Home » » Wavurugaji wa Katiba ,walimtaka JK asaini mswada pasipo kuangalia bada ya kutokuwepo nchini.

Wavurugaji wa Katiba ,walimtaka JK asaini mswada pasipo kuangalia bada ya kutokuwepo nchini.

WAZALENDO NET..
JK awatibulia Wassira, Chikawe • Filikunjombe asema wanapaswa kuwaomba radhi wananchi
na Waandishi wetu
HATUA ya Rais Jakaya Kikwete kukutana na viongozi wa vyama vya siasa vyenye wabunge na kuridhia muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba urejeshwe bungeni, imeungwa mkono na wengi, huku mawaziri wake wakisutwa.
Mawaziri hao ni Stephen Wassira (Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu), Mathias Chikawe (Katiba na Sheria) na William Lukuvi wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge).
Kwa nyakati tofauti baada ya vyama vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi, kususia muswada huo bungeni waliwakejeli wakidai kuwa wanapoteza muda kwani safari hii hakuna nafasi ya kukutana na Rais Kikwete kama ilivyokuwa awali mwaka 2011.
Mawaziri hao waliongeza kuwa viongozi wa upinzani wanatamani kwenda Ikulu kunywa chai na juisi, huku wakisisitiza kuwa milango hiyo sasa imefungwa na rais lazima asaini muswada huo kama ulivyopitishwa na Bunge, kwamba kutofanya hivyo ni kutangaza mgogoro na wabunge.
Licha ya kejeli hizo, Rais Kikwete aliamua kukutana na viongozi wa vyama hivyo vitatu jana huku akiwashirikisha pia wale wa CCM, TLP na UDP ambao wabunge wao waliupitisha muswada huo.
Akizungumza jana na gazeti hili, Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), alimpongeza rais kwa hatua hiyo na kumtahadharisha awe makini na wabunge wa chama hicho, akidai wamekuwa wakitumia wingi wao vibaya bungeni.
Filikunjombe alisema Kikwete ameonesha ukomavu na kwamba hiyo ndiyo demokrasia ya kuwasikiliza wachache pia.
“Kwenye katiba hakuna mshindi, muswada uliopitishwa si wa CCM, katiba si ya CCM, inapaswa kuwa ya wananchi wote hata wachache wasikilizwe.
“Katiba mpya haikuwa ajenda ya CCM, rais aliichukua labda kutoka chama kingine akaona inafaa. CCM wamepokea suala la mabadiliko ya katiba bila kukubali maumivu yake, ndiyo maana tunafikia hatua hii,” alisema.
Alifananisha hatua hiyo na mtu unayetaka kufika mbinguni halafu hutaki kufa, hivyo kuwataka wenzake wakubali mabadiliko na maumivu yake.
“Mimi ninamtia moyo Rais Kikwete asimamie vizuri suala la katiba, ila ajue wabunge wengi wa CCM tunamharibia, awe makini na sisi, kwani mara nyingi tunatumia wingi wetu vibaya.
“Imekuwa aibu sasa mara ya pili rais anarejesha muswada kufanyiwa marekebisho, ingefaa wabunge wa CCM tujitafakari, sisi tunamtumikia nani?”alihoji.
Filikunjombe aliongeza kuwa katika hilo Kikwete ameonesha amedhamiria kwa dhati kuusimamia mchakato, hivyo aungwe mkono.
Akizungumzia kauli za kejeli za mawaziri, mbunge huyo machachali alisema hao wana akili mgando tu, yafaa wawaombe radhi Watanzania.
“Na hii ni kwa sababu hapa kwetu utamaduni wa kujiuzulu haupo, lakini vinginevyo hizo si kauli za kusemwa na mawaziri,” alisema.
Alipotafutwa Waziri Wassira, kuelezea msimamo wake baada ya mazungumzo ya rais na viongozi wa vyama, alijibu kwa kifupi akiomba aulizwe Waziri Chikawe, kwa maana kwamba yeye hakuwa na la kusema.
Waziri Chikawe naye alipotafutwa, aliomba apigiwe simu baadaye kwa maelezo kuwa hakuwa katika nafasi ya kuzungumza kwa wakati huo.
Ndugai asahau kanuni
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, ambaye alisimamia ubabe wote bungeni hadi muswada kupitishwa na kasoro hizo, alipotafutwa alionesha kushangaa, kwa maana kuwa hajui wapinzani wanabishania nini na walikwenda kumuona rais kwa suala lipi.
“Ni issue (suala) gani hasa ambayo inahitaji udharura wa aina hiyo, unaposema wataurejesha muswada katika Bunge lijalo, je, kanuni zinaruhusu?
“Mimi sioni mantiki yoyote, labda wanaozungumza hoja ya uteuzi wa wajumbe 166, kama rais hataki hilo ni suala jingine, ila sisi tuliona rais ndiye chombo kinachofaa kuchuja wajumbe hao,” alisema.
Kwa mujibu wa Ndugai, bila mamlaka ya kuchuja wanaweza kujikuta wana wajumbe wa kutoka kanda, dini au jinsia moja, kwamba mamlaka ya kuchuja inahitajika.
Kuhusu muswada kurejeshwa bungeni, Ndugai alisema hana uhakika kama utarejeshwa, ila anachofurahi yeye ni kusikia kuwa muswada umesainiwa.
CCM wakubali
Chama Cha Mapinduzi kupitia kwa Katibu wake wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema Rais Kikwete kwa kusaini inaonesha anafuata sheria, lakini pia wanampongeza kwa kukutana na viongozi wa siasa.
Alisema kuwa yale yatakayorejeshwa bungeni, wabunge wataamua kama wakiona yana hoja wasikilize na wakiona hayana watajua wao kwa vile Bunge ni mhimili huru.
Kuhusu kauli za kejeli za baadhi ya mawaziri, Nape alisema hajui na hajawahi kusikia.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), Sadifa Khamisi, alisema Bunge ni chombo huru, hivyo litaangalia kama kuna masuala ya kubadili.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Alexanda Makulilo, kwa upande wake alisema rais ametumia busara kuwasikiliza wapinzani, kwa kuwa aliona wana hoja.
Alisema marekebisho yafanyike, wabunge sasa wakafanye majadiliano vizuri, waone umuhimu wa hoja na waweke masilahi ya vyama pembeni na kutanguliza manufaa ya nchi.
Viongozi wa dini wasifu
Baadhi ya viongzoi wa dini wamemsifu Rais Kikwete kwa hatua ya kukutana na viongozi wa vyama, kwamba kitendo hicho ni pigo kwa mawaziri ambao wameifanya Ikulu kuwa hatimiliki yao.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Mwenyekiti wa kamati ya viongozi wa dini wa taaluma, maadili na haki za binadamu kwa jamii, Mchungaji William Mwamalanga, alisema Kikwete ana nia njema lakini watendaji wake wamekuwa wakimpotosha.
Mwamalanga alisema kuwa hatua hiyo ya kuwa na majadiliano ya pamoja imeonesha ujinga uliokuwa ukifanywa na baadhi ya watendaji ambao wamekuwa wakitoa kauli za kukejeli wapinzani.
“Huwezi kuwa na hatimiliki ya Ikulu, hili ni lazima mawaziri Lukuvi, Chikawe na Wassira wakatambua. Maana hatua ya Rais Kikwete kukutana na viongozi hao imewadhalilisha wao mawaziri,” alisema.
Kiongozi huyo alisema kuwa watendaji hao ndio waliokuwa wakipotosha katika suala hilo na kumlazimisha asaini muswada huo haraka bila kuangalia kasoro.
Alisema kuwa ni muhimu sasa Rais Kikwete akasimamia utekelezaji wa makubaliano hayo ili malengo yaliyowekwa yakaweza kufikiwa.
Mwamalanga alisema kuwa iwapo Rais Kikwete atayaacha makubaliano hayo na kuwaachia watendaji hao kuna uwezekano wa kutokea kwa mtafaruku mkubwa ndani ya nchi katika suala hilo

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa