UZEMBE WA WAZAZI CHANZO CHA WATOTO WA MITAANI LUDEWA.


Na festus pangani, Ludewa-Njombe Yetu
ONGEZEKO la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi wilayani Ludewa katika mkoa mpya wa Njombe kunasababishwa na hali duni ya kipato, wazazi kutokuwajibika, idadi kubwa ya wategemezi na wengine kufiwa wazazi kutokana na ugonjwa wa ukimwi imefahamika.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa huduma za watoto walio katika mazingira hatarishi wilayani Ludewa wakati wa ufunguzi wa semina ya siku moja kwa asasi na wadau mbalimbali Afisa ustawi wa jamii Petro Mahanze alisema tatizo la watoto waishio katika mazingira hatarishi ni kubwa sana wilayani kwake na kwamba waliokwisha tambuliwa ni 8420.
“Tatizo la watoto waishio katika mazingira hatarishi wilayani hapa ni kubwa kutokana na sababu nyingi ikiwemo ugonjwa wa ukimwi, uzembe na ulevi wa wazazi, magonjwa sugu na umaskini wa kipiato” alisema Mahanze
Mahanze alisema hata hivyo watoto waliokwisha kutambuliwa wanaendelea kupata misaada mbalimbali kupitia mfuko wa halmashauri, mfuko wa mbunge na asasi mbalimbali kwa kutoa huduma kama mfuko wa afya wa jamii(CHF) elimu na kutoa vyeti vya kuzaliwa.
Stephen Mtweve Kalinjila ni mratibu wa shirika lisilokuwa la kiserikali la Milo Sayuni Orphanage (Miso) lenye makao yake makuu mjini Ludewa akitoa taarifa ya utekelezaji wa shirika hilo katika mradi wa pamoja tuwalee unaofadhiliwa na Africare alisema watoto zaidi ya 400 wamepatiwa vyeti vya kuzaliwa.
Alitaja kata zilizofikiwa na mradi huo kuwa ni pamoja na kata ya Luana ambayo watoto 365 waishio katika mazingira hatarishi walipewa vyeti vya kuzaliwa, kata ya Manda watoto 42, ikiwa ni pamoja na kupata chakula na lishe, elimu na mafunzo ya ufundi, msaada wa kisaikolojia, kuwajengea uwezo wa kipato walezi wa watoto hao na elimu ya afya ya uzazi kwa vijana.
Jumla ya watoto 1154 wamepatiwa vitambulisho vya bima ya afya kutoka katika kata mbalimbali ikiwemo kata ya Makonde watoto 142, Manda 341, Milo 327 kata ya Mavanga 306, na kata ya Madilu watoto 38.
“Watoto waliopata miradi ya huduma ya miti ya mbao na matunda ni pamoja na kata ya Luana watoto 17, Madilu watoto 286, Milo watoto 140, Manda 54 na Mavanga watoto 250 na sungura 86 kutolewa kwa watoto 43 wa kata za Milo na Luana” Alisema Kalinjila
Blogzamikoa

WASIOCHUKUA RISITI BAADA MANUNUZI KUFIKISHWA MAHAKAMANI.


Na Festus Pangani, Ludewa-Njombe Yetu
MKUU wa Wilaya ya Ludewa katika Mkoa wa Njombe Juma Solomoni Madaha amemtaka Mkuu wa Kituo cha Polisi Wialya kumkamata mtu yeyote atakayepatikana au kununua bidhaa dukani bila kuwa na risiti.
Madaha alitoa agizo hilo hivi karibuni katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye stendi ya mabasi yaendayo Manda na Njombe ambapo pamoja na mambo mengine aliutumia mkutano huo kwa kujitambulisha kwa wananchi wa vijiji vya Ludewa (M) Ludewa (K) vinavyounda kata ya Ludewa.
Kauli ya mkuu huyo wa wilaya imekuja baada ya kugundua kuwa serikali inakosa mapato kwa sababu ya wafanyabiashara wasio waaminifu ambao wamekuwa wakiuuza bidhaa bila kutoa risiti jambo linaloikosesha serikali mapato ingawa hakusema ni kwa kiasi gani serikali inakosa mapato kwa mwezi.
Ni kutokana na ukwepaji huo wa kodi akaliagiza jeshi la polisi wilayani humo kumkamata mtu yeyote atakayeonekana kabeba bidhaa isiyokuwa na risiti na kumfungulia mashtaka mahakamani na kutaja duka alilonunua bidhaa hiyo.
Aidha aliwaagiza wafanyabiashara wa bidhaa mbalimbali kuacha tabia ya kukwepa kodi kwa kugushi vitabu vinavyoshindwa kutoa mwongozo kwa maafisa mapato (TRA) kushindwa kumkadilia kodi mfanyabiashara jambo linaloisababishia serikali kukosa mapato.
Awali akitoa taarifa Onesmo Haule ambaye ni afisa mtendaji wa kata ya Ludewa yenye wakazi 10,195, alisema kata yake inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa maji safi na salama, barabara mbovu za mitaa, kuchelewa kwa mbolea ya ruzuku na ulimaji wa mahindi mjini.
 Kwa upande wa elimu Haule alisema kuwa kata yake inazo shule za msingi tano na sekondari tatu ikiwemo chief kidulile inayomilikiwa na serikali, St Alois inayomilikiwa na kanisa Katoliki na Ludewa sekondari inayomilikiwa na jumuia ya wazazi wa ccm. Na kwamba shule zote zinakabiliwa na upungufu wa walimu, vitabu na matundu ya vyoo.
Blogzamikoa

NAMBA YA MPESA NA AKAUNTI ZA KUMSAIDIA MTOTO ALIYETELEKEZWA NA WAZAZI BAADA YA KUUNGUA MOTO, TUNAOMBA RADHI KWA PICHA ZA MAJERAHA YA MOTO YA MTOTO HUYO


Festus Pangani, Njombe Yetu
Mtoto Juliana Mwinuka wa kijiji cha Mbugani kata ya Mavanga wilayani Ludewa Mkoani Njombe, anaomba msaada kwa wadau mbalimbali ili kumsaidia kupata matibabu baada ya kuungua moto na hali yake ni mbaya sana.
Mtoto huyo ambaye kwa sasa anaishi na bibi yake ambaye hana uwezo, baada ya baba mzazi kumtelekeza mara tu baada ya kupatwa na mkasa huo miaka miwili iliyopita.
Juliana ameishi katika maumivu hayo kwa miaka miwili na hana mtu wa kumsaidia kufanikisha matibabu yake.

account ni 6012300170 na kwa M-PESA ni 0755 008038
Blogzamikoa

TUNAWATAKIA IDD EL-FITRI NJEMA


WAISLAMU nchini leo watasherehekea Sikuuu ya Idd el- Fitri ambayo husheherekewa mara baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Tunapenda kuchukua fursa hii kuwatakia sikukuu njema Waislamu wote nchini na kuwaomba washerehekee kwa amani na utulivu kama vile walivyokuwa kwenye mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani ni miongoni mwa nguzo tano za Uislamu hivyo katika kipindi chote cha funga ya Ramadhani, mbali na kufunga mchana anatakiwa azidishe swala mbalimbali na kujiepusha kabisa na maovu.
Mwezi mtukufu wa Ramadhani una thamani na historia kubwa kwa Waislamu kwa sababu ndio mwezi kiliposhuka kitabu kitakatifu cha Kurani katika siku inayoitwa Lai latul Kadir usiku ambao ni bora kuliko miezi 1,000.
Si nia yetu kuanza kuzungumzia kwa undani faida za mwezi wa Ramadhani lakini katika kipindi chote cha mwezi huu tuliona idadi kubwa ya Waislamu wakivaa mavazi ya stara, kutenda matendo mema na kualikana kwenye futari.
Tusingependa Idd el- Fitri iwe mwanzo wa ajali, maasi, vifo na maovu mengi ambayo mara kwa mara tumekuwa tukiyashuhudia kwenye sikuu mbalimbali hapa nchini.
Kwa mujibu wa vitabu vya dini, Mwislamu yeyote akayetenda maovu siku ya leo ni sawa na kufanya dhambi mbele ya Mwenyezi Mungu siku ya kiama.
Tunaamini mafunzo waliyoyapata waumini wa Kiislamu kwenye mwezi mtukufu wa Ramadhani utawasaidia kuishi kulingana na maagizo ya Mwenyezi Mungu na kujiepusha na dhambi mbalimbali.
Tunachukua fursa hii kuwaomba madereva wote wa vyombo vya moto kuchukua tahadhari pamoja na kutoendesha kwa kasi wanapovitumia ili kuepusha ajali zinazozidi kuongezeka kila kukicha.
Wazazi na walezi wasiwaruhusu watoto wao kwenda matembezini, fukwe za bahari na kumbi za disko bila ya uangalizi maalumu.
Tunasema hivyo kwakuwa kila mara tumekuwa tukisikia watoto wakipata madhara kwenye kumbi za disko, kupotea, kuzama baharini na mikasa mbalimbali ambayo chanzo chake ni uangalizi mdogo wa wazazi au walezi.
Kwa wale wanaokwenda matembezini ni vema wakahakikisha majumbani mwao kunakuwa salama kwa kumuacha mtu atakayelinda au kuzifunga vizuri kwa lengo la kuzuia wezi.
Tunaamini kuwa Jeshi la Polisi litazidisha ulinzi katika maeneo mbalimbali ili kuwadhibiti wale wote waliolenga kufanya uhalifu kwenye sherehe za Idd el- Fitri.
Chanzo: Tanzania Daima

MWENYEKITI MUFINDI ADAIWA KUTAFUNA FEDHA ZA KIJIJI

Na Mwandishi Wetu, Mafinga
MWENYEKI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Peter Tweve, maarufu kwa jina la PP, anadaiwa kujimilikisha kibali cha uvunaji wa magogo katika shamba la Sao Hill, ambalo ni mali ya Kijiji cha Magunguli, kilichopo Mufindi, mkoani Iringa.

Wakizungumza mjini hapa kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa kijiji hicho walisema PP alijimilikisha kibali hicho kilichokuwa kikiuzwa kwa Sh milioni 15.

Wananchi hao ambao hawakutaka kutaja majina yao, walisema alipokichukua kibali hicho, hakuweka fedha katika akaunti ya kijiji kwa muda kama walivyokubaliana awali.

Walisema kwa muda wa mwaka mmoja sasa kila wanapohoji katika mikutano ya hadhara kuhusu kibali hicho wamekuwa wakikamatwa na polisi huku wengine wakitishiwa maisha.

Walisema mwaka jana, Wizara ya Maliasili na Utalii iligawa magogo yenye mita za ujazo 500 kwa kila kijiji kinachozunguka shamba la Sao Hill na hatimaye vijiji vivune magogo hayo na kupata fedha kwa ajili ya maendeleo na jumla ya vijiji 12 vilipata mgawo huo.

Habari zinasema kutokana na vijiji kutokuwa na uwezo wa kuchana magogo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Evarista Kalalu, aliitisha mkutano wa viongozi wa vijiji hivyo na kuwapatia bei elekezi kulingana na thamani ya mita za magogo walizopewa ambapo walitakiwa kuuza kibali kuanzia Sh milioni 13 na si chini ya hapo.

Aliwataka viongozi wa vijiji ambavyo havina akaunti katika benki wafungue haraka na watakapouza vibali hivyo fedha ziwekwe katika akaunti hizo.

Hata hivyo, wakazi wa Kijiji cha Magunguli wanasema fedha hizo hazijaingizwa katika akaunti yao hadi sasa.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Camillus Suta, alikiri kibali hicho kuchukuliwa na diwani huyo na kuhusu malipo, alisema tayari diwani huyo amekwishatoa Sh milioni nane ambazo zimetumia kujenga ofisi ya masijala ya kijiji hicho kwa ajili ya kutunza kumbukumbu za hati za ardhi za kimila.

Kauli ya mwenyekiti huyo ilipingana na maelezo ya wananchi kuwa jengo la ofisi hiyo ambalo halijakamilika limejengwa kwa nguvu za wananchi na mfadhili wao Jacob Mwajombe, anayeishi Dar es Salaam.

“Ni kweli mfadhili wetu Mwajombe alitoa shilingi milioni tatu, lakini fedha za diwani shilingi milioni nane na elfu arobaini zimetumika kununua bati wakati matofali na mawe ni nguvu za wananchi, jengo hili limetumia shilingi milioni 15,” alisema.

Kwa upande wake, PP alikiri kumiliki kibali cha kijiji hicho, lakini akasema wanaolalamika ni wale wanaopinga maendeleo.
Chanzo: Mtanzania

TAKUKURU YABURUZA MAHAKAMANI VIONGOZI WA KIJIJI NJOMBE

Festus Pangani, Njombe Yetu
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Wilayani Njombe jana imewafikisha mahakamani viongozi watatu wa Mtaa wa Wikichi Kata ya Ramadhani Akiwemo Afisa Mtendaji wa Kijiji Hicho Bw Zabron Mgeyekwa.
Akisoma Hati ya Mashtaka Mahakamani Hapo, Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Wilayani Njombe Richard Marekani Amewataja Watuhumiwa Wengine Kwenye Kesi Hiyo Kuwa ni Pamoja na Willy Ngaro Aliekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Msingi Wikichi na Emmanuel Mwalongo Aliekuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Wikichi
Akifafanua Zaidi Mahakamani Hapo Mwendesha Mashtaka Huyo Ameiambia Mahakama Kuwa Mnamo Mwaka 2007 Kwa Pamoja Wakiwa ni viongozi wa kijiji waliwatoza wananchi wa kijiji hicho Michango ya Zaidi ya shilingi laki mbili Huku stakabadhi ya malipo Ikionesha Kuwa Michango Iliyochangwa ni Shilingi Elfu 38 Tu.
Kesi Hiyo iliahirishwa Hadi Agost 23 Baada ya Watuhumiwa Kukana kuhusika na Makosa Hayo na Hivyo Kurudishaw Mahabusu Baaada ya Kukosa Wadhamini.

Akizungumza Nje ya Mahakama Hiyo Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Wilaya ya Njombe Richard Marekani Amesema Watuhumiwa hao Kwa Pamoja Wanatuhumiwa Kwenda Kinyume na Sheria ya Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007.
Katika Hatua Nyingine Taasisi ya Kuzuia n Kupambana na Rushwa TAKUKURU Wilayani Njombe imewataka Wananchi Kuendelea Kushirikiana na Taasisi Hiyo Katika KUwafichua na KUwataja Watu Wanojihusisha na vitendo Vya Rushwa Kama Njia ya Kusaidia Kupunguiza Tatizo la Rushwa Mkoani Hapa
Blogzamikoa

WENYE ULEMEVU WAHIMIZWA KUJITOKEZA KUHESABIWA


Festus Pangani, Njombe
Mkuu wa Mkoa wa Njombe Kaptein Mstaafu Aseri Msangi ameitaka jamii kutoa taarifa sahihi za watu katika Kaya husika ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za watu wenye ulemavu wakati wa zoezi la sense ya watu na makazi.

Katain Msangi aliyasema hayo jana wakati akifungua semina na wawakilishi wa watu wenye ulemavu kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Njombe juu ya Umuhimu wa sensa ya watu na makazi.

Aliwataka wakuu wa kaya wakuu wa Kaya kutoa ushirikiano kwa makarani wa sensa wakati wa zoezi hiilo linalolenga kupata takwimu sahihi kwa maendeleo ya nchi.
Alisema kuwa ni vyema kuandaa taarifa kamilia za kaya zao endapo hawatakuwa nyumbani siku ya zoezi hilo ili kuondoa usumbufu na upotoshaji wa habari ambao unaweza kujitokeza kutokana na kukosekana kwao katika kaya zao wakati wa zoezi.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mkuu wa Wilaya ya Njombe Sarah Dumba amewataka watu wenye ulemavu kuelewa kuwa sensa ya watu na makazi ni haki ya kila mtu hivyo wawe tayari kwa kuhesabiwa.

Sensa ya watu na makazi hufanyika kila baada ya miaka kumi ambapo kwa mwaka huu inatarajiwa kufanyika kwa siku saba kunzia Agosti 26 Mwaka Huu.
Blogzamikoa

RC NJOMBE AAGIZA KUFUKUZWA KAZI WATENDAJI WAZEMBE LUDEWA

Mkuu wa mkoa wa Njombe Kapten Aseri Msangi, akiapa mbele ya Raisi Kikwete.
Nickson Mahundi, Ludewa
Mkuu wa mkoa wa Njombe Kapten Aseri Msangi aliuagiza uongozi Halmashauri ya wilaya ya Ludewa kuwachukulia hatua za kisheria wafanyakazi wazembe ndani ya wilaya hiyo kutokana na kusababisha hati chafu ya hesabu za Serikali.
Kauli hiyo ilitilewa jana katika ziara yake wilayani Ludewa kutokana na ripoti chafu iliyotolewa  Mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za Serikali(CAG) kwa wilaya hiyo kutokana na uzembe wa baadhi ya wafanyakazi uliopelekea upatikanaji wa hati hiyo.

Kapten Msangi alisema asingependa wilaya za mkoa wake kupata hati chafu kwa uzembe wa baadhi ya wafanyakazi.
“Sijapenda na sitopenda ndani ya Mkoa wa Njombe kuwepo kwa uzembe wa namna hiyo kwani nitaonekana sifanyi kazi hivyo ninachohitaji ni kuanza na hawa wazembe waliopelekea upatikanaji wa hati chafu kuchukuliwa hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wilaya nyingine” alisema Kapten Msangi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauli hiyo Mathei Kongo alikiri kuwepo kwa uzembe huo miongoni mwa wafanyakazi na kuahidi kulifanyia kazi suala hilo ili lisijirudie katika wilaya ya Ludewa.
Kongo alisema kumekuwepo kwa ukiukwaji wa malipo na ukusanyaji wa fedha za Halmashauri katika miradi na vyanzo nya mapato katika maeneo mbalimbali hiyo ni sababu kubwa ya upatikanaji wa hati chafu.
Hivi karibuni ofisi ya mkaguzi mkuu na mdhibiti wa hesabu za Serikali (CAG) ilitoa hati chafu kwa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa kwa kushindwa kufikia malengo katika manunuzi na ukusanyaji wa fedha mbalimbali.
Katika hatua nyingine Kapten Msangi aliwataka Madiwani na viongozi mbalimbali kuhimiza kilimo cha Kahawa, Mahindi na ufugaji Kuku na Nyuki kwaajili ya asali ambapo itakuwa ni ukombozi kwa wananchi wa wilaya ya Ludewa.
Alisema watanzania wamekuwa wakiilalamikia Serikali kuwa maisha yamekuwa magumu bila kujua kuna fursa nyingi zikiwemo za ufugaji wa nyuki na kilimo ambazo zinaweza kumfanya kila mwananchi kuishi maisha bora.
Alisema vijana wamekuwa wakikaa bila kufanya kazi wakisubiri maisha bora na kuhamahama vyama ili kupata maisha bora hilo sio suruhisho la maisha bora bali maisha bora yanamtaka kila mmoja kufanya kazi kwa bidii.
Kuhusu pembejeo za kilimo Kept Msangi alisema kumekuwa na wizi mkubwa kwa wazabuni wasio waaminifu hivyo Serikali inaandaa utaratibu wa kuzipitisha Pembejeo hizo katika vyama vya msingi, Saccos na Vikoba ili kuondoa uchakachuaji.
Nae Mkuu wa wilaya ya Ludewa Juma Madaha alikili kuwepo kwa uchakachuaji wa pembejeo za kilimo kwa baadhi ya wazabuni na watendaji wa kata na vijiji wasio waadirifu hivyo hatua za kisheria zinafuata dhidi yao.
Kapten.Msangi aliwataka viongozi wa wilaya hiyo kuhimiza kilimo kwa haitakubarika kuwaruhusu wawekezaji wa kichina kufanya shuguri za kilimo katika wilaya hiyo ili kuwawezesha wakulima kujiinua kiuchumi.
Blogzamikoa

MBUNGE AWATAKA WANANCHI KUSHIRIKIANA

Festus Pangani, Njombe
Wito umetolewa kwa wananchi wa Mkoa wa Njombe kuungana katika kupambana na umasikini kwa kuanzisha miradi mbalmbali yenye manufaa kwao na taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Mbunge wa Viti Maalumu vijana Mkoa wa Dar es Salaam Neema Mgaya wakati wa semina iliyotolewa kwa umoja wa wanawake UWAT mkoani humo iliyoandaliwa na Taasisi ya Povert Reduction in Tanzania PRT.
Mbunge huyo amesma kuwa kuanzishwa kwa taasisi hiyo mkoani Njombe itahamasisha maendeleo ikiwa vikundi vitaungana pamoja na kuunda nguvu ya pamoja kwa kukopeshana fedha za kufanya miradi mbalimbali.
Akizungumza katika semina hiyo Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa taasisi hiyo Ally Manjesi amesema, kuanzishwa kwa taasisi hiyo ni mwanzo wa harakati za kujikomboa kwa wananjombe.
Taasisi ya Povert Reduction in Tanzania PRT imeanzishwa mwezi julai mwaka huu na inakusudia kufanya kazi ndani ya mikoa ya Tanzania bara.
Blogzamikoa

WANANCHI NJOMBE WAHAMASISHWA KUWEKEZA KATIKA SOKO LA HISA

Festus Pangani, Njombe yetu
BENKI ya wananchi Njombe (NJOCOBA) Mkoani Njombe, imehamasisha wananchi kununua hisa na kufanikiwa kuuza jumla ya hisa 55,000 zenye thamani ya sh. milioni 55, zilizofikisha jumla ya hisa 442,000 zenye thamani ya sh. milioni 442 katika kipindi cha mwaka 20111.

Akifafanua juu ya mtaji wa benki hiyo, Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi Bi. Twilumba Ulaya amesema, mapato katika benki hiyo kwa kipindi cha mwaka mwaka 2010/11 ilikuwa sh.bilioni 1.8 kwa akaunti zote.

Katika kipindi hicho mapato ya benki yalikuwa sh. milioni 554, ambapo faida ilikuwa sh.milioni 10, ingawa hasara ilikuwa sh. milioni 289 iliyotokana na gharama kubwa uendeshaji ambazo benki kuu iliamuru zihesabike kama manunuzi ya awali wakati benki hiyo inafunguliwa.

Hadi kufikia Desemba mwaka jana  benki hiyo imetoa mikopo ilikuwa imetoa mikopo yenye thamani ya sh. bilioni 3.6 urejeshaji wake umekuwa mbaya ambapo hadi wakati huo mikopo yenye thamani ya sh. milioni 267 sawa na silimia 18, haijarejeshwa. 

Blogzamikoa

WANANCHI NJOMBE WAITAKA CCM KUTEKELEZA AHADI ZAKE.


Mwandishi wetu, Njombe

WANANCHI wa Kata ya Kitandililo halmashauri ya Mji wa
Makambako Mkoani Njombe, Wameutaka uongozi wa Chama cha
Mapinduzi kutekeleza ahadi ambazo waliahidi ili kuondoa kero 
ambazo wanakabiriwa nazo.

Wakizungumza katika mkutano uliofanyika katika kata hiyo,
wananchi hao wamlalamikia huduma ambazo hazikidhi mahitaji yao 
ambapo wazee, watoto na wanawake wajawazito wamekuwa akilipia 
huduma za afya, pamoja na kukosekana kwa pembejeo kwa wakati 
katika msimu wa kilimo.

Upande wake m/kiti CCM wa Wilaya hiyo, Adamu Msigwa 
amewataka viongozi wa vijiji na kata kuhakikisha wanashiriki 
katika kusimamia shughuli za maendeleo.

Viongozi wa ccm Wilaya ya Njombe walifanya ziara ya kukagua 
miradi ya maendeleo katika Vijiji na kata za Kitandililo na Mahongole kama kutekeleza ilani ya ccm kuhakiki na kutathimini 
fedha za wananchi na halmashauri ikiwa zinatumika ipasavyo.

Blogzamikoa

RC NJOMBE: TUMIENI VYEMA BENKI ZA WANANCHI




Mwandishi wetu, Njombe


WANANCHI mkoani Njombe, wametakiwa kutumia vema benki ya wananchi (NJOCOBA) ili kujipatia mikopo na kukuza uchumi wao badala ya kutumia taasisi nyingine za kifedha ambazo riba ya mikopo yao ni kubwa na haziwasaidii kujikwamua kiuchumi.

Akiwahatubia wananchi waliohidhuria mkutano huo wa mwaka, mkuu wa mkoa wa Njombe, Aseli Msangi amewataka kuweka akiba na kununua hisa pamoja na kulipa mikopo kwa wakati.


Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi Twilumba Ulaya amesema, ili kuboresha huduma kwa wananchi benki hiyo imelenga kuwafikia wakazi wa wilaya za makete, Ludewa na kuhudumia mkoa mzima badala ya wilaya pekee.

Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Michael Ngwira ameeleza mafanikio na changamoto zinazoikabili benki hiyo na jinsi ambavyo amejipanga kukabiriana nazo.

Hadi kufikia Desemba mwaka jana benki hiyo imetoa mikopo ilikuwa imetoa mikopo yenye thamani ya sh. bilioni 3.6

urejeshaji wake umekuwa mbaya ambapo hadi wakati huo mikopo yenye thamani ya sh. milioni 267 sawa na silimia 18,
haijarejeshwa. 


Blogzamikoa

WANANCHI LUDENDE WALIA UKOSEFU WAHUDUMU WA AFYA.


Festus Pangani, Njombe Yetu Blog
Wananchi wa Kata ya Ludende wilayani Ludewa katika Mkoa wa Njombe wameulalamikia uongozi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa kushindwa kupeleka wahudumu wa afya katika Zahanati Ludende hali inayosababisha adha kubwa kwa wakazi wa kata hiyo.
Pamoja na Zahanati hiyo kufunguliwa wakati wa maadhimisho ya miaka hamsini ya uhuru wa Tanzania mwaka jana lakini hakuna mfanyakazi hata mmoja na kwamba majengo ya zahanati hiyo ikiwa ni pamoja na nyumba ya mganga mkuu vimetelekezwa.
Akiongea kwa sharti la kutotajwa jina lake, mmoja wa wananchi hao alisema kuwa haoni sababu ya kuwa na majengo mazuri yaliyojengwa kwa kodi ya wananchi bila ya kuwepo wahudumu wa afya huku wananchi wakiendelea kuumia.
Mtendaji wa Kata ya Ludende, Lezile Luoga alikiri kutokuwepo kwa mfanyakazi yeyote katika Zahanati hiyo na mpaka sasa hakuna maelezo ya kina yanayohusu upatikanaji wa wafanyakazi katika Zahanati hiyo.
Luoga alisema wananchi wamekuwa wakijitolea kufanya maendeleo ya ujenzi wa Zahanati hiyo cha kushangaza wamekuwa wakipata huduma za matibabu katika Zahanati za vijiji vya mbali wakati dhahanati yao iko katika ubora unaokubalika.
“Tumewahamasisha wananchi kuchangia ujenzi wa zahanati hii hadi imekamilika lakini cha kushangaza Serikali imeshindwa kuleta wafanyakazi, hii inakatisha tamaa na wananchi wanaweza wasijitolee kufanya kazi za kimaendeleo” alisema Luoga.
Naye Makamu Mkuu wa shule ya Sekondari Ikovo, Menrufu Mgaya alisema ukosefu wa huduma ya afya umeleta usumbufu kwa wanafunzi wa shule yake hasa pale yanapotokea magonjwa ya milipuko yanayowakumba wanafuzi kutokana na ukosefu wa maji safi na salama.
Blogzamikoa

BARABARA YA NJOMBE-LUDEWA YATENGEWA FEDHA


Festus Pangani, Dodoma

Hatimaye Serikali imesikia kilio cha Mbunge wa Ludewa, Mhe. Deo Filikunjombe (CCM) cha kuitaka barabara ya Njombe, kupitia Ludewa hadi Manda ijengwe kwa kiwango cha lami.

Akijibu Swali namba 264 bungeni jana, Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Gerson Lwenge, alisema kufuatia ombi la Filikunjombe, katika mwaka huu wa fedha wa 2012/2013, tayari Serikali imetenga shilingi 1,600 millioni kwaajili ya kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina barabara hiyo kwaajili ya ujenzi wa kiwango cha lami.

“Aidha, katika kuhakikisha barabara ya Ludewa inatengenezwa na kupitika kwa urahisi,” alisema jumla ya shilingi milioni 800 zingine zimetengwa katika bajeti hii ya 2012/2013 kwaajili ya matengenezo maalum ya barabara kuu kwa kiwango cha changarawe.

 “Lengo ni kuifanya barabara ya Njombe - Ludewa iweze kupitika katika majira yote ya mwaka,” alisema Waziri Lwenge aliyekuwa akijibu swali kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi - Mhe. John Pombe Magufuli.

 “Ujenzi wa barabara ya lami toka Njombe, kupitia Ludewa hadi Manda ni nuru mpya ya matumaini kwa wana Ludewa wote,” alisema Bwn. Filikunjombe akiongeza kuwa “barabara ya lami itachochea kasi kubwa ya Maendeleo katika wilaya ya Ludewa.”

Filikunjombe amemshukuru na kumpongeza Dr. Magufuli kwa kuwafanya wana Ludewa nao wanufaike na matunda ya miaka 50 ya uhuru wa nchi yetu. “Kwa niaba ya wananchi wa Ludewa ninakushukuru sana mhe. Waziri kwa kuitazama Ludewa kwa jicho la pekee,” alisema Filikunjombe. 

Katika mwaka 2011/2012 Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara, ilianza kujenga kwa kiwango cha lami kilomita 1.5 Ludewa Mjini na ujenzi bado unaendelea.

Barabara ya Njombe – Ludewa – Manda yenye urefu wa km 212 ni barabara kuu itakayohudumiwa na wakala wa barabara – TANROADS - mkoa wa Njombe.

Blogzamikoa

Karibu Mkoa Mpya wa Njombe



Mkoa mpya wa Njombe
Mkoa wa Njombe ni moja kati ya mikoa mipya Tanzania, ukiwa umeanzishwa rasmi mwaka 2012. Umepakana na mikoa ya jirani ya Morogoro, Ruvuma, Mbeya na Iringa.
Mwaka 2002 katika eneo hilo kulikuwa na wakazi 654,929 [1] katika wilaya zifuatazo: Makete (wakazi 106,061), Njombe (wakazi 420,348), Ludewa (wakazi 128,520).
Kutokana na hadhi mpya, wilaya ya Njombe imegawanyika kati ya ile ya mjini na ile ya vijijini. Pia imeanzishwa wilaya ya Wanging'ombe.
Makao makuu yako Njombe mjini.
Wenyeji wa mkoa ni hasa kati ya makabila yafuatayo: Wabena, Wakinga, Wapangwa, Wawanji, Wakisi na Wamanda.



 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa