Tangu gazeti dada la The Citizen
lichapishe mwishoni mwa wiki habari za upotevu wa Sh480 bilioni katika
Wizara ya Fedha, Serikali imekaa kimya kama vile wizi huo ni tukio la
kawaida, hivyo halihitaji maelezo ya kina wala ya haraka. Wananchi
walitegemea kwamba Serikali ingetoa kauli haraka iwezekanavyo kuhusu
mazingira ya upotevu huo na hatua inazochukua kuwawajibisha wahusika.
Tunasema kiasi hicho cha fedha zilizoibwa ni
kikubwa kwa sababu ni zaidi ya bajeti ya mwaka kwa baadhi ya wizara,
zikiwamo wizara kubwa kama ya Uchukuzi ambayo katika mwaka wa fedha wa
2013/14, kwa mfano ilitengewa Sh491 bilioni.
Tunaambiwa Sh480 bilioni zilizopotea katika Wizara
ya Fedha zinaweza kujenga kilomita 375 za barabara kwa kiwango cha lami
ikiwa ni urefu wa kutoka Dar es Salaam hadi Gairo, kilomita chache
kutoka Dodoma. Tujiulize kiasi hicho cha fedha kingeweza kugharamia
madawati, zahanati na madarasa mangapi kwa ajili ya wagonjwa na
wanafunzi wetu.
Pamoja na ukimya wa Serikali kuhusu wizi huo,
tumetiwa moyo na hatua ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha za Serikali
(PAC), ambayo imemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali
(CAG), Ludovick Utouh kuchunguza upotevu huo wa kiasi hicho kikubwa cha
fedha ambacho kilitumika pasipo maelezo katika kipindi cha miaka miwili
ya fedha cha 2012/13 na 2013/14.
Wasiwasi wa kamati hiyo ni kwamba kuna uwezekano
mkubwa wa kuwapo kwa mtandao mkubwa wa wizi wa fedha za Serikali katika
Wizara ya Fedha. Jambo hilo limethibitishwa na vitendo vya wizi wa
kimtandao ambavyo vimekuwa vikifanywa na baadhi ya watumishi wake
wakishirikiana na baadhi ya watendaji wa Tamisemi.
Ugumu uliopo hapa ni kwamba haijulikani kama fedha
hizo zilizopotea zilitokana na kodi za wananchi au wafadhili ambao
walichangia Sh842 bilioni katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2012/13. Ni
sahihi kabisa kwa Kamati hiyo ya Bunge kushangazwa na kuendelea kuwapo
kwa vitendo vya ufisadi serikalini, hasa kwa kuzingatia ukweli kwamba
ripoti za CAG kila mwaka zimekuwa zikifichua wizi wa mabilioni ya fedha
katika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa. Kujirudia kwa vitendo hivyo
kila mwaka ni ishara kwamba Serikali haina dhamira ya kupambana na
vitendo hivyo.
Mwenendo huo wa Serikali unashangaza, hasa
kutokana na ukweli kwamba mwaka 2013/14 ilikuwa na nakisi ya Sh847
bilioni katika bajeti yake. Hivyo, utekelezaji wa mipango yake ya
maendeleo ingekwama kama siyo kukopa mabilioni ya fedha kutoka vyanzo
vya nje na ndani ya nchi.
Matokeo yake ni kuzidi kuongeza mzigo wa Deni la
Taifa ambalo limefikia Sh27 trilioni sasa, huku ikishindwa kukusanya
kodi na kupanua wigo wa vyanzo vya kodi. Ndiyo maana iko hoi kifedha na
karibu shughuli zake zote zimesimama, huku ikisuasua kulipa mishahara ya
watumishi wake.
Pamoja na hali hiyo mbaya kifedha, bado vitendo
vya wizi na ufisadi serikalini vinaendelea kama tunavyoshuhudia
vikishamiri katika Wizara ya Fedha. Ni jukumu la Serikali kudhibiti
ubadhirifu na ufisadi miongoni mwa watumishi wake, vinginevyo uchumi
wetu utazidi kudidimia. Kwa kuanzia iwasake na kuwawajibisha wote
walioiba Sh480 bilioni kutoka Hazina.
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment