WAKULIMA wa zao la pareto mkoani Njombe na Iringa,
wameiomba serikali kuingilia kati ununuzi wa zao hilo kutokana na kuwapo kwa
baadhi ya wanunuzi wanaowadhulumu wakulima kwa kuchezesha mizani na kuisafirisha
nje.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakulima hao
wamesema hofu yao ni juu ya kuadimika kwa soko la pareto kama kiwanda kilichopo
kitakosa malighafi kwa muda mrefu na kufungwa, hivyo kutaka wanunuzi wengi wawe
wa ndani.
Walisema miaka ya nyuma kabla ya kuwapo kwa kiwanda
hicho zao la pareto liliyumba kwa kukosa soko lakini tangu kiwepo Kiwanda cha
PCT mjini Mafinga wamekuwa na uhakika wa kuuza zao hilo kwa wakati, tena bila
kukopwa.
“Kuna wanunuzi wengi ambao wakiingia tu wanatangaza
bei kubwa, lakini cha ajabu ukienda kupima kwao unashangaa fedha unayoipata ni
ile ile ambayo inapatikana kwa kiwanda cha Mafinga, hii ina maana kuwa bei yao
ipo juu kwa sababu wanajua kuwa wanachezesha mzani,” alisema Innocent Lukosi,
mkazi wa Kijiji cha Iniho, wilayani Makete.
Aliiomba serikali kuhakikisha kuwa wanunuzi waliopo
wanafuata sheria na taratibu badala ya kusafirisha zao hilo nje ya nchi wakati
likiwa malighafi licha ya kuwepo kwa kiwanda.
Ofisa Tarafa wa Matamba, wilayani Makete, Benedict
Mwageni, alisema wanahitaji ushindani kwenye soko la pareto lakini si kwa
wanunuzi wasiofuata sheria na taratibu.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment