CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimewataka wafanyakazi
wa serikali na umma nchini kote kuondoa hofu ya kukosa ajira endapo
chama hicho kitaingia madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu mwakani.
Hayo yamebainishwa jana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod
Slaa, katika hotuba zake kwenye mikutano tofauti ya Operesheni M4C
Pamoja Daima inayoendelea nchini kote, yenye lengo la kuwaunganisha
Watanzania kuelekea chaguzi zijazo, ukiwemo Uchaguzi Mkuu.
Akifafanua zaidi kuhusu hofu iliyojengeka kwa wafanyakazi wengi
nchini kutokana na propaganda zinazoenezwa na viongozi wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), alisema kuwa kamwe chama hicho hakitawabagua au
kuwaondoa kazini wafanyakazi wa serikali, kwa sababu tu walikuwa kwenye
serikali iliyokuwepo madarakani.
“Ni mtu mwenye akili finyu tu ndiye anaweza kufikiria hivyo, kwa
sababu CHADEMA kaiwezi kuongoza kuwaondoa wafanyakazi wa serikali
waliopo sasa na kutegemea wafanyakazi wapya, wapo wanaosema eti
CHADEMA ikiingia madarakani watatoa wapi wafanyazi, au Ikulu wataipata
wapi, hao waliopo ambao ni wasafi ndio watakaoendeleza gurudumu,”
alifafanua.
Alisema Ikulu iliyopo si mali ya CCM au chama chochote ni mali ya
serikali na kiongozi atakayechaguliwa kutoka chama chochote atakwenda
Ikulu hiyo hiyo na wafanyakazi waliopo ndio watakaoendelea kuitumikia
serikali hiyo mpya.
“Kwa hiyo nawataka wafanyakazi wote nchini wakiwemo askari polisi na
wanajeshi waondoe hofu hiyo, tutakachofanya ni kuchuja wafanyakazi
waadilifu na wasio waadilifu, kwa mfano askari polisi ambaye ni mla
rushwa au mfanyakazi ambaye ni fisadi, hatutakuwa naye,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, Dk. Slaa amemtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, kutekeleza kauli yake
aliyoitoa hivi karibuni kwamba serikali itamega sehemu ya ardhi
aliyopewa mwekezaji katika mashamba ya mpunga mkoani Mbeya ili
kuwarudishia wananchi ambao wanahangaika kutafuta ardhi ya kilimo.
Alisema serikali mara nyingi imekuwa na kauli zisizotekelezeka, hivyo kuwafanya wananchi kutokuwa na imani na serikali yao.
Aidha, katika hotuba zake hizo, Dk. Slaa amemtaka Msajili wa Vyama
vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, kukemea na kuchukua hatua kwa
vyama ambavyo vinaweka makambi ya kuwafundisha vijana wao kufanya
vurugu, ikiwamo kupiga watu wakati wa uchaguzi.
Alisema CHADEMA kimekuwa chama kivumilivu sana kutokana na vurugu
hizo ambazo mpaka sasa zinafanyika katika baadhi ya miji, jambo ambalo
linahatarisha amani nchini.
“CHADEMA hatuamini katika vurugu, lakini tuna uwezo wa kujitetea,
vijana wetu wamepigwa na wengine kupoteza maisha kutokana na vurugu
zinazofanywa na vijana wanaoitwa Green Guards, tunaamini msajili
aliyepo sasa atalifanyika kazi jambo hili, kama mnavyojua hata hapa
Mbeya yapo makambi ambayo yanaendelea kutoa mafunzo hayo,” aliongeza
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment