- Mbunge CCM aongoza mashambulizi
KIKOSI cha ulinzi cha Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilayani Njombe,
mkoani Iringa kimewashushia kipigo wanachama wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) na kumvunja taya mwanachama, Ally Kalonga.
Licha ya kushusha kipigo hicho, Mkuu wa Polisi wilayani Njombe, Lucy
Mwakafirwa, amelaumiwa kuwakumbatia watuhumiwa makada wa CCM, huku
akiwasweka ndani wanachama wa CHADEMA.
Akizungumza na Tanzania Daima jana kwa njia ya simu kutoka eneo la
tukio, mwananchi ambaye hakupenda jina lake litajwe, alisema kikosi cha
CCM cha ‘Green Guards’ kilitoa kipigo kwa wafuasi wa CHADEMA baada ya
kubaini mpango wao wa kutaka kugawa fedha kwa wapiga kura utabainika.
CCM na CHADEMA wako katika kampeni za udiwani wa Kata ya Njombe Mjini
unaotarajiwa kufanyika Februari 9, sambamba na kata nyingine 27 nchini
kote.
“Siku ya leo (jana) tulikuwa na mikutano ya kampeni za udiwani wa
Kata ya Njombe Mjini, mikutano ilifanyika salama huku vyama vyote
vikimaliza salama,” alisema.
Kwa mujibu wa shuhuda huyo, baada ya kukamilika kwa kampeni hizo
viongozi wa CCM wilayani hapo wakiongozwa na mbunge wa chama hicho (jina
linahifadhiwa), walielekea katika Kijiji cha Matalawe.
Mwananchi huyo alisema baada ya kufika Matalawe, walikusanya baadhi
ya wananchi na kuwaweka katika chumba kimoja na kuanza kugawa fedha.
“Baadhi ya Wana CHADEMA waliokuwepo pale, hawakupendezwa na jambo
hilo, hivyo waliamua kupiga simu kwa viongozi wao kuwajulisha mchezo huo
mchafu na viongozi hao walichukua gari kuja eneo hilo,” alisema.
Alisema kabla ya kufika walikutana na kundi la vijana wa CCM waliokuwa wametanda barabarani.
Alisema vijana hao wa CCM waliwaamuru Wana CHADEMA hao wasimame,
kisha walichomoa funguo za gari lao lililokuwa likiendeshwa na Ally
Muhagama.
“Green Guards walisimamisha gari la vijana wa CHADEMA,
wakamnyang’anya funguo dereva, wakamshusha chini na kuanza kumpiga.
Wakati wakiendelea kumpiga, ghafla alitokea mtu mmoja aliyevaa kiraia na
kujitambulisha kuwa askari na kuomba wamuachie mtu huyo.
“Kutokana na kauli hiyo mbunge aliyekuwa na vijana wa CCM alimuomba
raia huyo atoe kitambulisho lakini hakuwa nacho, ndipo naye
alipogeuziwa kibao na kuanza kupigwa na baadaye walifungiwa kwenye ofisi
ya CCM ya eneo hilo,” alisema mtoa habari wetu.
Alisema vijana wa CHADEMA waliojificha baada ya kuona wenzao wakipata
kipigo hicho walijaribu kukimbia lakini Green Guards waliwakamata na
kuwapa kipigo huku mmoja wao akivunjwa taya na hali yake si nzuri.
“Hata hivyo wananchi walilazimika kupiga simu polisi ambapo walifika
na kuwaamuru Wana CCM hao na mbunge wao wawatoe na kuelekea kituo cha
polisi,” alisema.
Kwa mujibu wa mtoa habari wetu, wakiwa polisi, mbunge huyo na
viongozi wa wilaya walifika kituoni na kwenda moja kwa moja katika ofisi
ya OCD Mwakafirwa.
Mwananchi huyo alisema baada ya dakika chache ilitolewa amri ya
kuwasweka ndani wanachama hao wa CHADEMA walioumizwa, huku baadhi yao
wakiendelea kuvuja damu.
Gazeti hili lililazimika kumtafuta Mwakafirwa ambaye hakukubali wala
kukataa kuwepo kwa vurugu hizo huku akimtaka mwandishi wa habari hizi
kuwasiliana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi
(ACP) Ramadhan Mungi, kwa taarifa zaidi.
Kwa upande wake Kamanda Mungi alisema hajapata taarifa kamili na kwamba anafuatilia kujua ukweli na undani wa tukio hilo
Chamzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment