Home » » Diwani CCM aliyejeruhiwa sasa ahamishiwa Muhimbili

Diwani CCM aliyejeruhiwa sasa ahamishiwa Muhimbili



  *Pia wamo Samia na Dk. Mwinyi
Diwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Kata ya Ramadhani, Wilaya ya Wanging’ombe mkoa wa Njombe, Livingstone Luvanda, ambaye alijeruhiwa vibaya kwa kupingwa na mgombea wa nafasi ya Katibu wa Siasa na Uenezi wa wilaya hiyo, amehamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Fulghence Ngonyani, akizungumza na NIPASHE jana alisema diwani huyo amehamishiwa katika hospitali hiyo kutoka Hospitali ya Mkoa ya Kibena alikokuwa amelazwa awali.

Mgombea huyo ambaye anagombea nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wilaya ya Njombe (jina tunalihifadhi), alimpiga diwani huyo kutokana na misuguano ya kiasa kwa madai kuwa  diwani huyo alikuwa kikwazo kwake ili asiweze kuchaguliwa ambapo sasa anashikiliwa na jeshi la polisi.

Awali diwani huyo akizungumza na gazeti juzi  akiwa amelazwa katika Hospitali ya Kibena,  alisema alivamiwa  majira ya saa 5:30 asubuhi wakati akitoka nyumbani kwake kuelekea katika Shule ya Kimataifa ya Mchepuo wa Kiingereza ya Livingstone kuhudhuria mahafali.

Luvanda alisema akiwa hatambui kinachoendelea, ghafla alivamiwa na mgombea huyo  na kuanza kumpiga kwa kutumia stuli hali iliyomfanya aanguke chini na kupoteza fahamu papo hapo.



Luvanda alisema kabla ya kupata mkasa huo, alidai mgombea huyo alimtumia ujumbe mfupi wa maneno (sms)  katika simu yake ya  mkononi akimweleza kuwa nilazima atamuua kutokana na kumuwekea vikwazo  ili asichaguliwe katika nafasi anayoomba.

Hata hivyo, wakati tunakwenda mitamboni, taarifa zilizopatikana zilieleza kuwa mgombea huyo alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Njombe kwa kosa la kumjeruhi diwani huyo ambapo amerudishwa mahabusu baada ya kukosa wadhamini hadi Oktoba 2, mwaka huu kesi hiyo itakaposikilizwa tena.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa