Home » » BARABARA YA NJOMBE-LUDEWA YATENGEWA FEDHA

BARABARA YA NJOMBE-LUDEWA YATENGEWA FEDHA


Festus Pangani, Dodoma

Hatimaye Serikali imesikia kilio cha Mbunge wa Ludewa, Mhe. Deo Filikunjombe (CCM) cha kuitaka barabara ya Njombe, kupitia Ludewa hadi Manda ijengwe kwa kiwango cha lami.

Akijibu Swali namba 264 bungeni jana, Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Gerson Lwenge, alisema kufuatia ombi la Filikunjombe, katika mwaka huu wa fedha wa 2012/2013, tayari Serikali imetenga shilingi 1,600 millioni kwaajili ya kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina barabara hiyo kwaajili ya ujenzi wa kiwango cha lami.

“Aidha, katika kuhakikisha barabara ya Ludewa inatengenezwa na kupitika kwa urahisi,” alisema jumla ya shilingi milioni 800 zingine zimetengwa katika bajeti hii ya 2012/2013 kwaajili ya matengenezo maalum ya barabara kuu kwa kiwango cha changarawe.

 “Lengo ni kuifanya barabara ya Njombe - Ludewa iweze kupitika katika majira yote ya mwaka,” alisema Waziri Lwenge aliyekuwa akijibu swali kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi - Mhe. John Pombe Magufuli.

 “Ujenzi wa barabara ya lami toka Njombe, kupitia Ludewa hadi Manda ni nuru mpya ya matumaini kwa wana Ludewa wote,” alisema Bwn. Filikunjombe akiongeza kuwa “barabara ya lami itachochea kasi kubwa ya Maendeleo katika wilaya ya Ludewa.”

Filikunjombe amemshukuru na kumpongeza Dr. Magufuli kwa kuwafanya wana Ludewa nao wanufaike na matunda ya miaka 50 ya uhuru wa nchi yetu. “Kwa niaba ya wananchi wa Ludewa ninakushukuru sana mhe. Waziri kwa kuitazama Ludewa kwa jicho la pekee,” alisema Filikunjombe. 

Katika mwaka 2011/2012 Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara, ilianza kujenga kwa kiwango cha lami kilomita 1.5 Ludewa Mjini na ujenzi bado unaendelea.

Barabara ya Njombe – Ludewa – Manda yenye urefu wa km 212 ni barabara kuu itakayohudumiwa na wakala wa barabara – TANROADS - mkoa wa Njombe.

Blogzamikoa

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa