Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.
Mjumbe huyo kutoka kundi la 201, Isaack Cheyo, amesema kwamba kinachotakiwa kufanyika ni pande zote zinazovutana kukaa chini na kutafuta maridhiano.
Jumatano jioni wiki hii, wajumbe kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) pamoja na wajumbe wengine 25 wa kuteuliwa kutoka kundi la 201 walitoka nje wakilalamikia pamoja na mambo mengine, kauli za vitisho na ubaguzi zilizotolewa katika Kanisa la Medhodist Jumamosi iliyopita mjini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuteka mapendekezo ya rasimu ya Tume ya Warioba kuhusu Muungano.
Cheyo alisema kwamba kutoka nje ni suala la kawaida katika mabunge yote duniani kwa upande husika kuonyesha hisia zake kuwa suala fulani hawakubaliani nalo.
Cheyo ambaye anatoka katika Chama cha United Democratic (UDP), aliliambia NIPASHE kuwa: “Pale msipokubaliana nkatafute maridhiano kwamba sisi tunataka haya, na hawa haya.”
Alisema kwamba katika hali ya sasa ya bunge hilo kwa sheria na kanuni, hakuna mshindi kwa sababu zinasema kuwa thelithi mbili ya wajumbe wa pande zote wanatakiwa kukubaliana.
“Kwa hali ya ndani Bara inawezekana theluthi mbili ikapatikana, lakini kwa upande wa Zanzibar haitapatikana, hivyo katiba hakuna,” alisema Cheyo, abaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu wa UDP.
Aliongeza: “Hata ikipelekwa kwenye referendum (kura ya maoni) Bara inaweza kupata theluthi mbili, lakini kwa Zanzibar haiwezi kupatikana.”
Alisema kuwa ili kuondoa hali hiyo, yatafutwe maridhiano kwa viongozi wa vyama kukutana na kuwashirikisha viongozi wa dini pamoja na makundi mengine ya wananchi, vinginevyo katiba haitapatikana na matokeo yake itarudi katiba ya zamani.
“Kwa CCM kubadili sura zilizomo katika rasimu na kuleta ya zamani, kwa nini wasilipeleke katika Bunge la Muungano na hili lingeepusha lawana kwa tume,” alisema.
“Kama ni hivyo basi, Bunge la Katiba lisingeitishwa na kusababisha gharama kubwa kuanzia za kugharamia tume,” alisema.
“Baadhi yetu tunachojiuliza ni kwamba kama kutashindawa kutondoka bila katiba, wananchi huko nje watatuonaje,” alisema.
Alisema kuwa muda wa mapumziko kwa ajili ya kupisha Bunge la Bajeti unaweza kutumika kukutana na kutafuta maridhiano.
“Kama wengi wanakataa rasimu, kwa nini tusiandae kura ya maoni kuuliza wananchi muundo wa Muungano wanaoutaka kisha turejee na kupendekeza muundo walioutaka na hilo litapunguza gharama,” alisema Cheyo na kuongeza kwamba: “Tumeanza vibaya, tungeanza na wananchi.”
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment