Home » » Fundi wa kujenga barabara achapwa bakora Ludewa

Fundi wa kujenga barabara achapwa bakora Ludewa

Alitakiwa kuondoa kifusi barabarani ili ofisa mmoja wa masuala ya usalama apite, akashindwa kwa vile katapila liliharibika, akaishia kuchapwa viboko hadharani 
Njombe. Mtu anayedaiwa kujihusisha na masuala ya ulinzi na usalama Wilaya ya Ludewa, anadaiwa kumshambulia kwa kumchapa bakora mfanyakazi wa Kampuni ya Boimanda Modern Construction Company Ltd (BMCC) Alphonce Lutengano (25) inayofanya ukarabati wa kilomita 56.5 za Barabara ya Njombe-Ludewa-Manda.
Tukio hilo la aina yake limetokea hivi karibuni katika Kijiji cha Muholo, Kata ya Luana Wilaya ya Ludewa, mkoani Njombe wakati mfanyakazi huyo akiwa kazini,  baada ya ofisa huyo kukuta vifusi vimemwagwa katikati ya barabara wakati akipita kwenda Kata ya Lugarawa kwenye shughuli zake.
Apigwa akiwa kazini
Lutengano anadai kuwa akiwa kazini na mtumishi mwenzake Mary Luca wakisubiri katapila lao lililokuwa linazibwa baada ya gurudumu moja kupata hililafu ili kusambaza vifusi hivyo, ofisa huyo alifika eneo hilo akiwa na mwenzake ndani ya gari akitumia gari aina Nissan Hard Top, alianza kumhoji kwa nini wamemwaga kifusi katikati ya barabara na kumtaka akitoe ili apitishe gari lake kwa madai kuwa haliwezi kupita pembeni kama walivyomshauri.
“Aliponihoji nilimwambia tunasubiri katapila ili tuweze kusambaza kifusi, kwani wakati huo lilikuwa linazibwa baada ya gurudumu moja kuishiwa upepo. Nikamshauri apite pembeni, akakataa akisema nisambaze kifusi haraka ili apite akidai kuwa gari lake haliwezi kupita pembeni. Alisisitiza kuwa tufanye hivyo haraka vinginevyo atanipa adhabu,” anasema na kuongeza.
“Nilidhani utani, ghafla kweli akachuma fimbo ya mti na kuanza kunipiga huku mwenzake akishuhudia, baada ya kuona hivyo mwenzangu alikimbia ndipo nikatoa taarifa kwa mkuu wangu wa kazi Ludewa akaja na polisi wakamkuta”.
Baada ya polisi kujibiwa hivyo walimwacha kwa madai kuwa aende akaendelee na majukumu yake baada ya hapo aripoti kituoni.
Shuhuda anena
Shuhuda wa tukio hilo Mwalimu mstaafu Gerald Meshack Hiluka mkazi wa Muhola akielezea mkasa huo anasema “Mimi niliona mtu anachapwa wakati natoka kumwagilia bustani, sasa nikabaki nimeduwaa kwa mshangao, na sikujua anayemchapa kijana huyu ni nani kwa kuwa nilikuwa napita, hivyo nikabaki naangalia tu”.
Kwa upande wake, Mary Luca anasema baada ya kuona hivyo aliamua kukimbia ili kujinusuru na kipigo ambacho kingeweza hata yeye kumpata.
Fundi Sanifu wa BMCC , Taji Omary alikiri kupokea taarifa ya kupigwa mfanyakazi na kutoa taarifa Kituo cha Polisi Ludewa wakaongozana kwenda eneo la tukio lakini walipofika licha ya polisi kumkuta mtuhumiwa walimwacha aendelee na safari yake kana kwamba tukio alilotenda ni jema kwa jamii.

chanzo;mwananchi.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa