MBUNGE
wa zamani wa Njombe, Yono Stanley Kevela amechaguliwa kuwa Kamanda wa
Umoja wa Vijana wa UVCCM wa Wilaya ya Wanging’ombe katika mkoa mpya wa
Njombe.
Kevela ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Njombe kati ya mwaka 2005-2010
anatarajiwa kusimikwa rasmi kwenye nafasi hiyo keshokutwa mkoani Njombe.
Akizungumza na gazeti hili mara baada ya uteuzi huo, Kevela
aliwashukuru viongozi wote wa CCM kwa kumwamini na kusema kuwa amebaki
na deni kubwa la kukitumikia chama hicho kwa uadilifu na uaminifu
mkubwa.
“Nawashukuru wanaCCM wenzangu kuanzia ngazi ya mabalozi, tawi, kata,
wilaya, mkoa hadi taifa kwa kuona ninafaa kukitumikia chama changu
kwenye nafasi hii, nimebaki na deni la kukitumikia chama changu kwa
unyenyekevu mkubwa na naahidi sitawaangusha,” alisema.
Kevela ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Yono Auction Mart,
alisema wanachama wote wa CCM washikamane kutekeleza ilani ya chama chao
na kuiga mfano wa Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete namna
anavyotekeleza ahadi kwa vitendo.
“Mheshimiwa Rais Kikwete ametekeleza ahadi zake kwa kiwango kikubwa
sana, ameipaisha Tanzania chati katika anga za kimataifa, hivyo
wanachama wengine lazima tufuate nyayo zake kwa kuchapa kazi na
kukiimarisha chama, tusitegeane, kila mwanachama atimize wajibu wake,”
alisema Kevela ambaye anasomea Shahada ya Uzamivu (PhD), katika Masoko,
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Pia alisifu ziara zinazofanywa na Katibu Mkuu wa chama hicho,
Abdulrahman Kinana na timu yake katika mikoa mbalimbali kuwa ni hatua
nzuri ya kukiimarisha na kukijenga chama hicho.
Kevela aliwashangaa baadhi ya viongozi wa chama hicho wanaojigeuza
miungu watu kwa kushindwa kuwasikiliza wanachama wanapokuwa na kero
mbalimbali.
“CCM ni ya wanachama, na viongozi hawapaswi kuwapuuzia wanapokuwa na
jambo badala ya kujigeuza miungu watu na kuendesha mambo wanavyotaka
wao,” alisema Kevela huku akisisitiza kwamba wapinzani wataambulia
patupu uchaguzi wa 2015 kutokana na namna CCM inavyotekeleza ahadi zake
kwa wananchi.
Alisema atatumia nafasi hiyo kuwasaidia vijana kupata fursa
mbalimbali za kiuchumi kwenye taasisi za fedha ili waweze kupata fedha
za kufanya ujasirimali na biashara hivyo kujiondoa kwenye lindi la
umaskini.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment