Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Makamu mkuu wa shule ya sekondari Iwawa Fadhili Dononda akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake hii leo.Ikiwa
zimepita siku chache tangu kutangazwa matokeo ya kidato cha sita mwaka
huu, shule ya sekondari Iwawa iliyoko wilayani Makete mkoani Njombe
imetoa siri ya mafanikio ya wanafunzi wake kufaulu na kushika nafasi ya
nne kitaifa.
Akizungumza
na mwandishi wetu ofisini kwake Makamu mkuu wa shule hiyo Mwl. Fadhili
Dononda amesema miongoni mwa sababu hizo ni pamoja na wanafunzi hao kuwa
na utayari wa kusoma hivyo wanafunzi hao hawakuwa walevi wala watoro
bali walikuwa wakizingatia masomo.
Amesema
kutokana na wanafunzi hao kutopenda utoro wala ulevi na kuwasikiliza
walimu wao na kufuata taratibu za shule kumepelekea wao kutumia muda
mwingi katika masomo.
Mwalimu
Dononda amesema pia nidhamu baina ya wanafunzi wenyewe kwa wenyewe
pamoja na kwa walimu wao kumesababisha walimu kuwa na ari ya
kuwafundisha na kutumia jitihada za hali ya juu kwa wanafunzi hao ili
waweze kufaulu vizuri jambo ambalo limefanikiwa.
"Unajua
kila mzazi anamleta mtoto wake shule ili afaulu, sasa ukiwakuta
wanafunzi wana ari kwa kweli hata mwalimu unapata moyo wa kufundisha kwa
bidii, wanafunzi hawa waliofaulu walikuwa wamechujwa ipasavyo toka
wakiwa o'level (kidato cha i-iv) kutoka kwenye shule walizosoma, hivyo
kila mmoja alikuwa na moyo wa kuhakikisha anafaulu, na pia wenyewe
walikuwa na mshikamano pia" amesema mwalimu huyo.
Ameongeza
kuwa katika mtihani wa utamirifu (mock) ambao ulifanywa na wanafunzi 39
pia ulionesha dalili njema za matokeo ya mwisho kuwa mazuri kwa sababu
wanafunzi 29 walipata daraja la I, 9 wakapata daraja la II, na mmoja
alipata daraja la III.
Kwa
upande wake mwalimu Jitahidi Sanga ambaye alikuwa akifundisha masomo ya
Jiografia na General Studies kwa wanafunzi hao na pia mwalimu wa
darasa, amesema siri ya wanafunzi hao kufaulu vizuri ni pamoja na walimu
kufundisha kwa muda wa ziada na wikiendi bila malipo yeyote.
Amesema utayari waliokuwa nao wanafunzi hao ulipelekea kufundishwa muda wa ziada bila kusukumwa.
"Kwa
mfano likizo ya mwezi Juni mwaka jana wanafunzi hao wengi wao
hawakwenda likizo, na mimi mwenyewe nilikuwa nikiwafundisha kwa muda wa
ziada bila kudai malipo yeyote, na pia kwa kuwa nilikuwa mwalimu wa
darasa nilikuwa nikiwasihi wazingatie masomo pamoja na yale waliyoaswa
na wazazi wao" amesema mwalimu Sanga.
Bi
Anita Sanga ni mzazi ambaye amezungumza na mwandishi wetu na kusema
kuwa matokeo hayo wameyapokea kwa furaha na hawakutegemea kama shule
hiyo ingefanya vizuri kwa kiasi hicho.
Amesema
wanafunzi wote wazingatie masomo kama walivyofanya hao waliomaliza
kidato cha sita ili shule hiyo iendelee kufanya vizuri na hatimaye iwe
ya kwanza kitaifa kwa kidato cha nne na cha sita.
Shule ya sekondari Iwawa ni miongoni mwa shule tatu za serikali zenye kidato cha tano na sita wilayani hapo.
Na Edwin Moshi
Na Edwin Moshi
0 comments:
Post a Comment