Home » » SHULE YA SEKONDARI IWAWA WILAYANI MAKETE YATOA SIRI YA KUFANYA VIZURI MATOKEO YA KIDATO CHA SITA 2014‏

SHULE YA SEKONDARI IWAWA WILAYANI MAKETE YATOA SIRI YA KUFANYA VIZURI MATOKEO YA KIDATO CHA SITA 2014‏


Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 



Makamu mkuu wa shule ya sekondari Iwawa Fadhili Dononda akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake hii leo.Ikiwa zimepita siku chache tangu kutangazwa matokeo ya kidato cha sita mwaka huu, shule ya sekondari Iwawa iliyoko wilayani Makete mkoani Njombe imetoa siri ya mafanikio ya wanafunzi wake kufaulu na kushika nafasi ya nne kitaifa. 
 
Akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake Makamu mkuu wa shule hiyo Mwl. Fadhili Dononda amesema miongoni mwa sababu hizo ni pamoja na wanafunzi hao kuwa na utayari wa kusoma hivyo wanafunzi hao hawakuwa walevi wala watoro bali walikuwa wakizingatia masomo. 
 
Amesema kutokana na wanafunzi hao kutopenda utoro wala ulevi na kuwasikiliza walimu wao na kufuata taratibu za shule kumepelekea wao kutumia muda mwingi katika masomo. 
 
Mwalimu Dononda amesema pia nidhamu baina ya wanafunzi wenyewe kwa wenyewe pamoja na kwa walimu wao kumesababisha walimu kuwa na ari ya kuwafundisha na kutumia jitihada za hali ya juu kwa wanafunzi hao ili waweze kufaulu vizuri jambo ambalo limefanikiwa. 
 
"Unajua kila mzazi anamleta mtoto wake shule ili afaulu, sasa ukiwakuta wanafunzi wana ari kwa kweli hata mwalimu unapata moyo wa kufundisha kwa bidii, wanafunzi hawa waliofaulu walikuwa wamechujwa ipasavyo toka wakiwa o'level (kidato cha i-iv) kutoka kwenye shule walizosoma, hivyo kila mmoja alikuwa na moyo wa kuhakikisha anafaulu, na pia wenyewe walikuwa na mshikamano pia" amesema mwalimu huyo. 
 
Ameongeza kuwa katika mtihani wa utamirifu (mock) ambao ulifanywa na wanafunzi 39 pia ulionesha dalili njema za matokeo ya mwisho kuwa mazuri kwa sababu wanafunzi 29 walipata daraja la I, 9 wakapata daraja la II, na mmoja alipata daraja la III.
 
Kwa upande wake mwalimu Jitahidi Sanga ambaye alikuwa akifundisha masomo ya Jiografia na General Studies kwa wanafunzi hao na pia mwalimu wa darasa, amesema siri ya wanafunzi hao kufaulu vizuri ni pamoja na walimu kufundisha kwa muda wa ziada na wikiendi bila malipo yeyote. 
 
Amesema utayari waliokuwa nao wanafunzi hao ulipelekea kufundishwa muda wa ziada bila kusukumwa. 
 
"Kwa mfano likizo ya mwezi Juni mwaka jana wanafunzi hao wengi wao hawakwenda likizo, na mimi mwenyewe nilikuwa nikiwafundisha kwa muda wa ziada bila kudai malipo yeyote, na pia kwa kuwa nilikuwa mwalimu wa darasa nilikuwa nikiwasihi wazingatie masomo pamoja na yale waliyoaswa na wazazi wao" amesema mwalimu Sanga.
 
Bi Anita Sanga ni mzazi ambaye amezungumza na mwandishi wetu na kusema kuwa matokeo hayo wameyapokea kwa furaha na hawakutegemea kama shule hiyo ingefanya vizuri kwa kiasi hicho. 
 
Amesema wanafunzi wote wazingatie masomo kama walivyofanya hao waliomaliza kidato cha sita ili shule hiyo iendelee kufanya vizuri na hatimaye iwe ya kwanza kitaifa kwa kidato cha nne na cha sita. 
 
Shule ya sekondari Iwawa ni miongoni mwa shule tatu za serikali zenye kidato cha tano na sita wilayani hapo.

Na Edwin Moshi

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa