DOLA BILIONI 3 ZA KIMAREKANI KUTUMIKA KUTEKELEZA MRADI WA LIGANGA NA MCHUCHUMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Na Benedict Liwenga, MAELEZO
 
JUMLA ya dola Bilioni 3 za Kimarekani zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa  Mgodi wa Makaa ya  Mawe na Chuma wa Liganga na Mchuchuma.
 
Kauli hiyo imetolewa  na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage wakati akiongea na Waandishi wa habari mini Dodoma.
 
Amesema mradi huo unaojengwa kwa ubia kati ya Tanzania Kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Kampuni ya China ya Sichuan Hongda Group unatarajia kuanza mwaka huu.
 
Mhe. Mwijage amesema kuwa fedha za kuwalipa fidia wananchi wanaozunguka maeneo ya mradi huo ziko tayari ambapo zinatarajiwa kutumika zaidi ya bilioni 13 kwa ajili ya fidia na makazi.
 
Alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasadia kuzalisha umeme Megawati 600 ambapo 250 zitatumika katika Kiwanda cha Chuma na nyingine 350 zitapelekwa kwenye Gridi ya Taifa kwa ajili ya kuongeza nguvu katika nishati ya umeme.
 
‘’Pamoja na kuchimba chuma, Mradi wa Mchuchuma na Liganga utahusisha ujenzi wa Kinu cha Umeme chenye uwezo wa Megawati 600”, alisema Mhe. Mwijage.
 
Ameongeza kuwa, Tanzania kwa sasa itakuwa na umeme wa gesi, maji na umeme wa makaa ya mawe ambapo umeme wa makaa ya mawe utakuwa msaada mkubwa kwa nchi kwani hautegemei tabianchi kama ilivyo vyanzo vingine vya umeme.
 
Mhe. Mwijage amesema kuwa katika mradi huo, Tanzania itakuwa na hisa asilimia 20 na Mwekezaji kutoka China atakuwa na asilimia 80, lakini hisa za Tanzania zinaweza kuongezeka hadi kufikia 45.
 
Chini ya mradi huo, Mwekezaji huyo anatakiwa kutoa elimu kwa Vijana katika ngazi zote za teknolojia zitakazohusika kutengeneza mgodi huo.
 
‘’Tutafundisha vijana wetu kwa ngazi tofauti kwani kampuni hii ni ya ubia kati ya Tanzania na China, tuna mamlaka sawa, tuna Wakurugenzi wetu wa Tanzania ndani ya hiyo kampuni, kwahiyo tutashiriki na hatutakuwa watazamaji”, alisema Mhe. Mwijage.
 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayosimamia Viwanda, Biashara na Uwekezaji ambaye pia ni Mtaalam katika masuala ya madini, Mhe. Dkt. Dalaly Kafumu amesema kuwa, lengo la kuwajengea makazi wakazi wa maeneo ya mradi huo ni kuwawezesha wakazi hao kuwa na uhusiano mzuri na mgodi unaotarajiwa kujengwa.
 
‘’Serikali imeamua kuwajengea makazi wananchi ambao wanazunguka mradi Ili kuepusha wakazi hao kutumia pesa watakayolipwa kama fidia kwa matumizi mengine na kukosa makazi baadaye kuja kuilaumu Serikali kwamba imewadhulumu kwa kutowapa pesa za kutosha za kujenga nyumba”, alisema Dkt. Kafumu.
 

Halmashauri ya Mji Njombe yapongezwa kwa miradi

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Njombe wakifuatana na wataalamu kutoka Halmashauri ya Mji Njombe wakikagua ujenzi wa mradi wa kituo kipya cha mabasi, unaoendelea katika eneo la Mji Mwema jana. Wa pili kushoto ni Mhandisi Mshauri kutoka Masasi Construction akionesha ujenzi wa njia za kutokea mabasi. (Na Mpigapicha Maalumu).
KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Njombe, imepongeza jitihada zinazofanywa na Halmashauri ya Mji wa Njombe katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwenye ujenzi wa miradi mbalimbali.
Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi hiyo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Edward Mgaya alisema amefurahishwa na jinsi Halmashauri kupitia mapato ya ndani imekuwa ikitoa fedha kusaidia uendelezaji wa miradi hiyo.
“Mkurugenzi na Mwenyekiti napenda niwapongeze kwa jitihada nzuri mnazofanya. Miradi yenu ni mizuri na wakandarasi wenu wapo vizuri. Miradi ipo imara, thamani ya hela iliyotumika inaonekana na ninaamini mpaka kufikia mwaka 2020 Halmashauri itakuwa imepiga hatua kubwa sana kimaendeleo kwani miradi mingi itakuwa imekamilika na imeanza kutumika,” alisema Mgaya na kuongeza:
“Napenda pia niwapongeze wataalamu wa Halmashauri ya Mji Njombe kwa kazi nzuri ya usimamizi wa miradi hii. Kazi inaridhisha.” Aliongeza, “Nimefurahishwa zaidi pia na wananchi ambao wamekuwa hawaisubiri serikali kufanya kila kitu.
Tumeona kuna baadhi ya miradi ambayo imejengwa kwa nguvu za wananchi wenyewe na Halmashauri nayo inaongezea fedha ili kukamilisha miradi hiyo.” Alisema hilo ni jambo jema na angependa wananchi katika maeneo mengine ya Njombe, waige mfano huu, na inasikitisha pale unapopita na kuona miradi mingine imesimama kutokana na ukosefu wa fedha na wananchi wa eneo husika hawaoneshi ushirikiano wa aina yoyote ile na badala yake wanatupia lawama serikali na kusahau kuwa miradi hiyo inapokamilika inakuwa ni kwa manufaa yao zaidi.
Jumla ya miradi yenye thamani ya zaidi ya Sh 6,905,588,815 imekaguliwa, ikihusisha miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na vyoo katika shule za msingi na sekondari, ujenzi wa zahanati, ujenzi wa mradi wa maji, kituo cha kukusanyia maziwa, ujenzi wa kituo kipya cha mabasi, ujenzi wa vyumba vya maduka, ujenzi wa mabweni na ujenzi wa nyumba za walimu katika shule za sekondari.

Chanzo Gazeti la Habari Leo

Mtihani wa Kidato cha Sita unaendelea vizuri

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 



Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako

BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA) limesema Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita na ule wa Ualimu, umeanza vizuri katika maeneo yote nchini. Akizungumza jana ikiwa ni siku ya pili tangu kuanza kwa mtihani wa taifa, Ofisa Habari wa Necta, John Nchimbi alisema mtihani huo umeanza kwa wakati uliopangwa na umefanyika katika hali ya utulivu na na amani.
“Taarifa za kanda zote zinaonesha kuwa mtihani umeanza vizuri maeneo yote, kwa wakati na umefanyika katika mazingira ya utulivu kama taratibu za mtihani zinavyotaka,” alisema Nchimbi. Mtihani wa Kidato cha Sita ulianza Jumatatu na utafanyika hadi Mei 19, mwaka huu wakati ule wa Ualimu utafikia tamati Mei 13, mwaka huu.
Jumla ya watahiniwa 74,920 wanafanya mtihani wa kuhitimu Kidato cha Sita katika shule mbalimbali nchini huku watahiniwa 11,597 wakifanya mtahini wa ualimu. Kati ya watahiniwa hao waliosajiliwa, watahiniwa 65,610 ni watahiniwa wa shule huku watahiniwa wa kujitegemea wakiwa 9,310.
Kati ya watahiniwa wa shule 65, 610, wasichana ni 24,549 na wavulana ni 41,061 huku watahiniwa wa kujitegemea wasichana wakiwa ni 3,176 na wavulana ni 6,134. Kwa upande wa mtihani wa ualimu, watahiniwa 11,597 wanafanya mtihani wa Ualimu.
Kati ya hao watahiniwa 10,942 wanafanya mtihani wa Ualimu daraja A na watahiniwa 654 wanafanya mtihani wa Diploma ya sekondari na mmoja anafanya mtihani wa Ualimu wa Diploma ya Ufundi.
Chanzo Gazeti la Habari leo
 

KAMATI YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI YAKAGUA MIRADI YA UMEME VIJIJINI MKOANI NJOMBE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wameendelea na ziara ya kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya Wizara husika ambapo mwishoni mwa wiki hii walitembelea miradi ya umeme vijijini, mkoani Njombe.

Miradi waliyotembelea Wajumbe hao ni pamoja na wa ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovolti 220 kutoka Makambako hadi Songea na usambazaji umeme kwenye vijiji vya mikoa ya Njombe na Ruvuma.

Vilevile, Kamati ilitembelea maeneo ya vijiji mbalimbali mkoani Njombe ambako miradi ya umeme vijijini inatekelezwa kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Pili.

Aidha, Kamati ilipata fursa kuzungumza na baadhi ya wananchi wa vijiji husika ambako miradi hiyo ya umeme inatekelezwa na kusikiliza maoni yao.

Baada ya ziara mkoani Njombe, Kamati hiyo itatembelea Mkoa wa Mbeya, eneo la Kiwira katika Mradi wa Makaa ya Mawe na baadaye itaelekea Biharamulo kukagua mgodi wa dhahabu wa Tulawaka.

Awali, Kamati ilifanya ziara mkoani Mtwara ambapo ilitembelea Mtambo wa kuchakata gesi asilia wa Madimba pamoja na Kiwanda cha kutengeneza Saruji cha Dangote. Pia, Wajumbe wa Kamati hiyo walitembelea machimbo ya Tanzanite yaliyopo Mirerani mkoani Manyara.
Mkandarasi anayesambaza umeme vijijini kwa Mkoa wa Njombe, kutoka Kampuni ya Lucky Exports Ltd (wa tatu kutoka kushoto), akimwonesha na kumpa maelezo kuhusu transfoma iliyofungwa katika Kijiji cha Isindagosi – Njombe, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Ussi Pondeza, wakati wa ziara ya kamati hiyo mkoani humo hivi karibuni kukagua miradi ya umeme vijijini.
Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Njombe, Mhandisi Emmanuel Kachewa (mwenye suti ya bluu-kushoto), akiwapa maelezo wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, kuhusu sehemu ya kuchukulia umeme (taping point) iliyopo kijiji cha Italahumba – Njombe, wakati wa ziara ya Kamati hiyo kukagua miradi ya umeme vijijini mkoani humo hivi karibuni.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Njombe ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Anatory Choya, akiwasilisha taarifa fupi ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ya Mkoa wake kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, walipotembelea mkoani humo hivi karibuni kukagua utekelezwaji wa miradi ya umeme vijijini.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Madini, Profesa James Mdoe (wa pili kutoka kulia) akijadiliana jambo na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anatory Choya (kulia), wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini (hawapo pichani), mkoani humo hivi karibuni, kukagua utekelezwaji wa miradi ya umeme vijijini. Wa kwanza kushoto ni Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje.
Mwananchi kutoka Kijiji cha Ihanzutwa – Njombe, Karison Mgoba akitoa maoni yake kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, kuhusu utekelezwaji wa miradi ya umeme vijijini, hususan katika kijiji chake.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakiwa katika ziara kukagua miradi ya umeme vijijini mkoani Njombe hivi karibuni.
Meneja wa Mradi wa Ujenzi wa Njia ya Umeme wa Msongo wa Kilovolti 220 kutoka Makambako hadi Songea, Mhandisi Didas Lyamuya, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakati Wajumbe wa Kamati hiyo walipokuwa ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, kabla ya kutembelea miradi ya umeme vijijini inayotekelezwa mkoani humo.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Ussi Pondeza, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Isindagosi – Njombe kuhusu miradi ya umeme vijijini inayotekelezwa mkoani humo, wakati wa ziara ya Kamati hiyo hivi karibuni. Wa kwanza kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Madini, Profesa James Mdoe.
Mmoja wa wananchi katika kijiji cha Isindagosi – Njombe, akitoa maoni yake kuhusu utekelezwaji wa miradi ya umeme vijijini kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakati Kamati hiyo ilipofanya ziara mkoani humo hivi karibuni kutembelea miradi ya umeme vijijini.
Baadhi ya Maafisa wa Wizara ya Nishati na Madini wakiwaongoza Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, kutembelea miradi ya umeme vijijini inayotekelezwa mkoani Njombe hivi karibuni.

Sara Dumba kuzikwa kesho

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Sara Dumba enzi za uhai wake
MKUU wa Wilaya ya Njombe, Sara Dumba aliyefariki ghafla juzi jioni, anatarajiwa kufanyiwa ibada leo mjini Njombe na kuagwa rasmi na wananchi wa wilaya hiyo na Mkoa wa Njombe na baadaye jioni kusafirishwa kuja jijini Dar es Salaam ambako ndiko atakapozikwa.
Kwa mujibu wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Jackson Saikadau, ratiba ya awali inaonesha kuwa Dumba anatarajiwa kuzikwa kesho nyumbani kwake eneo la Mbutu Mwembe Mdogo Kigamboni na msiba wake utafanyika Kigamboni nyumbani kwa baba yake mzazi eneo la Ferry Midizini.
Saikadau alisema ratiba hiyo inaonesha kuwa mwili wa marehemu ambao baada ya mauti ulihifadhiwa katika Hospitali ya Ilembula, utawasili mjini Njombe saa nne asubuhi kwa ajili ya ibada na baadaye kuagwa na wananchi.
“Tunatarajia kuanza safari majira saa 10 jioni kutoka Njombe kwenda Dar es Salaam na maiti itawasili jijini humo alfajiri siku ya Alhamisi (kesho) kwa ajili ya taratibu za msiba na mazishi,” alisema Saikadau. Alisema Dumba alifariki ghafla juzi baada ya kusumbuliwa na tatizo la shinikizo la damu.
Alisema kabla ya mauti, alilalamika kusumbuliwa na kichwa na hivyo kukimbizwa katika Hospitali ya Kibena, lakini pamoja na jitihada za madaktari za kuokoa maisha yake, alifariki dunia majira ya saa moja na nusu usiku.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Makete, Daudi Yassin alisema mkoa umepata pigo kwa kuondokewa na Dumba ambaye katika uhai wake ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Wakuu wa Wilaya wa mkoa huo wa Njombe.
“Kwa kweli huu msiba umetushtua sana, kwani Jumamosi iliyopita tulikuwa na Dumba katika sherehe za kumpokea Mkuu wetu wa Mkoa, Rehema Nchimbi baada ya kuapishwa, kwa kweli mchango wake utakumbukwa sana,” alisema Yassin.
Kitaaluma Dumba ni Mwandishi wa Habari aliyekuwa mtangazaji wa iliyokuwa Radio Tanzania ambao kwa sasa inajulikana kama Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Aidha, alishika nyadhifa mbalimbali za ukuu wa wilaya katika maeneo tofauti zikiwemo wilaya za Kilindi na Njombe alikofikwa na mauti.
Katika hatua nyingine, Rais John Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk Rehema Nchimbi kutokana na kifo cha ghafla cha Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sara Dumba.

Chanzo Gazeti la Habari leo

Vyama vya ushirika Hufa kutokana na madeni makubwa

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

WANAWAWAKE KUMILIKI ARDHI BADO NI NDOTO MAKETE MKOANI NJOMBE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Hii  ni Ofisi ya afisa Mtendaji Kata ya Iwawa, Kituo cha wakulima

Na Blogs za Mikoa Tanzania
Mila potofu zinazokandamiza wanawake zimeripotiwa kuendelea kushamiri katika baadhi ya mambo baada ya kutembelea katika maeneo tofauti tofauti ya wilaya ya Makete mkoani Njombe na kuzungumza na wakazi wa wilaya hiyo

Katika kijiji cha Iwawa wilaya ya Makete mkoani Njombe mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la Jane Sanga amesema wanawake wengi wilayani hapo hawamiliki ardhi kutokana na mila potofu kuwa wamiliki wa ardhi ni wanaume pekee
"Kwa hapa Makete wanawake unaowaona wanamiliki ardhi kwa kiasi kikubwa unakuta ni mjane anaimiliki baada ya kufiwa na mumewe au unakuta mwanamke huyo ana uwezo wa kifedha na ameamua kukunua kipande chake cha ardhi na anakimiliki mwenyewe, hapo hakuna anayemuingilia, na hata wale wajane bado utakuta wanasumbuliwa na ndugu wa marehemu mumewe, kwa hiyo bado hali ni ngumu" amesema Jane
Hiki ni kipande kidogo sana ambacho analima Bi. Jane(Hayupo Pichani)

Mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Grace Mbilinyi ambaye amekutwa na mwandishi wetu akiandaa shamba kwa ajili ya kilimo cha mazao ya chakula katika msimu ujao, amesema anamiliki shamba aliloachiwa na marehemu mumewe, licha ya kuendelea kusumbuliwa na ndugu wa marehemu wakidai kuwa mwanamke hataweza kuendeleza ardhi aliyoachiwa na mumewe

"Kwa kweli ni shida lakini Tutafanyaje sasa, mimi ni mama  wa nyumbani ambaye sana sana najishughulisha na ujasiriamali na kilimo kama hivi, kwa sasa ninamiliki hili shamba nililoachiwa na mume wangu kwa ajili ya kilimo, lakini vijimaneno vya ndugu vipo lakini bado sikati tamaa maana uwezo wa kumiliki ninao, na nitaiendeleza kwa kilimo" amesema Bi Grace

James Sigala ni mkazi wa Makete ambaye amekiri kuwepo kwa mila hizo zinazokandamiza wanawake hasa katika umiliki wa ardhi na kusema ingawa elimu inaendelea kutolewa na wanaharakati lakini bado kuna haja ya kuendelea kuitoa ili jamii ibadilike na kuamini kuwa hata wanawake wanaweza kimilikishwa ardhi kama wanaume
Afisa mtendaji kata ya Iwawa Bw. Festo Msigwa akiongea na mwandishi wa Blogs za Mikoa

Blog za Mikoa kupitia Njombe yetu  haikuishia hapo imebisha hodi katika ofisi za kata ya Iwawa iliyoko katika mji mdogo wa Iwawa (Makete Mjini) na kukutana na afisa Mtendaji Bw. Festo Msigwa ambaye amekiri kuwa bado umilikishwaji au umiliki wa ardhi kwa wanawake ni mdogo kutokana na mila potofu 

Amesema katika kata yake zipo kesi za ardhi zinazoletwa katika ofisi yake zikiwemo za wanawake wajane kupokonywa umiliki wa ardhi kutoka kwa ndugu wa mume wake kwa madai kuwa yeye kama mwanamke hawezi kumiliki wala kuiendeleza jambo ambalo limepingwa na kulaaniwa vikali na mtendaji huyo

"Wanawake wanaweza kwanza katika shughuli za shambani wao ndio wachakarikaji kuliko sisi wanaume, fikiria kwa mfano hawa wajane wanaokuja kwenye kesi za ardhi katika baraza la ardhi hapa, unakuta wakati wa uhai wa waume zao wao ndio walikuwa walimaji wazuri na watunzaji wakubwa wa mashamba, sasa kama aliweza toka mwanzoni iweje sasa washindwe" amesema Msigwa

Machi 8 mwaka huu ni kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambapo kwa wilaya ya Makete maadhimisho yatafanyika katika kata ya Iwawa katika mji mdogo wa Iwawa

NAIBU WAZIRI WA AFYA DK. KIGWANGALLA AUPA SIKU 90 UONGOZI WA HOSPITALI YA MKOA WA NJOMBE-KIBENA KUBORESHA HUDUMA ZAKE LA SIVYO KUIFUNGIA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
DSC_0068

Naibu Waziri Dk. Kigwangalla akikagua mahabara ya hospitali hiyo ambayo alikutana na matatizo mbalimbali ikiwemo mashine na vifaa kutotumika ipasavyo na kuagiza uongozi wa kufanya maboresho ndani ya miezi mitatu huku akiahidi kuifungia endapo itashindwa kutekeleza maagizo hayo.

kigwangaccszz

Naibu Waziri wa Afya, Dk Kigwangalla akiangalia moja ya maeneo ya wodi hizo ambapo alikuta hali ya uchafu pamoja na kuwa na mpangilio mbovu wa namna ya utoaji wa huduma.

kigwanj

Dk. Kigwangalla akitoa maelezo kwa Mganga mkuu wa hospitali ya Mkoa wa Njombe-Kibena, Dk. Samwel Mgema wakati wa maagizo hayo ndani ya siku 90 na endapo hawatafanya utekelezaji ataichukuia hatua ya kuifungia.

kigwaza

Naibu Waziri wa Afya, Dk Kigwangalla akielekea kwenye baadhi ya majengo ya hospitali hiyo wakati wa ukaguzi huo.

Kigwangala

Naibu Waziri wa Afya, Dk Kigwangalla akikagua eneo la kutolea huduma ikiwemo wagonjwa wanaoingia kumuonna Daktari. (Picha zote na Andrew Chale,modewjiblog-Njombe).

Uongozi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Njombe umepewa muda wa siku 90 kurekebisha mapungufu ya utoaji wa huduma za afya, lazima hospitali hiyo itafungwa.
Kauli hiyo imetolewa jana jioni na Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi Kigwangalla wakati akizungumza na viongozi Mganga Mkuu wa Mkoa, Samwel Mgema na na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Imelda Mwenda na watumishi wa hospitali hiyo.
Dkt. Kigwangalla alitoa agizo kufuatia ziara yake ya ukaguzi wa hospitali, vituo vya afya na zahati ili kuweza kubaini changamoto na mafanikio waliyoyapata baada maagizo mbalimbali kutolewa na Serikali.
Miongoni mwa maagizo hayo ni uboreshaji wa huduma kwa kuwepo na vifaa tiba na vya maabara za kisasa, dawa za kutosha, kuaanza malipo ya mtandao.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri huyo alibaini kwamba hospitali hiyo haina baadhi ya vifaa vya maabara, ambavyo ni muhimu kwa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali, ikiwemo mashine ya CT-Scan na kuwepo kwa vifaa vibovu ambayo havijafanyiwa matengenezo, ukiwemo mfumo mbovu wa ukusanyaji taka ngumu na nyepesi.
“Sijaridhishwa na uendeshaji wa hospitali hii na utoaji wa huduma zinazotolewaa ninakuagiza Mganga Mkuu wa Wilaya, John Luanda kurekebisha mapungufu yaliyopo baada ya miezi mitatu nitarudi nikikuta huduma bado hairidhishi nitakifunga kituo.,” alisema Dkt.Kigwangalla.
Aliongeza kuwa akikuta huduma hadhirishi atafunga hospitali hiyo licha ya kuwa ya Serikali, hivyo hatasubiri kutumbuliwa jipu.
Dkt. Kigwangalla aliutaka uongozi wa hospitali hiyo kuandaa mpango kazi na mkakati wa kuboresha mapungufu yaliyopo katika hospitali hiyo na kuuwasilisha kwake.
Aliutaka uongozi wa hospitali huo kujenga chumba cha upasuaji cha wakina mama na watoto.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa Njombe, Mgema alisema watatekeleza maagizo hayo.

KIPINDUPINDU CHAINGIA PAWAGA, 20 WALAZWA.

WAKAZI wa Kijiji cha Mbolimboli Kata ya Pawaga wilayani Iringa, wamekumbwa na ugonjwa wa kipindupindu.
Hadi jana watu 20 waliripotiwa kuwekwa karantini, wakiugua ugonjwa huo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Robert Salim alisema ugonjwa huo umelipuka baada ya eneo hilo kukumbwa na mafuriko.
“Mafuriko hayo yamesababisha uchafu wa vyoo vilivyobomoka na mwingine kusambaa hadi katika visima vya maji yanayotumiwa na wakazi wa eneo hilo,” alisema Dk Salim.

Aliongeza kuwa wagonjwa hao 20, wamepokewa na kuweka katika kambi maalumu kijijini hapo wakiwa wanatapika na kuharisha mfululizo.
Alisema wengi wa waliothiriwa na ugonjwa huo ni wakazi wa Wilaya ya Kilolo, waliokwenda katika kijiji hicho kufanya kazi ya vibarua katika mashamba ya mpunga.

Alisema Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewapatia dawa na vifaa tiba kunusuru maisha ya watu hao. Dk Salim alionya wakazi wa Pawaga wasipodhibiti ugonjwa huo, utasambaa katika maeneo mengi ya mkoa wa Iringa.
“Halmashauri zote zimekwishajulishwa kuchukua tahadhari na kuelimisha jamii kuzingatia usafi, matumizi ya vyoo bora na kutokula ovyo ovyo ili kujiepusha na maambukizi ya ugonjwa huo,” alisema.

Alisema halmashauri hizo, zinatakiwa kufunga sehemu za biashara za vyakala zinazoendeshwa katika mazingira ya uchafu na wahudumu ambao hawajapima afya zao.
“Agizo hilo linatakiwa kwenda sambamba na kuudhibiti uuzaji wa vyakula na matunda yaliyomenywa katika sehemu zisizoruhusiwa,” alisema.
CHANZO: GAZETI LA HABARI LEO.

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa