Home » » WAATHIRIKA WA VVU WILAYANI MAKETE WASUSA KUNYWA DAWA ZA ARV

WAATHIRIKA WA VVU WILAYANI MAKETE WASUSA KUNYWA DAWA ZA ARV

Mkuu wa wilaya ya Makete Josephine Matiro akihutubia kwenye maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani katika kata ya Mbalatse wilaya ya Makete 
 Wakazi wa Mbalatse wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Makete akitoa hotuba yake
 Diwani wa kata ya Mbalatse Sikumu Msigwa akisoma Risala ya wanaoishi na VVU mbele ya mgeni rasmi
 Akimkabidhi mkuu wa wilaya hotuba yao.
*********
Na Edwin Moshi
Pamoja na jitihada za kuhakikisha kila pembe ya nchi hii dawa za kupunguza makali ya VVU zinapatikana kwa urahisi, kioja kimejitokeza wilayani Makete mkoani Njombe kwa baadhi ya wanaoishi na virusi vya ukimwi ambao walikuwa wanatumia dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo (ARV) kuacha kutumia dawa hizo kwa makusudi

Pamoja na hayo wengine wanakataa kuzinywa dawa hizo licha ya kushauriwa na wataalamu wa afya kuanza kutumia kutokana na afya zao kuanza kuzorota

Hayo yamebainika katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani yakliyoadhimishwa kiwilaya katika kata ya Mbalatse wilayani Makete mkoani Njombe

Akisoma risala ya wanaoishi na virusi vya UKIMWI katika kata ya Mbalatse, diwani wa kata hiyo Mh. Sikumu Msigwa amesema miongoni mwa mambo yanayosababisha kasi ya maambukizi mapya ya VVU katani hapo ni pamoja na mila potofu za kurithi wajane na wagane, wanaume kuoa wake wengi, ngono zembe, wenye vvu kukataa kutumia dawa za kupunguza makali ya virusi na kujiingiza katika ulevi wa kupindukia na kufanya ngono bila kondomu

Akihutubia mamia ya wakazi wa Mbalatse waliofika kwenye maadhimisho hayo mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Makete Josephine Matiro amekemea vitendo vinavyochangia ongezeko la VVU ikiwemo kuwasihi waviu kutumia dawa za kupunguza makali ya VVU kama walivyoshauriwa na wataalamu wa afya ili waimarike afya zao na wazidi kujenga nguvu kazi ya Taifa

Amesema endapo watatumia dawa hizo kwa usahihi upo uwezekano wa kuishi zaidi ya miaka 20 na wakaendelea kufanya shughuli zao kama kawaida, ikiwemo kuitunza familia ambayo inamtegemea kwa kiasi kikubwa

"Ukitumia arv ndugu zangu lazima maisha yako yatakuwa marefu, na uzuri serikali yetu inawajali wananchi wake na dio maana hizo dawa zinafika mpaka huku, kwa kweli naombeni tubadilike, mkoa wetu ndio unaoongoza kitaifa, lakini bado jitihada tunatakiwa sisi ndio tuongeze, tukikubali kubadilika sisi, hata hizi kampeni za kupamban na VVU zitafanikiwa sana" alisema Matiro

Maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani huadhimishwa Desemba Mosi ya kila mwaka, ambapo mwaka huu kauli mbiu ilikuwa Tanzania bila maambukizi mapya ya VVU, na vifo vitokanavyo na UKIMWI inawezekana



0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa