Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu
Tukio hilo lilitokea Jumatatu wiki hii wakati Waziri Nyalandu alipokuwa ofisi za makao makuu ya NCAA kwa ajili ya kuzindua bodi aliyoiteua, lakini kabla ya kufanya hivyo, alizuiwa na kundi la wafugaji wanaoishi eneo hilo huku wakiwa wameshika mabango yenye ujumbe wa maneno tofauti tofauti.
Hali hiyo ilimfanya Waziri Nyalandu kusimama na kuwasikiliza kilio chao.Baadhi ya mabango yalisomeka: “Tunataka uwakilishi wa asilimia tano katika bodi, tunataka maeneo ya ufugaji, haki zangu kama mwenyeji wa hapa haijaheshimika. Wenyeji wa hapa hawajahusishwa katika kusimamia na kuhifadhi Ngorongoro, ahadi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, haijatekelezwa. Hatuhitaji zaidi uwekezaji hoteli katika kingo za creta ya Ngorongoro.”
Ujumbe mwingine ulisomeka: “Tunahitaji kuhusishwa katika ajira, chakula cha lishe bora na sio tu mahindi. Njaa: haki ya kuishi ipo hatarini kwa Wamasai wanaoishi Ngorongoro.”
Akijibu malalamiko ya Wamasai hao, Waziri Nyalandu aliahidi baada ya majuma mawili atateua mtu mmoja maarufu katika jamii ya Wamasai kuwa mjumbe wa bodi hiyo.
“Hii ni sehemu ya kutekeleza matakwa yenu kwa kuzingatia tunataka Wamasai kuwa sehemu muhimu ya kulinda raslimali hii,” alisema.
Hata hivyo alisema bodi ya sasa ina mjumbe mmoja kutoka Baraza la Wafugaji, taasisi ambayo inawakilisha wafugaji wenyeji wa eneo hilo.
Waziri Nyalandu alikiri kuwapo kwa changamoto nyingi zinazoikabili mamlaka hiyo ikiwemo kuongezeka kwa idadi kubwa ya shughuli za kibinadamu, huku akieleza wakati Mamlaka hiyo ilipoanzishwa mwaka 1959, ilikuwa na idadi ya watu 8,000 lakini miaka 50 baadaye yaani 2009 idadi hiyo iliongezeka hadi kufikia zaidi ya 66,000 na katika sense maalum iliyofanyika hivi karibuni, imeonyesha kuwa hifadhi hiyo ina jumla ya watu 87,000.
Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA ni Balozi Mwanaidi Maajar, ambaye aliahidi kufanya kazi kwa karibu katika kutekeleza maagizo yanayotolewa na wizara ili kuhakikisha mamlaka hiyo inaendeshwa pasipo vikwazo vyo vyote.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment