Home » » Kasi ya maambukizi VVU Njombe inatisha

Kasi ya maambukizi VVU Njombe inatisha



KATIBU Tawala wa Mkoa wa Njombe, Mgeni Baruani, amesema kuna kazi kubwa ya kutokomeza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto katika mikoa ya Njombe na Iringa ambayo kiwango cha maambukizi kiko juu.
 Baruani alitoa kauli hiyo jana katika uzinduzi wa kampeni ya Tokomeza Maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, uliofanyika katika Kituo cha Afya cha mji mdogo wa Makambako.
 Alisema Tanzania imeanzisha mpango wa kutokomeza maambukizi mapya ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na wakati huohuo kunawawezesha kina mama hao kuendelea kuishi wakiwa na afya bora.
Alisema jambo muhimu katika mpango huu ni mjamzito kupima afya ili anapogundulika na maambukizi, hatua husika zichukuliwe ili asimwambukize baada ya kuzaliwa.
 Mpango huu utakaotekelezwa nchini kote unatarajiwa kufanyika kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza itahusisha mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Geita, Simiyu na Kagera na ya pili inatahusisha mikoa mingine yote iliyobaki.
 Alisema mapambano ya maambukizi mapya ya VVU ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha yanatokomea kwa kuwajibika kufuata ushauri na kubadili mienendo katika maisha yao.
 Utoaji huduma za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto katika mji wa Makambako ulianza tangu mwaka 2007 ambapo hadi kufikia mwaka 2013 Oktoba, watu 8,641 wamenufaika na huduma hiyo japo kina mama 1,148 walikutwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi.
 Hata hivyo watoto 738 waliozaliwa na kina mama hao walipimwa, watoto 85 walikutwa na maambukizi ya VVU.
Mkoa wa Iringa unaongoza kuwa na maambukizi ya VVU kwa asilimia 19.1 wakati Mkoa wa Njombe ukiwa na maambukizi ya VVU kwa asilimia 14.8. 

Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa