Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MKUU wa Mkoa (RC) wa Njombe, Kapteni Mstaafu, Assery Msangi,
amekaribisha watu binafsi, mashirika na taasisi yoyote kujitokeza
kusaidia ujenzi wa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Mkoa
ya Kibena kutokana na kilichopo kuwa katika hali mbaya hivi sasa.
Kapteni Msangi, aliyasema hayo wakati akikabidhiwa msaada wa taa
maalumu mbili za kufanyia upasuaji kwenye chumba cha upasuaji cha
hospitali hiyo iliyopo mjini hapa, uliotolewa na Shirika la Hifadhi ya
Jamii (NSSF), wenye thamani sh milioni 9.
Msangi, alitoa rai kwa yeyote ambaye atakuwa tayari kufanya kazi ya
kuwekeza kwenye chumba cha maiti, hatakuwa na kipangamizi.
Aliipongeza NSSF kwa msaada huo, lakini akatoa rai kwa shirika hilo,
taasisi na watu binafsi, kufikiria namna ya kuweza kusaidia kujenga
chumba cha maiti kwenye hospitali hiyo ya Kibena.
“Kwa niaba ya wananchi wangu na viongozi wa Mkoa wa Njombe, napenda
kuwashukuru NSSF kwa msaada huo, lakini tunalo tatizo kubwa hivi sasa
la mochwari, na mochwari hivi sasa hazijengwi na serikali, bali
zinajengwa na mtu binafsi, taasisi na shirika lolote,” alisema Msangi.
Alisema endapo watajitokeza kuwekeza kwa kujenga chumba cha
kuhifadhia maiti, kutasaidia kupata faida ya haraka na yenye manufaa.
“Mochwari na mila zetu ni mahali nyeti sana, lakini nataka niseme
kwamba hili Katibu Tawala mliangalie, kwani zinajengwa na watu binafsi
au taasisi, kwa sababu ukiweka maiti nane au kumi, maana yake utakuwa
unamdai maiti hela kwa kila siku, ni biashara nzuri tu,” alisema
Msangi.
Alitoa mfano kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuph
Makamba, aliporuhusu biashara ya majeneza wengi waliona kama ni
biashara ya ajabu, lakini hivi sasa imekuwa ni muhimu na isiyokuwa na
shaka kwa jamii.
“Wapo walimfuata Makamba na kumwambia sasa mkuu hii si balaa,
majeneza yanauzwa barabarani kama mashati, akawaambia muda wake ukifika
mtaona umuhimu wake, ukienda hospitali ya KCMC pale, ile wamejenga
wenyewe, lakini ile wameibinafsisha, kuna mtu anafanya shughuli pale,
ukilaza maiti unalipia sh 5,000 au 10,000 kwa ‘night’, hivyo nataka
nitoe wito kwa mashirika na watu binafsi wajitokeze kujenga.
“Ni biashara ambayo haina ubishi wala mapatano, kwa kawaida mfiwa
hana mapatano au nipunguzie, huwa hamna mapatano ya kupunguziana bei,
ni eneo ambalo ni zuri la biashara, hivyo watu wajitokeze kujenga,
Watanzania wenye moyo na kuguswa na tatizo hili, wajitokeze kujenga
hospitali yetu.”
Meneja wa NSSF Mkoa wa Njombe, Godwin Mwakalukwa, alisema shirika lao
limetoa msaada huo, baada ya kuguswa na tatizo la ukosefu wa taa
maalumu ya kufanyia upasuaji kwenye chumba hicho
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment