Home » » MWENYEKITI MUFINDI ADAIWA KUTAFUNA FEDHA ZA KIJIJI

MWENYEKITI MUFINDI ADAIWA KUTAFUNA FEDHA ZA KIJIJI

Na Mwandishi Wetu, Mafinga
MWENYEKI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Peter Tweve, maarufu kwa jina la PP, anadaiwa kujimilikisha kibali cha uvunaji wa magogo katika shamba la Sao Hill, ambalo ni mali ya Kijiji cha Magunguli, kilichopo Mufindi, mkoani Iringa.

Wakizungumza mjini hapa kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa kijiji hicho walisema PP alijimilikisha kibali hicho kilichokuwa kikiuzwa kwa Sh milioni 15.

Wananchi hao ambao hawakutaka kutaja majina yao, walisema alipokichukua kibali hicho, hakuweka fedha katika akaunti ya kijiji kwa muda kama walivyokubaliana awali.

Walisema kwa muda wa mwaka mmoja sasa kila wanapohoji katika mikutano ya hadhara kuhusu kibali hicho wamekuwa wakikamatwa na polisi huku wengine wakitishiwa maisha.

Walisema mwaka jana, Wizara ya Maliasili na Utalii iligawa magogo yenye mita za ujazo 500 kwa kila kijiji kinachozunguka shamba la Sao Hill na hatimaye vijiji vivune magogo hayo na kupata fedha kwa ajili ya maendeleo na jumla ya vijiji 12 vilipata mgawo huo.

Habari zinasema kutokana na vijiji kutokuwa na uwezo wa kuchana magogo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Evarista Kalalu, aliitisha mkutano wa viongozi wa vijiji hivyo na kuwapatia bei elekezi kulingana na thamani ya mita za magogo walizopewa ambapo walitakiwa kuuza kibali kuanzia Sh milioni 13 na si chini ya hapo.

Aliwataka viongozi wa vijiji ambavyo havina akaunti katika benki wafungue haraka na watakapouza vibali hivyo fedha ziwekwe katika akaunti hizo.

Hata hivyo, wakazi wa Kijiji cha Magunguli wanasema fedha hizo hazijaingizwa katika akaunti yao hadi sasa.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Camillus Suta, alikiri kibali hicho kuchukuliwa na diwani huyo na kuhusu malipo, alisema tayari diwani huyo amekwishatoa Sh milioni nane ambazo zimetumia kujenga ofisi ya masijala ya kijiji hicho kwa ajili ya kutunza kumbukumbu za hati za ardhi za kimila.

Kauli ya mwenyekiti huyo ilipingana na maelezo ya wananchi kuwa jengo la ofisi hiyo ambalo halijakamilika limejengwa kwa nguvu za wananchi na mfadhili wao Jacob Mwajombe, anayeishi Dar es Salaam.

“Ni kweli mfadhili wetu Mwajombe alitoa shilingi milioni tatu, lakini fedha za diwani shilingi milioni nane na elfu arobaini zimetumika kununua bati wakati matofali na mawe ni nguvu za wananchi, jengo hili limetumia shilingi milioni 15,” alisema.

Kwa upande wake, PP alikiri kumiliki kibali cha kijiji hicho, lakini akasema wanaolalamika ni wale wanaopinga maendeleo.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa