Rais Jakaya Mrisho Kikwete akibofya kitufe huku wazee wa Njombe wakirusha njiwa kuashiria kuzinduliwa rasmi mkoa wa Njombe leo Oktoba 18, 2013 katika Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amesema kuwa Maisha Bora kwa Watanzania hajawezi kuja kwa watu kushinda
wanacheza mchezo wa pool badala ya kujihangaisha kwa kufanya kazi na
shughuli nyingine za kujiingizia mapato.
Aidha,
Rais Kikwete ameahidi kuwa Serikali yake itakomesha haraka iwezekanavyo
kero ya wananchi wa sehemu za Mkoa wa Njombe kulazimika kupanda mitini
ili kupata mawasiliano ya simu za mkononi.
Rais
Kikwete amayesema hayo leo, Ijumaa, Oktoba 18, 2013, wakati
alipohutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Wanginyi, Kata ya
Lupembe, Wilaya ya Njombe katika Mkoa Mpya wa Njombe kwenye siku yake ya
kwanza katika ziara yake ya siku saba kukagua na kuzindua miradi ya
maendeleo katika Mkoa huo.
Akizungumza
na wakazi wa Kijiji hicho na vijiji vya jirani, Rais Kikwete
amezungumzia dhana nzima ya Maisha Bora kwa Watanzania akisisitiza kuwa
maendeleo na Maisha Bora kwa Kila Mtanzania hajawezi kupatikana kwa watu
kushinda wanacheza mchezo wa pool mchana kucha.
“Ndugu
zangu, nimepata kusema huko nyuma na nataka kurudia tena kuwa Maisha
Bora kwa Kila Mtanzania yanawezekana kwa watu kujituma na kuchapa kazi
na siyo kwa watu kushinda kwenye meza za pool wakipiga kale kampira huko
wakiilaumu Serikali na kuulizana ‘Maisha Bora yako wapi?’”
Ameongeza
Rais Kikwete: “Inawezekana kweli Maisha Bora yakaja kwa mtu anayeshinda
anagonga mpira wa pool kwenye meza? Ni kwa kufanya kazi kwa bidii na
shughuli nyingine za kutuingizia kipato ndipo maisha yetu yatakapokuwa
bora.”
Kuhusu
hali ya mawasiliano ya simu Mkoani Njombe, Rais Kikwete, baada ya kuwa
ameambiwa kuwa katika baadhi ya sehemu za Mkoa huo, watu wanalazimika
kupanda juu ya miti ili kupata mawasiliano, alisema kuwa Serikali yake
itakomesha haraka kero hiyo.
“Ni
ajabu na aibu kabisa kwamba watu wanalazimika kupanda miti ili kupata
mawasiliano….Hii ni hatari … kwa sababu mtu anaweza kuanguka na kuvunja
viungo…mtu anaweza kuvunja kiuno,” alisema Rais Kikwete huko watu
wakiangua kicheko.
“Tutahakikisha
kuwa watu hawavunjiki viungo kwa sababu ya kupiga ama kupokea simu za
ndugu zao,” Rais Kikwete amewahakikishia wana-Njombe.
Katika
kufafanua azma hiyo ya Serikali kumaliza kero hiyo, Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa
amesema kuwa Serikali italimaliza tatizo la mawasiliano katika Mkoa wa
Njombe kwa awamu mbili.
Alisema
kuwa katika awamu ya kwanza, kiasi cha sh milioni 260 zimetengwa kwa
ajili ya kuboresha mawasiliano katika vijiji 25 vya Jimbo la Uchaguzi la
Njombe Kaskazini na kuwa kazi hiyo itakuwa imekamilika ifikapo Machi,
mwakani, 2014. “Tunataka watu waache kupanda miti kwa kutafuta
mawasiliano ya simu tu.”
Amesema
kuwa katika awamu ya pili, kiasi cha sh bilioni 1.552 zitatumika kutoka
Mfuko wa Mawasiliano Vijijini kwa ajili ya kuboresha mawasiliano ya
simu katika Mkoa mzima wa Njombe.
Amesema kuwa kazi ya kuboresha mawasiliano katika awamu hiyo ya pili, itakamilika ifikapo Agosti, mwakani, 2014.
Kuhusu
matumizi ya simu zenyewe, Mheshimiwa Mbarawa amewataka Watanzania
kuzitumia simu hizo za mkononi vizuri kwa mawasiliano ya maana na
yasiyokuwa na ovyo ikiwa ni pamoja na kutukana watu. “Tuzitumie simu
zetu vizuri kwa mawasiliano mazuri na ya maana na siyo kutumia simu
kujenga na kusambaza fitina na majungu ama kushiriki matusi dhidi ya
watu wengine.”
Baadaye
jioni, Rais Kikwete alikuwa anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika sherehe
za Uzinduzi Rasmi wa Mkoa wa Njombe kwenye Uwanja wa Sabasaba mjini
Njombe.
Picha na Ikulu