Home » » SEKTA YA UTALII NJOMBE IMETELEKEZWA?

SEKTA YA UTALII NJOMBE IMETELEKEZWA?

Na Festus Pangani, Njombe Yetu
Sekta ya utalii katika mkoa wa Njombe imesahaulika licha ya kuliingizia taifa kipato kutokana na wageni mbalimbali wanaotembelea vituo vya utalii kwa ajili ya kujionea maajabu mbalimbali katika vivutio hivyo.

Mkoa wa Njombe unavivutio vingi vya utalii, ikiwamo hifadhi ya wanyama ya kitulo, shamba la maua yenye kuvutia na kustaajabisha lililopo Uwemba na mwamba wenye ramani ya afrika unaopatikana katika Kijiji cha Igodiva Tarafa ya Imalinyi wilayani Wanging’ombe.

Hata hivyo kutokuwapo kwa juhudi za kutosha katika kuhamasisha wananchi kutembelea vivutio hivyo kumechangia vivutio vingi vya utalii kutofahamika hata kwa baadhi ya wenyeji wa mkoa wa huo.
Akizungumza na Blogzamikoa Afisa Utalii, Maliasili na Mali kale wa Wilaya ya Njombe Abed Henry Chaula alikiri kuwa  wakazi wa mkoa wa Njombe kutokuwa na mwamko wa kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo mkoani hapa hali ambayo inachangia kutofahamika kwa vivutio hivyo.
“Baadhi ya wakazi wengi wa mkoa huu hawana mwamko wa kutembelea vivutio vya utalii kwa kuzani kuwa anayepaswa kutembelea vivutio hivyo ni watalii kutoka nje ya nchi pekee, lakini wengine wako hapa mkoani hawajui vivutio vya utalii vilivyopo mkoani hapa wakiamini kuwa fursa ya utalii ipo katika mikoa ya kusini pekee,” alisema Chaula.

Chaula alikiri kutofanya jitihada za makusudi katika kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo mkoani hapa pamoja na kutoa hamasa ya kutosha kwa wananchi hususani wenyeji wa mkoa wa Njombe kutembelea vivutio hivyo vya utalii.

Hata hivyo alitoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya utalii ili kuwa mabolozi wazuri wa vivutio hivyo.
“Nawaomba wakazi wa Njombe kuwa na utaratibu wa kutembelea vituo vya utalii, unajua ni aibu mgeni anakuja anakuuliza kivutio cha utalii kilichpo katika eneo lako halafu mwenyeji hukijui,’’ alisema.
Chaula alisema kukua kwa sekta ya utalii katika mkoa kutasaidia kupatikana kwa fursa nyingi za ajira na hivyo kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira nchini.
Baadhi ya vivutio vya utalii vilivyopo katika mkoa wa Njombe ni pamoja na mapango na misitu ya nyumba nitu, mwamba wenye ramani ya afrika wenye ukubwa wa hekari  saba, mpanga kipengele, hifadhi ya Kituro na Mdandu ambako kunapatikana boma la Wajerumani na mahakama ya mwanzo iliyojengwa na wajerumani pamoja na mti mkubwa wa asili wa Mlizombe.
Blogzamikoa

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa