Home » » Serikali yaanza kusaka masoko ya mazao

Serikali yaanza kusaka masoko ya mazao

SERIKALI mkoani Njombe kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara imeanza kutafuta ufumbuzi tatizo la ukosefu wa masoko ya uhakika kwa mazao ya kilimo ikiwemo viazi mviringo ambapo, ujenzi wa soko la kimataifa mjini Makambako utasaidia kumaliza tatizo hilo.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010-2015 kwa kipindi cha miezi nane iliyopita, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Assery Msangi, alisema katika kipindi hicho pamoja na mafanikio yaliyopatikana mkoani hapa, bado kumekuwa na changamoto mbalimbali.
Alitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na baadhi ya wakulima kukataa kutumia mbolea ya minjingu kwa madai ya kuwa haina ubora katika kilimo. Aliongeza kuwa, serikali inaendelea kuwahamasisha wakulima kuimarisha vyama vya ushirika wa mazao ili kuwa na nguvu ya pamoja wakati wa kupanga ili kuuza mazao kwa bei nzuri.
Alisema, kwa sasa mkoa unaendelea kuiomba wizara ya kilimo kutoa nafasi kwa mkulima kuchagua ni aina gani ya mbolea anayotaka kutumia badala ya kuendelea kuwalazimisha kutumia minjingu ambayo wakulima wengi wameonesha kutokuwa na imani nayo.
"Tunaendelea kuhamasisha wananchi na tunaiomba wizara kama inawezeka na msimu ujao watoe uhuru mtu achague aina ya mbolea ambayo anataka kutumia," alisema Msangi.
Aliongeza kuwa, mwaka ujao wa fedha serikali imekusudia kupunguza changamoto za miundombinu ikiwemo kuboresha barabara zitakazoweza kuunganisha kati ya wilaya moja hadi nyingine bila matatizo ikiwemo wilaya za Ludewa na Makete.

Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa