Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Wako waandishi na watafiti ambao ni wageni na hupenda zaidi
kujifunza Kiswahili. Ukiwauliza kwa nini wanapenda Kiswahili, wanajibu
kuwa ni lugha ya pekee isiyobanwa na dhana za kikabila na kieneo,
inavuka mipaka ya nchi na kuwa ni ya kimataifa.
Mgeni mmojawapo ni Pete Muhunzi (jina la kupanga)
ambaye ni Mmarekani mwenye asili ya Afrika. Ni Profesa mstaafu wa
historia na anafanya utafiti wa masuala ya lugha katika jamii na hasa
Kiswahili.
Alifafanua kuwa sababu ya kutambuliwa kwa
Kiswahili kuwa ni lugha ya kazi katika vikao vya Umoja wa Nchi za Afrika
(AU) ni hatua muhimu katika historia ya lugha hiyo. Uamuzi uliotolewa
wa kukifanya Kiswahili kuwa ni lugha ya kazi, uliotokana na kukosekana
kwa lugha nyingine za Kiafrika zinazokidhi viwango vya kimataifa.
Kwa mfano, lugha kama Kiigbo, Kiyoruba na Kihausa
zote zikiwa ni za Afrika Magharibi na zinavuka mipaka ya nchi. Umoja wa
Nchi huru za Afrika (OAU) uliamua kuteua moja ya lugha za Kiafrika na
kupendelea kukiteua Kiswahili.
Hatua ya kukiteua Kiswahili ilitokana na uamuzi
uliofanyika katika kikao cha Mawaziri wa Utamaduni wa Umoja wa Nchi Huru
za Afrka nchini Mauritius mwaka 1988. Mawaziri wa Utamaduni waliibua
wazo la kupata lugha moja ya Kiafrika itakayotumika pamoja na lugha za
kazi, ambazo ni za kikoloni yaani Kiingereza, Kifaransa, Kireno na
Kiarabu. Pendekezo la mawaziri wa utamaduni la kutumia Kiswahili kuwa ni
lugha ya Kiafrika na ya tano katika vikao vya OAU ni uamuzi wa kipekee.
Pendekezo hilo liliwasilishwa katika kikao cha Wakuu wa Nchi na Serikali za Afrika huko Addis Ababa na lilikubaliwa.
Kwa kuwa Tanzania ni kitovu cha lugha ya Kiswahili
na kina vyombo kadhaa vya kukikuza na kukiendeleza katika ngazi
mbalimbali za jamii ikiwamo katika shughuli za Serikali, shuleni na
vyuoni, iliteuliwa kusimamia na kutekeleza suala hili.
Hatua ya kwanza ni kuwatambua wafanyakazi waliohitimu chuo kikuu wenye digrii ya kwanza na waliosomea lugha ya Kifaransa.
Kwa maana hiyo, waliochaguliwa walikuwa wakifahamu
Kifaransa, Kiingereza na Kiswahili, lugha zilizokuwa zikitumika katika
vikao vya OAU. Ilibidi kuwaandaa wataalamu katika fani za wakalimali na
wafasiri ili waende kupata taaluma ya juu ya ukalimani na tafsri, ili
watakaporejea kutoka masomoni wapelekwe Addis Ababa kutekeleza majukumu
yao kwenye shughuli za kazi.
Je, hali ilikuwaje baadaye. Hapo awali ilibidi
waandaliwe vijana waliosomea lugha katika ngazi ya shahada ya kwanza ili
kupelekwa kujiendeleza katika taaluma hizi. Serikali ya Ufaransa
ilikubali kugharimia mafunzo ya vijana hawa kwa safari na mafunzo. Kwa
bahati nzuri waliteuliwa vijana wanne kwenda kusoma Ufaransa kwa mwaka
mmoja. Baada ya kurejea nchini waliripoti Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa.
Jambo la kushangaza ni kuwa wizara husika
haikuwajali, hivyo wakaanza kujitafutia kazi wao wenyewe katika nchi za
nje. Mmoja alikwenda Burundi katika Umoja wa Nchi za Maziwa Makuu,
mwingine alikwenda Ivory Coast katika Shirika la Uchumi la ECOWAS,
Afrika Magharibi.
Tanzania imekosa nafasi ya kuwapatia vijana wake
ajira ya uhakika. Hivi sasa huduma za ukalimani na tafsiri zinafanyika
kwa mtindo wa kazi za muda (part time), badala ya kuwapo kwa wafanyakazi
wa kudumu
Sasa, ipo haja kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa pamoja na Wizara ya Utamaduni, Vijana na Michezo kuwa na
makubaliano ya kulikabili suala hili kwa pamoja na kurejesha nchi katika
hadhi iliyopewa huko awali.
Kutokana na Tanzania kushindwa kutekeleza
mapendekezo ya OAU, tutajilaumu wenyewe. Hii siyo mara ya kwanza kwa
Tanzania kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kimataifa kuhusu lugha ya
Kiswahili. Soma makala yajayo..
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment