UKARABATI WA BARABARA YA MAKETE - NJOMBE SEHEMU ILIYOHARIBIWA NA MVUA WAANZA


Katapila likiwa eneo lililoharibiwa na maji ya mvua kwenye kipande cha lami barabara kuu ya Makete-Njombe katika kijiji cha Usungilo wilayani Makete tayari kabisa kurekebisha eneo hilo
 Ukarabati ukiendelea, mapipa yakiashiria hapo ndipo sehemu iliyoathiriwa na mvua 
 Huu udongo unaouona haukuwepo baada ya mvua kuusomba hali iliyosababisha eneo hili kumegeka na kumomonyoa lami, na huu ni udongo mpya uliojazwa wakati ukarabati ukiendelea
Kina mama wakiangalia eneo hilo linalofanyiwa ukarabati 
Hapa panapoonekana ndipo palipobomolewa na mvua, hivyo kwa hivi sasa pamejazwa kifusi kabla ya kufanyika utaratibu wa kurejesha lami kama palivyokuwa awali 
Wajameni hiki kibao kitasomeka kweli hasa kwa madereva ambao hawajui kama ujenzi unaendelea jirani? maana hii rangi waliyotumia kuandikia duuuuuu!
(Picha zote na Edwin Moshi)

Mkuu wa wilaya ya Makete Josephine Matiro Makete asisitiza amani




 Mkuu wa wilaya ya Makete Josephine Matiro

Na Edwin Moshi
Serikali wilayani Makete imewataka wananchi wa wilaya hiyo kuwa makini na kutoa taarifa kwa viongozi pale wanapokiona kitua ambacho hawakifahamu ama wanapomuaona mtu ama watu wageni ambao hawawafahamu katika maeneo yao

Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ikiwa ni siku kadhaa zimepita tangu kulipuka kitu kinachosadikika kuwa ni bomu katika kanisa moja jijini Arusha

Matiro amesema kufuatia tukio hilo lililotokea Arusha hakuna budi wananchi kuwa makini kwa kuwa kumekuwa na muingiliano wa watu ambao wanafika kwenye wilaya yake na wengi wao wakiwa wageni lakini hawatoi taarifa na pia hakuna mtu mwingine ambaye anatoa taarifa kuwa kuna watu wageni ambao hawafaamiki na wameingia kwenye eneo hilo

Amesema si lazima watu ama mtu huyo afike kwako lakini endapo ataonekana hata kwa jirani ni lazima utoe taarifa ili ahojiwe na kujulikana ametoka wapi.

“zamani kulikuwa na utaratibu mzuri ambao hivi sasa tutaurejesha, watu walikuwa hawakubali kumpokea mtu yeyote mgeni bila taarifa zake kujulikana wazi ikiwemo kwa viongozi, lakini hivi sasa hicho kitu hakipo” alisema Matiro

Katika hatua nyingine mkuu huyo amewataka wale wote wenye kanda ama CD zenye uchochezi wa kidini kuzisalimisha kwenye vyombo vya usalama kwa kuwa ni kosa kisheria na atakayekamatwa nazo atachukuliwa hatua za kisheria

Amesema cd hizo zinachochea uvunjifu wa amani na zitaweza kupelekea vita ya kidini ambyo ni vita hatari kuliko zote, hivyo kuwataka wenye nazo kuzipeleka wenyewe kwenye vyombo vya usalama na kusisitika kila mtu kulilinda amani iliyopo wilayani mwake isivunjike

Mwanafunzi ajinyonga Njombe

WATU watatu wamekufa mkoani Njombe katika matukio tofauti likiwemo la ajali iliyosababisha mwanafunzi kupoteza maisha  na wengine wawili kujinyonga.

Kamanda wa polisi mkoani Njombe kamishna msaidizi wa polisi Fulgence Nginyani amesema katika tukio la kwanza, la april 19 saa 11 jioni katika maeneo ya uwanja wa polisi makambako, mwanafunzi aliyetambuliwa kwa jina la jina la Helen Mwitula (9) mwanafunzi wa shule ya msingi Mwembetogwa  darasa la tatu alikufa baada ya kugongwa na gari.

Kamanda Ngonyani amesema,ajali hiyo ilisababishwa na gari lenye namba T. 809 BHC double Cabin pick-up mali ya kampuni ya Jah- People investment  Ltd. ya mjini makambako lililokuwa likiendeshwa na dereva Seily Mtafya (28) ambapo katika ajali hiyo hiyo,mwanafunzi mwingine Joyce mwakipesile (9) amelazwa katika hospitali ya kkkt ilembula baada ya kuvunjika miguu yote miwili.

Katika tukio jingine april 19 Oktar Mahenge (12) mwanafunzi wa darasa la na tano katika shule ya Lupalilo wilayani Makete alijinyonga hadi kufa kwa kutumia koti la suti nje ya nyumba yao.

Wakati huo huo, Ezekiel Haule (28) mkazi wa kijiji cha Kiwe kata ya Mawengi wilayani Ludewa alikutwa akiwa amekufa baada ya kujinyinga na kamba ya manila porini nje ya nyumba yake chanzo kinachunguza.

Afariki kwa kupigwa na kuvunjwa viungo vya mwili

MTU mmoja mwanaume amekufa wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Wilaya ya Kibena mkoani Njombe, baada ya kukutwa akiwa amepigwa na watu wasio julikana mjini Makambako.

Kamanda wa polisi,kamishna wa polisi mkoani humo, Fulgence Ngonyani, amemtaja mtu huyo kuwa ni Peles Sanga (33) mkazi wa mji mwema makambako ambaye Aprili 10 saa 10 alfajiri alipokutwa katika pipeline akiwa amevunjwa miguu yote miwili, na mkono wa kulia kisha kutelekezwa eneo la tukio.

Kamanda Ngonyani amesema, mtu huyo aliokotwa na wasamalia kisha kufikishwa katika kituo cha afya ambapo alihojiwa na kueleza bayana kuwa alitoka matembezini na kuvamiwa na watu watatu ambao walivalia makoti meusi marefu,ambao baada ya kumjeruhi walitokomea kusiko julikana.

Marehemu alifikishwa kibena na kuanza matibabu ambapo hata hivyo alikufa saa 6 mchana april 11, baada ya  kuvuja damu nyingi katika majeraha, na jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.

HASSAN MAAJAR TRUST YAKABIDHI MADAWATI 680 KWA RC WA NJOMBE.



 Mkuu wa mkoa wa NjombeKaptain Mstaafu Asseri Msangi katika picha ya pamoja na baadhi ya wanafunzi.

 Mkuu wa mkoa wa Njombe Kaptain Mstaafu Asseri Msangi (aliyekaa wa pili kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi Hassan Majaar Trust Bi. Zena Maajar Tenga (waliosimama wa pili kushoto) na Mwakilishi kutoka Kampuni ya Tigo pamoja na baadhi ya Walimu na Wanafunzi wakiwa katika picha ya ukumbusho.

Wanafunzi wakionyesha furaha baada ya kuboreshewa mazingira ya kusoma na Taasisi ya Hassan Maajar Trust ambayo lengo lake ni kutatua tatizo la Madawati nchini na kuhakikisha kauli mbiu yao ya “Dawati kwa kila mwanafunzi” inatimia.

MAFUTA YA PETROLI YAADIMIKA MKOANI NJOMBE

Festus Pangani, Njombe Yetu
Kwa siku ya tatu sasa mji wa Njombe umekumbwa na adha ya kukosekana kwa nishati ya mafuta ya petroli kwenye vituo vya mafuta hali inayopelekea kukwama kwa usafiri na kushuka kwa uchumi miongoni mwa jamii.
Hali hiyo imetokea kuanzia septemba 30 mwezi uliopita hadi sasa ambapo hadi hii leo ni kituo kimoja tu cha mafuta cha Ndime PetrolSstation kinauza mafuta hayo.
Wakizungumza na Njombe Yetu kwa nyakati tofauti baadhi ya madereva wa magari na pikipiki mjini Njombe wamesema kuwa adha hiyo imepelekea baadhi ya magari na pikipiki kuzima njiani yakiwa na abiria kitu ambacho kimeleta usumbufu kwa abiria.
Kwa upande wao mameneja wa baadhi ya vituo vya mafuta mjini hapa Prosper Mtewelewa wa kituo cha Ndime Petrol Station na Kaimu Meneja wa kituo cha mafuta cha Total wamesema tatizo hilo limetokea sehema ya kusambazia mafuta kutokana na siku za jumamosi na jumapili kutokuwepo kikazi.
Hata hivyo pamoja na kutokuwepo kwa mafuta mjini Njombe hakuna ongezeko lolote la bei ya mafuta mkoani hapa.
Blogzamikoa

TANESCO NA MWEKEZAJI KUTOKA MAREKANI KUZALISHA UMEME MEGAWATI 400

Na Festus Pangani, Njombe Yetu
Serikali ya Tanzania kupitia shirika la umeme tanesco kwa kushirikiana na mwekezaji kutoka nchini marekani, inajiandaa kutekeleza mradi wa umeme wa maji katika mto ruhuji.
Akizungmza wakati wa baraza la madiwani Mpimaji ardhi   mwandamizi wa Tanesco makao makuu Hamis Boby amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika hadi kufikia mwaka 2019 na kuzalisha umeme wa megawati takribani mia tatu hadi mia nne.
Boby amesema mradi huo utahusisha ujenzi wa mgodi kufua  umeme wa megawati 350 hadi 400, bwawa la kuhifadhi maji, bwawa la kuzalisha umeme, njia ya umeme, barabara, njia ya kusafirisha maji chini ya ardhi, ofisI na makazi.
Hata hivyo amesema hatua hiyo itazingatia haki za wananchi katika eneo husika kwa kulipwa fidia ya ardhi, kupata huduma za kijamii, elimu ya mahusiano, pamoja na huduma nyingine zitakazopendekezwa kwenye makubaliano yao na wadau.
Kwa upande wao madiwani wa halmashauri ya mji wa Njombe na wilaya ya Njombe wameupongeza mpango huo wa serikali na kuwataka wawekezaji hao kutoa fidia kwa wananchi watakaohamishwa ili kupisha utekelezaji wa mradi huo bila ubaguzi wala upendeleo.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa Venancy Kabelege amewataka madiwani kushirikiana na serikali katika kuwahamasisha wananchi ili kufanikisha zoezi hilo la mradi.
Blogzamikoa

KATIBU MWENEZI WA CHADEMA MAKETE HASOMEKI......


Mwenyekiti  wa Chadema Taifa Mhe. Freeman Mbowe

Katika hali ambayo haikutegemewa na wengi, katibu wa itikadi na uenezi wa CHADEMA wilayani Makete Bw. Sinene amekifagilia chama cha mapinduzi kwa kusema kuwa kimejitahidi katika mambo yake ikiwemo kuwa na wanachama wengi wilayani hapo kwa zaidi ya asilimia 90

Sinene ameyasema hayo alipokuwa akitoa nasaha zake alipoalikwa kuhudhuria mkutano wa uchaguzi wa CCM uliofanyika jana kwenye ukumbi wa shule ya sekondari Iwawa wilayani hapo

Katibu huyo alisema “nikilinganisha huko nyuma na hii leo kwa kweli chama chenu kimejitahidi kwa zaidi ya asilimia 90, mna wanachama wengi na mnaendelea kufanya mengi”

Awali wakati akianza kutoa salamu zake alisema unapokwenda sehemu inabidi utumie taratibu za eneo hilo, hivyo kulazimika kusema ‘CCM hoyeeeeeee’ hali iliyowafurahisha wajumbe wa mkutano huo wakiwemo viongozi wa CCM

Baada ya kumaliza salamu zake hizo kulipelekea utani wa hapa na pale ikiwemo kumvalisha kofia ya CCM ingawa alikataa kuivaa huku wengine wakitaka kumpa shati la kijani, na sauti za kumkaribisha CCM zikisikika

Akizungumza mara baada ya kiongozi huyo wa CHADEMA kumaliza kutoa salamu zake, katibu wa CCm wilaya ya Makete Miraji Mtaturu alisema ni kweli chama chake ni kikubwa na wapinzani watazidi kupata tabu kama alivyokiri mwenyewe

“Ndugu wajumbe kauli ya katibu mwenezi wa CHADEMA mmeisikia wenyewe, kwa kawaida katibu mwenezi ni msemaji wa chama, hivyo kauli yake ni kauli ya chama, nachopenda kumwambia hakuna haja ya kupoteza muda, njoo CCM ndugu yangu” alidai Mtaturu

Kauli hiyo ya katibu mwenezi wa CHADEMA ilizua gumzo miongoni mwa wanachama wake waliokuwa nje ya ukumbi huo huku wakisikika wakisema amejimaliza kisiasa na kuona hana haja ya kuendelea kuwepo ndani ya Chadema na badala yake ahamie CCM aliyoifagilia

Kauli hiyo pia ilitumiwa na wagombea wa CCM katika uchaguzi huo hasa wale waliokuwa wakitetea nafasi zao akiwemo Mzee Mwamwala kwa kusema kuwa “katika uongozi wangu nimefanya mengi mazuri hadi mmesikia mwenyewe CHADEMA wanaikubali CCM na wasingeikubali bila uongozi wangu mahiri, hivyo naomba kura zenu”

Pamoja na kutumia fursa hiyo Mzee Mwamwala alishindwa kutetea kiti chake na nafasi yake ilichukuliwa na Francis Chaula aliyepata kura 791 dhidi ya Mwamwala aliyepata kura 155
Francis Godwin Blog

Diwani CCM aliyejeruhiwa sasa ahamishiwa Muhimbili



  *Pia wamo Samia na Dk. Mwinyi
Diwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Kata ya Ramadhani, Wilaya ya Wanging’ombe mkoa wa Njombe, Livingstone Luvanda, ambaye alijeruhiwa vibaya kwa kupingwa na mgombea wa nafasi ya Katibu wa Siasa na Uenezi wa wilaya hiyo, amehamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Fulghence Ngonyani, akizungumza na NIPASHE jana alisema diwani huyo amehamishiwa katika hospitali hiyo kutoka Hospitali ya Mkoa ya Kibena alikokuwa amelazwa awali.

Mgombea huyo ambaye anagombea nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wilaya ya Njombe (jina tunalihifadhi), alimpiga diwani huyo kutokana na misuguano ya kiasa kwa madai kuwa  diwani huyo alikuwa kikwazo kwake ili asiweze kuchaguliwa ambapo sasa anashikiliwa na jeshi la polisi.

Awali diwani huyo akizungumza na gazeti juzi  akiwa amelazwa katika Hospitali ya Kibena,  alisema alivamiwa  majira ya saa 5:30 asubuhi wakati akitoka nyumbani kwake kuelekea katika Shule ya Kimataifa ya Mchepuo wa Kiingereza ya Livingstone kuhudhuria mahafali.

Luvanda alisema akiwa hatambui kinachoendelea, ghafla alivamiwa na mgombea huyo  na kuanza kumpiga kwa kutumia stuli hali iliyomfanya aanguke chini na kupoteza fahamu papo hapo.



Luvanda alisema kabla ya kupata mkasa huo, alidai mgombea huyo alimtumia ujumbe mfupi wa maneno (sms)  katika simu yake ya  mkononi akimweleza kuwa nilazima atamuua kutokana na kumuwekea vikwazo  ili asichaguliwe katika nafasi anayoomba.

Hata hivyo, wakati tunakwenda mitamboni, taarifa zilizopatikana zilieleza kuwa mgombea huyo alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Njombe kwa kosa la kumjeruhi diwani huyo ambapo amerudishwa mahabusu baada ya kukosa wadhamini hadi Oktoba 2, mwaka huu kesi hiyo itakaposikilizwa tena.
CHANZO: NIPASHE

Bweni la wanafunzi lawaka moto Njombe



Zaidi ya wanafunzi 93 wa kidato cha tatu na nne katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Wanike mkoani Njombe, wamenusurika kifo baada ya bweni lao kuteketea kwa moto.


Mkuu wa Wilaya ya Wang’ing’ombe, Esterina Kilasi, alisema tukio hilo lilitokea Septemba 13, mwaka huu saa 4:00 usiku.


Alisema moto huo uliteketeza vifaa mbalimbali  vya wanafunzi.

Hata hivyo, alisema moto huo hakuleta madhara kwa upande wa wanafunzi na thamani ya vifaa pamoja na chanzo cha moto huo havijafahamika.

CHANZO: NIPASHE

MWENYEKITI MPYA WA CCM LUDEWA AAHIDI MAKUBWA KWAVIJANA

Festus Pangani, Njombe Yetu.

Mwenyekiti wa vijana kupitia Chama Cha Mapinduzi wilayani Ludewa Bi.Elizabeth Augustino Haule ameahidi kufanya mambo makubwa kwa vijana baada ya kumchagua kuwa mwenyekiti kwa kipindi cha miaka mine.

 Akizungumza na waandishi wa habari jana Bi. Elizabeth alisema kutokana na yeye kuwa mjasiliamali atatumia fulsa hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine wilayani humo kutoa elimu ya kujitambua kwani vijana walio wengi bado hawajitambui.

 Alisema kijana anapaswa kijiajiri na si kusubiri kuajiriwa kwa maisha bora kwa kila mtanzania hayaji kwa kutofanya kazi na kusubiri mtu au kampuni ianzishe ndipo uajiliwe.

Elizabeth alibainisha kuwa mafanikio yake mpaka alipofikia kuwa mwenyekiti ni juhudi binafsi na si mtu alikuwa nyuma yake kwani katika mikakati yake ilikuwa kuwa diwani wa viti maalumu lakini bado lengo hilo halijafikiwa na hajakata tamaa kwa hilo.

Aidha amewataka vijana wa Chama Cha Mapinduzi kutokukubali kurubuniwa na wanasiasa kwa kuwa mgongo wao bali kuzingatia kanuni na sheria za chama hicho katika kuwapata viongozi bora na kuendeleza juhudi za kukijenga chama.

Bi.Eliza alisema vijana kwa sasa wanahitaji elimu ya ujasilia mali na mitaji na si vinginevyo hivyo kama itaanzishwa Bank ya vijana itakuwa ukombozi mkubwa kwani vijana wengi wataweza kupata mitaji na kufanya biashara zao.

Aliwaasa vijana wa wilaya ya Ludewa kutobweteka badala yake kujituma katika kazi mbalimbali kwani kupitia migodi ya Mchuchuma na Liganga vijana wa Ludewa wataweza kujikwamua kiuchumi na kuendesha maisha yao bila hofu.

Bi.Elizabeth alisema vijana wengi nchini wamekuwa ni watu wa kulalamika badala ya kufanya kazi hiyo si busala kwani maisha bora kwa kila mtanzania hayaji kwa malalamiko bali kwa kujitambua katika ufanyaji kazi za kujiongezea kipato.

Blogzamikoa

SEKTA YA UTALII NJOMBE IMETELEKEZWA?

Na Festus Pangani, Njombe Yetu
Sekta ya utalii katika mkoa wa Njombe imesahaulika licha ya kuliingizia taifa kipato kutokana na wageni mbalimbali wanaotembelea vituo vya utalii kwa ajili ya kujionea maajabu mbalimbali katika vivutio hivyo.

Mkoa wa Njombe unavivutio vingi vya utalii, ikiwamo hifadhi ya wanyama ya kitulo, shamba la maua yenye kuvutia na kustaajabisha lililopo Uwemba na mwamba wenye ramani ya afrika unaopatikana katika Kijiji cha Igodiva Tarafa ya Imalinyi wilayani Wanging’ombe.

Hata hivyo kutokuwapo kwa juhudi za kutosha katika kuhamasisha wananchi kutembelea vivutio hivyo kumechangia vivutio vingi vya utalii kutofahamika hata kwa baadhi ya wenyeji wa mkoa wa huo.
Akizungumza na Blogzamikoa Afisa Utalii, Maliasili na Mali kale wa Wilaya ya Njombe Abed Henry Chaula alikiri kuwa  wakazi wa mkoa wa Njombe kutokuwa na mwamko wa kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo mkoani hapa hali ambayo inachangia kutofahamika kwa vivutio hivyo.
“Baadhi ya wakazi wengi wa mkoa huu hawana mwamko wa kutembelea vivutio vya utalii kwa kuzani kuwa anayepaswa kutembelea vivutio hivyo ni watalii kutoka nje ya nchi pekee, lakini wengine wako hapa mkoani hawajui vivutio vya utalii vilivyopo mkoani hapa wakiamini kuwa fursa ya utalii ipo katika mikoa ya kusini pekee,” alisema Chaula.

Chaula alikiri kutofanya jitihada za makusudi katika kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo mkoani hapa pamoja na kutoa hamasa ya kutosha kwa wananchi hususani wenyeji wa mkoa wa Njombe kutembelea vivutio hivyo vya utalii.

Hata hivyo alitoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya utalii ili kuwa mabolozi wazuri wa vivutio hivyo.
“Nawaomba wakazi wa Njombe kuwa na utaratibu wa kutembelea vituo vya utalii, unajua ni aibu mgeni anakuja anakuuliza kivutio cha utalii kilichpo katika eneo lako halafu mwenyeji hukijui,’’ alisema.
Chaula alisema kukua kwa sekta ya utalii katika mkoa kutasaidia kupatikana kwa fursa nyingi za ajira na hivyo kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira nchini.
Baadhi ya vivutio vya utalii vilivyopo katika mkoa wa Njombe ni pamoja na mapango na misitu ya nyumba nitu, mwamba wenye ramani ya afrika wenye ukubwa wa hekari  saba, mpanga kipengele, hifadhi ya Kituro na Mdandu ambako kunapatikana boma la Wajerumani na mahakama ya mwanzo iliyojengwa na wajerumani pamoja na mti mkubwa wa asili wa Mlizombe.
Blogzamikoa

BWENI LATEKETEA KWA MOTO NJOMBE, WANAFUNZI 93 WANUSURIKA KIFO

Festus Pangani, Njombe Yetu
WANAFUNZI 93 wamenusurika kufa baada ya bweni lao kutekea kwa moto usiku wa kuamkia leo katika shule ya sekondari ya wasichana ya Wanike iliyopo Kata ya Mdandu wilaya ya Wanging'ombe Mkoani Njombe.

Mkuu wa wilaya hiyo Bi. Estelina Kilasi amesema, tukio hilo limetokea septemba 13 saa 4 usiku na kuteketeza vifaa mbalimbali vya wanafunzi hao ambavyo thamani yake bado haijajulikana na chanzo cha moto huo hakijafahamika.aa

Bi Kilasi amsema, bweni ambalo limeteketea ni la wasichana wanaosoma kidato cha tatu na cha nne ambao wote walifanikiwa kutoka nje na kuacha mali zao zikiteketea kwa moto.

Amevitaja vitu hivyo kuwa ni pamoja ni daftari, vitanda, magodoro na nguo za kiraia na sare zao vyote vimeteketea kwa moto huo.

Kutokana na ajali hiyo Mkuu huyo wa wilaya ameagiza wazazi wote kufika shuleni hapo septemba 16 ili kujadili kwa pamoja kuhusiana na tatizo hilo.
Blogzamikoa

NJOMBE MEDIA CLUB YAZINDULIWA





Mwandishi wetu, Njombe Yetu
Septemba 11, mwaka huu jamii ya Wananjombe ilishuhudia uzinduzi wa jumuiya ya wanahabari Njombe ambayo inajulikana kwa jina la Njombe Media Club itakayokuwa ikiwaunganisha wanahabari na wadau wa habari wa mkoani humo.
Lengo la kuanzishwa kwa club hiyo ya kutetea maslahi ya wanahabari Njombe na kuwekana sawa katika kahakikisha tasnia ya habari mkoani hapa inakua na kuchangia katika maendeleo.
Pamoja na kwamba mkoa wa Njombe umeanzishwa muda kidogo uliopita, klabu hii ya waandishi imeanzishwa sasa hasa kwa msukumo wa mauaji ya mwandishi wa kituo cha Channel Ten Iringa, Daudi Mwangosi aliyeuawa kijiji cha Nyololo wilayani mufindi katika shughuli ya kisiasa ya Chadema.
Klabu hiyo ya wanahabari mkoani Njombe imejumuisha wadau na wanahabari kutoka vituo mbalimbali vya habari kama vile gazeti la Kwanza Jamii – Njombe, Radio Uplands – Njombe, Best FM Ludewa, Kitulo FM na wawakilishi wa vituo mbalimbali vya redio na televisheni za kitaifa mkoani hapa na waandishi binafsi.
Pamoja na mambo mengine, wajumbe wa Njombe Media Club walitoa maoni yao kwa namna tofauti kuhusiana na mauaji ya Mwangosi na hatimaye klabu kutoa tamko rasmi na mtazamo kuhusiana na tukio hilo na mengine yanayofanana na hilo.
Bazil Makungu ambaye ni Mwenyekiti wa Njombe Media Club alisema “Nimesikitishwa na tukio zima, inasikitisha kuona uongo unaendelea kuenezwa wakati ukweli upo wazi na kila mtu anaona kupitia picha na video. Nina laani kitendo hicho na matumizi ya silaha zamoto si suluhu ya matatizo katika Jamii”
Naye Simon Mkina akichangia maoni yake alisema “Uandishi wa habari ni taaluma inayotakiwa kuheshimiwa, tufungue ukurasa mpya, Njombe inatakiwa kuwa na chama chenye nguvu  na umoja ambao utahakikisha usalama kwa waandishi. Kwa kuwa na umoja wenye nguvu waandishi watajiimarisha kiuchumi, tutakuza taaluma na kupata fedha kutoka kwa mashirika mengine”
Tamko la Njombe Media Club kuhusu mauaji ya mwandishi ni kuwa “Kwa suala la mwangosi, ni wazi kwamba alikuwa ni mwandishi jasiri . kifo chake kimekuwa cha kinyama sana kiasi kwamba ni ngumu kuelezeka mdomoni. Natoa pole kwa familia, waandishi wote na kwa wananchi wote kwa ujumla”
 Blogzamikoa

UJENZI WA BARABARA ZA MITAA KWA KIWANGO CHA LAMI NJOMBE WAANZA KWA KASI













Ujenzi huo unatarajiwa kukamilika miezi sita kutoka sasa kwa kiwango cha lami. Ujenzi huo unaanzia eneo la soko la wakulima karibu na ofisi za CCM wilaya na barabara ya mtaa wa Kongo
Blogzamikoa

NJOMBE KUANZA KUSAMBAZA PEMBEJEO

Festus Pangani, Njombe
Wakati msimu wa kilimo ukiwa umeanza kwa baadhi ya mikoa hapa nchini, tayari serikali imeanza kusambaza vocha za  ruzuku za pembejeo kwa wakulima ili kwenda sanjari na msimu  wa kilimo.
Mwenyekiti wa kamati ya pembejeo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Njombe Sara Dumba amesema wilaya ya Njombe ni miongoni mwa wilaya ambazo tayari zimepokea vocha hizo huku wakitarajia kuanza kuzisambaza kwa wakulima ambao shughuli za kilimo huanza mapema katika maeneo yao.
Akielezea mchakato wa kufikisha vocha za pembejeo kwa wakulima  Dumba amesema hatua za kuwafikishia wakulima hao zinafanyika huku akieleza kuwa  zoezi hilo kwa mwaka huu linafanywa na serikali kwa kuyatumia makampuni ambayo yatatafuta mawakala watakaofanya kazi ya usambazaji.
Aidha mwenyekiti huyo wa kamati ya vocha za pembejeo amesisitiza kuwa pembejeo hizo lazima ziwafikie walengwa na si vinginevyo.
blogzamikoa
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa