TUSHIRIKIANE KUWAWEZESHA WANANCHI KIUCHUMI - NAGU

 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk. Mary Nagu.
 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk. Mary Nagu, amesema kazi ya kuwawezesha wananchi kiuchumi si ya serikali pekee hivyo wadau malimbali na taasisi za fedha zinapaswa kutumia sehemu ya faida yake kuwasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi.
 
Aliyasema hayo ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana wakati wa kikao cha kazi baina yake na Wajumbe wa Baraza la Uwezeshaji la Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), akiwamo Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Beng’i  Issa na Mwenyekiti wa Bodi, Omari Issa.
 
Baadhi ya ajenda kwenye kikao hicho ilikuwa ni kupata na kujadili taarifa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi Tanzania, fedha za mpango wa uwezeshaji wananchi kiuchumi na kuongeza ajira na uzinduzi wa mkakati wa sekta mbalimbali wa uwezeshaji wananchi kiuchumi.
 
Dk. Nagu alitoa wito kwa NEEC kukutana na Chama cha Wenye Benki nchini na kuwashawishi waone umuhimu wa kutumia sehemu ya faida yao katika kuwawezesha wananchi kiuchumi kwenye miradi ya biashara.
 
“Tangu mfuko wa uwekezaji uanzishwe, haukui na sababu ni kwamba unategemea chanzo kimoja tu serikali, sasa lazima tuondokane na mawazo ya kuitegemea serikali tu tuwe na vyanzo vingine vya mapato na tukikutana na kuwashirikisha wadau mbalimbali, naamini watakuwa tayari kuchangia jitihada hizi za serikali,” alisema.
 
Aidha, alisema vikundi vya kuweka na kukopa maarufu kama vicoba, vikisimamiwa na kuendeshwa  vizuri, vitakuwa mkombozi mkubwa wa uchumi wa Tanzania na kuwakwamua wananchi wengi kuondokana na tatizo la umaskini kwa kuanzisha miradi.
 
Waziri Nagu alisema kuna ushahidi wa baadhi ya wananchi walioanzisha na kusimamia vizuri vicoba na hivi sasa wana mitaji mikubwa inayowawezesha kufanya biashara kubwa na kuongeza mitaji.
 
“Kuna mfano dhahiri wa kikundi cha watu 30 ambao wamefanikiwa kukusanya Sh. milioni 300 ndani ya muda mfupi, sasa kama watu 30 tu wanaweza kukusanya kiasi hicho cha fedha, si jambo la kubeza, inaonyesha kwamba tukivisimamia vizuri vitawakomboa wananchi wengi kiuchumi,” alisema.
 
Alisema iwapo wananchi watajiunga na vicoba na kuwekeza kwenye miradi inayowapa faida ni dhahiri wananchi wengi watakata tamaa ya kujiunga na vikundi hivyo lakini kama vitakuwa vikijiendesha kwa hasara hakuna atakayejiunga.
 
"Kwa bahati nzuri vicoba ni watu wanaofahamiana na wanaoaminiana na wakipata mwongozo mzuri naamini kabisa watafika mbali zaidi, ndiyo sababu nimeona umuhimu wa kumjumuisha Mwenyekiti wao Taifa, Devotha Likokola, kwenye baraza hili, kwa sababu naamini kabisa kupitia Vicoba tunaweza kufika mbali zaidi kiuchumi,” alisem Dk. Nagu.
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

AIBU NYUMBA ZA WAKUBWA KUTUNZA MIHADARATI

Tanzania imekuwa katika vita ngumu ya kupambana na matatizo mbalimbali yanayoisumbua, yakiwamo ya kiuchumi, kijamii na hata kisiasa.
Katika baadhi ya nyakati, matatizo hayo yamegeuka kuwa kikwazo kwenye azma ya kuwapa maendeleo na ustawi wananchi.
Pamoja na matatizo hayo, siku za karibuni na pengine miaka michache iliyopita, biashara za dawa za kulevya imegeuka adui anayeichachafya nchi.
Kwa kiasi kikubwa, biashara hii ambayo inaonekana dhahiri kuwa inahusisha wengi, wakiwamo watu wazima na hata watoto na wengine vijana wasomi wazuri, imegeuka vita ambayo kama nchi ijihesabu kuwa imeshindwa kuidhibiti.
Hatuchelei kusema nchi yetu imeshindwa vita ya kupambana na biashara hii ya dawa za kulevya kutokana na kauli lukuki za baadhi ya viongozi wetu wa kisiasa wa ngazi mbalimbali pamoja na juhudi zinazofanyika kuhakikisha biashara hiyo inakomeshwa.
Ipo mifano michache ya jinsi ambavyo biashara hiyo imekuwa ikiendelea kuisumbua nchi yetu katika siku za karibuni na hata watu wake, ikisababisha ongezeko la vijana kugeuka watumiaji, wauzaji.
Tumeeleza awali kuwa Tanzania inapigana vita hii ikiwa kama tayari imeshindwa, hasa kwa kuzingatia ukweli kwamba baadhi ya viongozi wamekuwa wakituhumiwa kujihusisha nayo, lakini hawachukuliwi hatua zozote licha ya kuambiwa kuwa wanajulikana.
Ni bahati mbaya zaidi kuona kauli za baadhi ya viongozi wetu zikiendelea kusikika, zikiwataja wahusika wa biashara hii kuwa wanajulikana, lakini kwa nini hawakamatwi?
Bahati mbaya, baadhi ya vijana wetu ambao ni nguvukazi muhimu ndio watumiaji, wasafirishaji na hata wauzaji wa dawa hizo, huku baadhi yao wakikamatwa na wengine kuhukumiwa vifungo vya muda mrefu au kunyongwa nje ya mipaka ya nchi yetu.
Hukumu hizo chache kati yake zimefahamika, kuripotiwa kwenye vyombo vya habari nchini au nje ya mipaka ya nchi, lakini zinachafua, kutia doa jina zuri ambalo nchi yetu imejijengea kwa miaka mingi iliyopita. Inafaa viongozi watuambie, ni kwa nini kama nchi tumeshindwa kudhibiti biashara hii ya dawa za kulevya kama wahusika wanajulikana?
Jeshi la Polisi, Kitengo cha Dawa za Kulevya wametueleza kuwa baadhi ya nyumba za wakubwa ndizo zinazotumika kama maficho au vichaka vya biashara hii.
Tunawaamini polisi, walilolisema ni kweli wanawajua wamiliki wa nyumba zile ambao ni wakubwa, lakini tunawauliza wamewachukulia hatua gani ili maficho au vichaka hivyo vya dawa kulevya yaondolewe?
Hakuna shaka, polisi wanaufahamu ukweli wa mtandao huo wa dawa za kulevya, viongozi au wakubwa waliojenga au kumiliki nyumba hizo, ambao hawaishi ndani yake bali wamezipangisha kwa wengine ambao wamezigeuza maficho ya biashara ya dawa za kulevya.
Kama hivyo ndivyo, tunawashauri kuwa badala ya kulalamika, wachukue hatua kwa mujibu wa Sheria ya Dawa za Kulevya, ambayo wanaikariri kuwa inawapa mamlaka ya kuwafikisha wahusika kwenye vyombo vya sheria ambako huchukuliwa hatua zikiwamo za kufungwa maisha au mali zao kufilisiwa.
Tunawashauri viongozi wetu wa kisiasa, vyombo vya dola au ulinzi na usalama wachukue hatua kukomesha tatizo hilo.
Tunadhani, kwa kufanya hivyo, wafanyabiashara wa dawa za kulevya kama ni wapangaji kwenye nyumba hizo za wakubwa, wabanwe wawataje wahusika ili mtandao huo uvunjwe.
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

SIMU ZINAVYOSHAWISHI MAPENZI KWA WANAFUNZI

Tangu teknolojia ya mawasiliano ya simu za mkononi ilipoingia nchini, mambo mengi katika jamii, ukiwamo mfumo mzima wa maendeleo na namna ya kuishi, yamebadilika.
Teknolojia hiyo imeondoa usumbufu uliokuwapo awali, mtu alikuwa analazimika kukaa muda mrefu kusubiri kuunganishiwa simu posta na baadaye katika Kampuni ya Mawasiliano ya Simu Tanzania (TTCL). Hata baada ya kupata mawasiliano bado usikivu ulikuwa hafifu licha ya kupiga kelele sana.
Si hivyo tu, watu walikuwa wanalazimika kufika mjini au miji maarufu kwa ajili ya kusaka mawasiliano ya simu. Pia, wengi walikosa.
Kutokana na gharama kubwa ya simu wakati ule, haikuwa rahisi kwa wanafunzi kuzifikia. Wale waliomudu kupiga walikuwa watoto wa viongozi au wenye uwezo mkubwa.
Leo ni tofauti. Simu za mkononi zimeondoa ukiritimba huo kiasi kwamba watu wengi mjini na vijijini wanamiliki na kufanya mawasiliano wakati wowote na bila kuzuiwa. Ubora wa teknolojia hiyo, ambayo vijana wanaita mtandao, ni kwamba mtu anaweza kuzungumza kwa sauti ya chini hata jirani yake asisikie.
Teknolojia hiyo ina faida kadhaa; imerahisisha muda wa mawasiliano, imeongeza ufanisi katika biashara na kazi. Lakini pia imechangia uvunjifu wa maadili hasa upande wa wanafunzi.
Uchunguzi unaonyesha kwamba japokuwa hakuna sheria iliyotungwa kuwabana wanafunzi kumiliki na kutumia simu katika mazingira ya shule, baadhi ya shule zimeweka taratibu za kuwabana.
Mwanya huo ndio unatumiwa na baadhi ya wazazi kuwapa simu watoto wao kwa madai watumie kuwajulisha wazazi ikiwa wamepata matatizo.
Lengo hilo ni zuri, lakini uchunguzi unaonyesha wengi wao hutumia katika mawasiliano ya hovyo na kupanga miadi ya utovu wa maadili na wavulana au wanaowaita wapenzi wao. Waathirika wakubwa katika mlolongo wote ni wasichana.
Pia, uchunguzi unaonyesha wanafunzi wasichana ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuwanunulia simu hupata vishawishi vya kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi na wavulana ili wanunuliwe simu. Madhara yake huwa ni mimba na kisha kufukuzwa shule.
Udhibiti mdogo
Udhibiti mdogo wa wazazi kuhusu mienendo ya watoto wao ndio umesababisha kubaki wakishuhudia simu za thamani ya hadi Sh200,000 zikimilikiwa na mabinti wao badala ya zile za Sh15,000 ambazo hazina mvuto.
Baadhi ya shule za sekondari kama Ndwika ya Lindi, Mara na Benjamin Mkapa zimeweka sheria kuzuia umiliki wa simu. Aliyekuwa kiranja mkuu wa Mara Sekondari aliadhibiwa kwa kukiuka sheria hizo na alipokataa kikawa chanzo cha vurugu na uharibifu shuleni, akafukuzwa shule.
Uongozi wa Jitegemee Sekondari umeweka sheria kuwa mwanafunzi yeyote atakayekutwa na simu eneo la shule atanyanganywa na mwisho wa muhula simu zote huuzwa kwa mnada mbali ya adhabu nyingine.
Utaratibu huo wa adhabu kali umesaidia kupunguza tatizo hilo na uongozi unaamini umechangia kuzuia wanafunzi wa kike kufanya mawasiliano ya kimapenzi.
Viongozi wa shule wanaamini hatua hizo inawazuia wanafunzi wa kike kujiingiza katika ngono zembe na wengine kupata mimba pamoja na magonjwa ya zinaa kwa lengo tu la kupata simu.
Maoni ya wazazi, walimu na hata wanafunzi ni kwamba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iweke sheria kwa shule zote wanafunzi wasiruhusiwe kumiliki simu pindi wanapokuwa shuleni.
Kuwapo kwa sheria hiyo kutatoa uwiano sawa wa kosa hilo kwa wanafunzi wa shule zote za Serikali na za binafsi ambazo zaidi ya asilimia 80 ya wanafunzi wanamiliki simu tena za thamani.
Katika shule za Serikali mwenye simu hata ya Sh45,000 au Sh35,000 anaonekana wa tabaka la juu.
Kwa hiyo, japokuwa mtandao umekuwa moja ya nyanja kuu za mawasiliano katika maisha ya leo, pale unapotumiwa vibaya na wanafunzi, matokeo yake huwa mabaya kama kujiingiza katika biashara haramu ili wapate pesa za kununulia na wengine kujiingiza katika vishawishi vya mapenzi na wanaume kwa lengo la kununuliwa mtandao.
 Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

FAMILIA YA MSWEMWA YATUMIA MILIONI 100 KUSAIDIA JAMII YA WANANJOMBE‏


Mkurugenzi  wa Hotel ya  Miriam Njombe  Bw Ditram Msemwa wa sita  kushoto akimpongeza  Bw Ngamanga  kwa  uzinduzi wa  kitabu  chake
Mkurugenzi  wa  Hotel ya  Miriam Njombe Bw Ditram Msemwa akizungumza katika hafla ya  kufunga mwaka
Baadhi ya  vijana  wanaonufaika na fursa   hiyo
Baadhi ya  wanafamilia na  wadau mbali  mbali
washiriki  wakifuatilia hafla  hiyo
Mkurugenzi wa taasisi ya  Mafanikio  foundation for  personal development na  mratibu  wa raslimali watu Bw Michael uhahula akitoa  maelezo  mafupi kabla ya  mgeni rasmi
Mgeni  rasmi  katika  hafla  hiyo  Adam Ngamanga  kutoka Afrika ya  kusini akifungua hafla hiyo
Mkurugenzi  wa  Hotel ya  Miriam akifuatilia hotuba  ya  ufunguzi
Baadhi ya  washiriki  wakiwa  katika  hafla    hiyo
baadhi ya  washiriki wa hafla hiyo  wakiungana na Mkurugenzi  wa Hotel ya  Miriam Njombe  Bw Ditram Msemwa wa sita  kushoto  akiungana na mgeni rasmi  Bw Ngamanga  kuzindua  kitabu  cha  Jitambue kilichoandikwa na Ngamanga wa katikati ,

Hiki ndicho  kitambu   cha  jitambue
Mwigizaji maarufu nchini Bw ras   katikati akiwa na  kitabu  hicho
Na Matukiodaimablog

KIASI  cha  Tsh  milioni 100  zimetumika   kusaidia   kusomesha  familia zenye  shida na  kutoa  mitaji ya  Tsh milioni 20  kwa  kila  kijana mwenye  ndoto ya  kujiendeleza  katika familia ya Msemwa na nje ya wanafamilia  hao wilayani Njombe mkoani Njombe.

 Akizungumza  katika hafla  fupi iliyofanyika  jana  katika  ukumbi wa  Hotel ya  Miriam Njombe mkurugenzi  wa Hotel ya  Miriam   Bw Ditram Msemwa alisema  kuwa  wameanzisha utaratibu   huo ambao  uliamnza  ndani ya  familia  kwa  dhana ya  kusaidiana  kimaisha  ila  kwa sasa  wameendelea  kupanua  wigo zaidi kwa  kusaidia jamii nyingine ya  wana Njombe.

"Tilianza kusaiodiana kama  familia kwa  kupeana  mitaji na  pesa za  kusomesha  watoto  ila  sasa  tumepanua  wigo kwa  kusaidia  wengine wa nje ya  familia na lengo letu kuona  Njombe inakuwa na  vijana  wasomi  wengi  zaidi"

Hata  hivyo wanamapango  wa kuanzisha  taasisi  kamili  ambayo  itafanya kazi  ya  kuisaidia jamii ya  wana Njombe  ili kuondokana na  dhana  iliyojengeka toka kwa  baadhi ya  viongozi ambao  wamekuwa  hawapendi  kurudi  kusaidia kwao  baada  ya kupata nafasi ya  uongozi.


Pia  mkurugenzi huyo alimpongeza  mkazi wa Njombe Bw Ngamanga  ambae  kwa  sasa anaishi  nchini Afrika ya  kusini kwa  kuendelea  kuwakilisha  vema  mkoa wa Njombe kwa  kutoa elimu kupitia  kitabu chake  cha  jitambue  ambacho  kimezinduliwa Njombe  na kutaka  vijana   wengine  kuiga mfano  huo .

Kuhusu  mitaji inayotolewa  alisema  kuwa  kila mwaka  wameweka  utaratibu wa  kutoa mtaji wa Tsh milioni 20 kwa  mtu mmoja  ili  kufanya  biashara  pamoja na  kusomesha   watoto  na  kuwa  toka  wameanza mpango huo  kiasi cha Tsh milioni 100  zimetolewa .







Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa