Home » » ABIRIA WALIOKUWA WAKISAFIRI NA BASI LA UKINGA EXPRESS WANUSURIKA KIFO KUFUATIA AJALI MBAYA WILAYANI MAKETE

ABIRIA WALIOKUWA WAKISAFIRI NA BASI LA UKINGA EXPRESS WANUSURIKA KIFO KUFUATIA AJALI MBAYA WILAYANI MAKETE


 Muonekano wa Basi la Ukinga Express likiwa kwenye eneo la ajali.
Abiria waliokuwa wakisafiri kwa basi la Ukinga Express kutoka Njombe kwenda Makete mkoani Njombe, wamenusurika kifo baada ya basi hilo walilokuwa wakisafiria kuigonga fuso kwa nyuma iliyokuwa imepata hitilafu na kuegeshwa barabarani

Ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia leo katika eneo linalohofiwa na wengi la Lwamadovela kata ya Tandala wilayani Makete, baada ya dereva wa basi hilo kuigonga kwa nyuma fuso hiyo ambayo ilipata hitilafu kwenye eneo lenye kona

Wakizungumza na mwandishi wa eddy blog aliyefika eneo la tukio na kushuhudia ajali hiyo, mashuhuda hao bila kutaja majina yao wamesema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa basi hilo kushindwa kulimudu gari lake licha ya kuwepo na kona kali, lakini pia mwenye fuso alishindwa kuweka ishara za kutosha kuonesha kama gari lake limepata hitilafu barabarani

"Unajua braza(akimaanisha kaka) dereva huyu wa hili basi alikuwa mwendo na ndio maana ghafla alipoanza kukunja kona akakutana na hii fuso mbovu, kwa kuwa alikuwa na mwendo kasi ilikuwa ngumu kushika breki ingawa alijitahidi kama unavyoona lakini ilishindikana, ndipo akaigonga hii fuso kwa nyuma" alisema shuhuda huyo

wamesema kutokana na ajali hiyo, baadhi ya abiria walipata majeraha hasa waliokuwa wamekaa viti vya mbele, ingawa mashuhuda hao hawakujua mara moja ni idadi ya abiria wangapi wameumia na hali zao zikoje

Hadi mwandishi wetu ambaye alikuwa akipita eneo hilo kuendelea na safari na kukutana na tukio hilo anaondoka eneo hilo, polisi walikuwa wakisubiriwa kuja kupima na kufanya taratibu za kijeshi kuhusu ajali hiyo, hivyo kuacha wananchi waliokuwepo eneo hilo wakiwasubiri

Ikumbukwe kuwa eneo hilo lililotokea ajali hiyo halina mtandao wa simu, hivyo aliyekuwa akitaka mawasiliano alikuwa akitembea umbali mrefu kutafuta mtandao, hali inayodaiwa kuchelewesha kufikisha taarifa hizo kwa polisi Makete mjini
Chanzo ni Edwinmushi.com

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa