kama 'Shilingi ni Vita' amefariki  nyumbani katika Mitaa wa Kwivaha Njombe mjini na mazishi yalifanyika katika kijiji cha lisitu.
Mkuu wa mkoa wa Njombe Cept. mstaafu Aseri Msangi (kushoto ) wa pili ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe Bw Saitabau na wa mwisho (kulia) ni Kamanda wa polisi mkoa  SACP  Ngonyani.
"MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU PEMA PEPONI"
 'AMINA'
PICHA ZOTE NA JAMES FESTO & PROSPER MFUGALE.

WAAJIRI WATAKIWA KULINDA AFYA ZA WAFANYAKAZI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

SERIKALI imewataka waajiri wote kuhakikisha wanaanzisha mifumo bora mahali pa kazi itakayohakikisha wafanyakazi wao wana usalama na wenye afya bora.
Alisema suala hilo si jambo la hiari kwani linagusa uhai na maisha ya watu.Akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya afya na usalama mahali pa kazi Duniani, Makamu wa Rais, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, aliwataka waajiri wasikwepe wala kuogopa gharama katika hilo.
"Zingatieni kuwa hakuna kitu chenye thamani kuzidi uhai na maisha ya watu," alisema.
Alisema takwimu za Shirika la Afya Duniani (ILO) zinaonesha kuwa Kila mwaka duniani takriban watu milioni 337 hupata ajali kazini na kati yao wafanyakazi milioni 2.3 hufariki kutokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi wanazofanya.
"Takwimu zinatuonesha kuwa watu wanaofariki kutokana na magonjwa ya ajali kazini ni wengi kuliko wale wanaofariki vitani, ni wazi kuwa ajali nyingi na magonjwa kazini hutokana na wafanyakazi kutozingatia kanuni za usalama na afya kazini na waajiri kutochukua hatua za kupunguza ajali na magonjwa hayo," alisema Dkt. Bilal.
Alisema kila mfanyakazi anastahili kufanya kazi yenye ujira wa kutosha kukidhi mahitaji ya msingi katika mazingira salama bila kuhatarisha afya yake, kinyume na hapo kazi hiyo haitakuwa ya staha na haipaswi kufanywa na binadamu yeyote, inayostahili kupigwa marufuku.
Hata hivyo, alisema siku ya usalama na afya mahali pa kazi duniani ni siku muhimu kimataifa ambapo nchi zote wanachama wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) tangu mwaka 2001 zilitakiwa kuadhimisha siku hiyo.
Pia alisema maadhimisho hayo yanatoa fursa ya kubainisha njia mbalimbali za kuzuia magonjwa na ajali zinazotokea kazini na kuimarisha kampeni za kuboresha usalama afya na ustawi wa wafanyakazi wakiwa kazini.
Alisema Serikali inafanya juhudi kubwa kuhakikisha inadhibiti matumizi yasiyofaa ya kemikali sehemu za kazi na maeneo mengine kwa manufaa ya afya na wananchi wake.
"Pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali madhara ya kemikali yameendelea kuathiri jamii yetu kwa njia moja au nyingine na haya yanachangiwa na tabia za baadhi ya watu wasio waungwana miongoni mwa jamii," alisema Dkt. Bilal. Alisema Serikali itaendelea kusimamia na kudhibiti matumizi mabaya ya kemikali kwa kutoa elimu kwa watumiaji na wananchi kuhusu matumizi sahihi na madhara yatokanayo na matumizi mabaya ya kemikali.

Chanzo;Majira

Wezi waiba miundombinu ya soko la Ngiu Makete

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Katika hali ya kushangaza na kusikitisha, wezi wasiofahamika wameiba baadhi ya miundombinu ya soko la Ngiu wilayani Makete mkoani Njombe licha ya soko hilo kuwa na mlinzi.

Mwandishi wa blog hii ambaye amefika eneo la tukio mara baada ya kupenyezewa taarifa hizi na wananchi, ameshuhudia baadhi ya miundombinu haipo ikiwemo mifuniko yote ya chuma inayofunikia masinki ya vyoo, pamoja na mabomba ya kutiririshia maji ya mvua

Taarifa kamili na picha zote za tukio hilo zitakujia baadaye kidogo.
 Muonekano wa soko la Ngiu lililopo kata ya Iwawa, Makete mjini.
 Chemba ya choo cha soko hilo ikionekana baada ya wezi kuiba mifuniko yote mitatu ya kufunikia chemba hiyo
Na Edwin Moshi

MAONI:RIPOTI YA CAG HAITOI MATUMAINI YOYOTE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha wa 2012/13 imefichua madudu ya ajabu, ambayo bila shaka yatakuwa yameondoa matumaini ya wananchi ya kukua kwa uchumi na kuwaondolea umaskini uliokithiri. Ripoti za CAG za miaka ya fedha iliyopita zilikuwa pia zinafichua madudu ya kutisha, lakini baada ya Serikali kuahidi kwamba ingeepuka kurudia madudu hayo na kuzifanyia kazi changamoto nyingi zilizokuwa zikiibuliwa na ripoti mbalimbali za CAG, wananchi wengi walipata matumaini.
Inasikitisha kwamba ripoti hiyo iliyotolewa ufafanuzi na CAG mwenyewe, Ludovick Utouh juzi, imeonyesha dhahiri  kwamba Serikali haijawa na dhamira ya kweli ya kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za Serikali na kupambana na vitendo vya ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma. Pamoja na kuwapo kwa Bunge na mifumo mingine kadhaa ya kuhakikisha kwamba Serikali inakuwa na nidhamu katika kusimamia mapato na kudhibiti matumizi yake, bado hakuna mabadiliko wala dalili za uwajibikaji katika matumizi ya fedha za Serikali.
Ripoti ya CAG inaonyesha kwamba matumizi hayo mabaya yanaendelea pamoja na hali mbaya ya uchumi inayolikabili taifa. Kwa mwenendo huo, inaonekana hakuna uwezekano wa kupunguza Deni la Taifa ambalo lilifikia Sh21.20 trilioni, ambalo ni ongezeko la Sh4.23 trilioni sawa na asilimia 25, ikilinganishwa na Sh16.98 trilioni katika mwaka wa fedha wa 2011/12. Ndani ya Serikali umekuwamo utamaduni wa ufujaji wa fedha tunaoweza kusema ni wa mashindano, ambao umechangia kupanda kwa deni la ndani kutoka Sh4.55 trilioni mwaka 2011/2012 hadi Sh5.78 mwaka wa 2012/13, likiwa ni ongezeko la Sh1.23 trilioni, sawa na asilimia 27.
Mwenendo huo ni hatari kwa uchumi na maendeleo ya taifa letu. Baya zaidi ni pale Serikali inapoendekeza mikopo kutoka katika benki za biashara nje ya nchi. Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), inasema kwamba Serikali imekuwa ikikopa wastani wa Sh360 bilioni kwa mwezi kutoka nje. Kutokana na hali hiyo,  Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki  ya Dunia (WB), vimeonya dhidi ya mwenendo huo kwamba utahatarisha uchumi, ingawa Ripoti ya CAG inasema mikopo hiyo imesaidia miradi mikubwa ya maendeleo kama uboreshaji wa miundombinu na kadhalika.
Sisi hatudhani kama mikopo hiyo ina madhara kwa uchumi iwapo utakuwapo uwazi na itasimamiwa kwa uadilifu, kwa maana ya kuhakikisha kwamba siyo tu unakuwapo usimamizi katika  matumizi ya fedha hizo, bali pia zinatumika kuendesha miradi iliyokusudiwa. Miradi mingi ya maendeleo imekuwa ikikwama kutokana na fedha zake kuingizwa katika michepuko isiyofaa, mbali na wizi na ubadhirifu wa baadhi ya wanasiasa, watendaji wa Serikali na taasisi zake.
Ripoti ya CAG imebaini ufisadi mkubwa katika maeneo mengi ya mapato na matumizi ya fedha za Serikali. Kwa mfano, magari mapya 11 yenye thamani ya mamilioni ya shilingi yalinunuliwa lakini yaliishia katika miliki za watu binafsi. Sh1.62 zililipwa kama mishahara kwa watumishi hewa, huku misamaha ya kodi ikilipotezea taifa Sh1.52 trilioni ambazo zingeweza kujenga shule za sekondari za kisasa zaidi ya 300. Ripoti ya CAG haitoi matumaini. Serikali isipopambana na ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma, maendeleo na ustawi wa jamii nchini utabaki kuwa ndoto za mchana.
Chanzo:Mwananchi

VETA MAKETE WATEMBELEA WATOTO YATIMA NA KUTOA MISAADA MBALIMBALI‏

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

 Wafanyakazi wa VETA Makete wakiwa katika picha na watoto yatima wa kituo cha Bulongwa.
 Mfanyakazi wa VETA Makete akiwa amembeba mtoto yatima anayelelewa kituoni hapo
 Sanga akiwa amembeba mtoto yatima anayelelewa katika kituo cha Bulongwa
 Wakifurahia pamoja na watoto hao kwa kuimba nyombo.
 Wakiwa katika picha ya pamoja nje ya kituo hicho.
 Methew Komba akiwa amembeba mtoto yatima
 watoto wakifurahia kutembelewa na wafanyakazi wa VETA Makete.
 Hapa mmoja wa wafanyakazi wa VETA Makete akicheza na watoto hao.
---------
Kufuatia wilaya ya Makete mkoani Njombe kuwa miongoni mwa wilaya zenye watoto yatima, wafanyakazi wa chuo cha VETA Makete wametembelea kituo cha kulelea watoto yatima cha Bulongwa kilichopo wilayani hapa na kutoa misaada mbalimbali

Akizungumza na mwandishi wetu kwa niaba ya wafanyakazi wenzake alioambatana nao Bw. Mathew Komba amesema wao kama VETA Makete wameguswa na namna watoto hao wanavyopata tabu kwani hawakupenda kuishi maisha hayo lakini kutokana na kufiwa na wazazi wao ndiyo maana wapo katika kituo hicho

Amesema awali walikuwa wamepanga kuwatembelea watoto hao kabla ya pasaka lakini kutokana na sababu zisizoepukika walishindwa kufanya hivyo lakini walijipanga kama walivyokuwa wamedhamiria na jana walifika kituoni hapo kuwaona watoto hao na kuwapa msaada huo

Bw. Komba amesema baadhi ya vitu walivyovikabidhi ni pamoja na mafuta ya kupikia, sukari, mchele, sabuni, juisi, dawa za meno na vingine vingi vyote vikiwa na thamani ya tsh. 329,000/=

Amewaomba wadau wengine kuwaunga mkono kwa kwenda kuwasaidia watoto yatima kwani ni jukumu la jamii kwa ujumla kuhakikisha wanawatunza watoto hao licha ya kwamba wanalelewa kwenye vituo mbalimbali

Kwa upande wake Bi Sekela Nkyami kutoka kituo hicho cha kulelea watoto yatima Bulongwa amesema ingawa kituo hicho kina vitega uchumi mbalimbali lakini bado kinategemea misaada kutoka kwa wafadhili mbalimbali wakiwemo wakazi wa Makete wenye moyo wa huruma kama walioufanya chuo cha VETA

Amesema watoto hao waliopo katika kituo hicho si mali ya kituo pekee bali ni wa jamii yote kwa hiyo kuiomba jamii kushirikiana nao katika matunzo ili watoto hao wasijisikie wapweke kutokana na uyatima walio nao

"Ni kweli uyatima unatesa, ila tunawaomba wananchi waje kutoa misaada mbalimbali kwa watoto hawa, kumekuwa na kasumba kuwa wakishaletwa hapa basi si wao tena bali ni wa kituo, hii sia sawa bali tunatakiwa tushirikiane kwa pamoja chochote kidogo utakachokipata kinatosha kutusaidia" amesema Bi. Nkyami

Na Edwin Moshi, Makete

USHIRIKIANO KATI YA EPZA,KOREA KUIMARISHWA ZAIDI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

SERIKALI ya Tanzania kupitia Mamlaka ya U kanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA), inatarajia kuanza kupata wawekezaji wengi kutoka Jamhuri ya Korea Kusini kwa faida ya nchi zote mbili.
Matarajio hayo yanatokana na ziara iliyofanywa hivi karibuni na wawekezaji katika mamlaka hiyo na kujionea maeneo maalumu ya uwekezaji na fursa zinazopatikana katika maeneo hayo.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt. Adelhelm Meru, hatua hiyo ni muhimu kwa nchi hizo mbili katika kuimarisha uchumi na uwekezaji endelevu.
Ujumbe huo ulijumuisha wafanyabiashara wakubwa kutoka kampuni 22 za nchi hiyo.
"Wamekuja na ujumbe mkubwa sana na tunatarajia sasa kuanza kupata wawekezaji wengi kutoka nchi hii," alisema Dkt. Meru.
Ujumbe wa wafanyabiashara hao uliongozwa na balozi wa nchi yao nchini Tanzania, Chung H na ilikuwa ni mara ya kwanza kwa kundi kubwa la wafanyabiashara wa nchi hiyo kuja nchini.
"Sisi tulitumia nafasi hii kuwaonesha vivutio ambavyo vinarahisisha biashara na uwekezaji katika maeneo yetu," alisema. Pia walioneshwa fursa zilizopo katika maeneo ya mamlaka zikiwemo za kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani mazao ya kilimo na madini kwa ajili ya masoko ya nje.
Fursa nyingine zilizotajwa zilikuwa za ujenzi wa miundombinu ya nishati, maji na utoaji wa huduma mbalimbali katika maeneo maalumu ya mamlaka hiyo yaliyopo katika mikoa 20 hapa nchini.
Alisema maeneo maalumu ya vipaumbele ni pamoja na Bagamoyo, Mtwara na Kigoma ambayo yana fursa nyingi.
 "Kwa bahati nzuri tumekuwa tukifanya nao kazi kwa muda mrefu na tunajua wao ni mabingwa wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)," alisema.
Naye Balozi Chung H, alisema nchi yake inauhusiano mzuri na Tanzania na ziara ya wafanyabiashara wa nchi yake inadhihirisha uhusiano huo.
"Tunahitaji kuzidi kuongeza ushiriki wa wafanyabiashara wetu kufanya biashara na nchi hii ya Tanzania," alisema.
Mkuu wa ujumbe wa wafanyabiashara hao, Lee Kang Min, alisema wamekuja nchini Tanzania kwa ziara ya kuangalia mazingira ya uwekezaji na wamefurahi kuona fursa nyingi zilizopo.
"Tutarudi kuwekeza," alisema na kuongeza kuwa wafanyabiashara hao waliridhika na hali halisi ya mazingira ya uwekezaji na fursa zilizopo Tanzania. Wafanyabiashara hao pia walifanya ziara katika kiwanda cha nguo kilicho katika eneo la mamlaka hiyo cha Tanzania Tooku Garments Co. Ltd.

Chanzo:Majira

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa