Home » » NJOMBE MEDIA CLUB YAZINDULIWA

NJOMBE MEDIA CLUB YAZINDULIWA





Mwandishi wetu, Njombe Yetu
Septemba 11, mwaka huu jamii ya Wananjombe ilishuhudia uzinduzi wa jumuiya ya wanahabari Njombe ambayo inajulikana kwa jina la Njombe Media Club itakayokuwa ikiwaunganisha wanahabari na wadau wa habari wa mkoani humo.
Lengo la kuanzishwa kwa club hiyo ya kutetea maslahi ya wanahabari Njombe na kuwekana sawa katika kahakikisha tasnia ya habari mkoani hapa inakua na kuchangia katika maendeleo.
Pamoja na kwamba mkoa wa Njombe umeanzishwa muda kidogo uliopita, klabu hii ya waandishi imeanzishwa sasa hasa kwa msukumo wa mauaji ya mwandishi wa kituo cha Channel Ten Iringa, Daudi Mwangosi aliyeuawa kijiji cha Nyololo wilayani mufindi katika shughuli ya kisiasa ya Chadema.
Klabu hiyo ya wanahabari mkoani Njombe imejumuisha wadau na wanahabari kutoka vituo mbalimbali vya habari kama vile gazeti la Kwanza Jamii – Njombe, Radio Uplands – Njombe, Best FM Ludewa, Kitulo FM na wawakilishi wa vituo mbalimbali vya redio na televisheni za kitaifa mkoani hapa na waandishi binafsi.
Pamoja na mambo mengine, wajumbe wa Njombe Media Club walitoa maoni yao kwa namna tofauti kuhusiana na mauaji ya Mwangosi na hatimaye klabu kutoa tamko rasmi na mtazamo kuhusiana na tukio hilo na mengine yanayofanana na hilo.
Bazil Makungu ambaye ni Mwenyekiti wa Njombe Media Club alisema “Nimesikitishwa na tukio zima, inasikitisha kuona uongo unaendelea kuenezwa wakati ukweli upo wazi na kila mtu anaona kupitia picha na video. Nina laani kitendo hicho na matumizi ya silaha zamoto si suluhu ya matatizo katika Jamii”
Naye Simon Mkina akichangia maoni yake alisema “Uandishi wa habari ni taaluma inayotakiwa kuheshimiwa, tufungue ukurasa mpya, Njombe inatakiwa kuwa na chama chenye nguvu  na umoja ambao utahakikisha usalama kwa waandishi. Kwa kuwa na umoja wenye nguvu waandishi watajiimarisha kiuchumi, tutakuza taaluma na kupata fedha kutoka kwa mashirika mengine”
Tamko la Njombe Media Club kuhusu mauaji ya mwandishi ni kuwa “Kwa suala la mwangosi, ni wazi kwamba alikuwa ni mwandishi jasiri . kifo chake kimekuwa cha kinyama sana kiasi kwamba ni ngumu kuelezeka mdomoni. Natoa pole kwa familia, waandishi wote na kwa wananchi wote kwa ujumla”
 Blogzamikoa

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa