WAKAZI wa Kijiji cha Mbolimboli Kata ya Pawaga wilayani Iringa, wamekumbwa na ugonjwa wa kipindupindu.
Hadi jana watu 20 waliripotiwa kuwekwa karantini, wakiugua ugonjwa huo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk
Robert Salim alisema ugonjwa huo umelipuka baada ya eneo hilo kukumbwa
na mafuriko.
“Mafuriko hayo yamesababisha uchafu wa vyoo vilivyobomoka na mwingine
kusambaa hadi katika visima vya maji yanayotumiwa na wakazi wa eneo
hilo,” alisema Dk Salim.
Aliongeza kuwa wagonjwa hao 20, wamepokewa na kuweka katika kambi
maalumu kijijini hapo wakiwa wanatapika na kuharisha mfululizo.
Alisema wengi wa waliothiriwa na ugonjwa huo ni wakazi wa Wilaya ya
Kilolo, waliokwenda katika kijiji hicho kufanya kazi ya vibarua katika
mashamba ya mpunga.
Alisema Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
imewapatia dawa na vifaa tiba kunusuru maisha ya watu hao. Dk Salim
alionya wakazi wa Pawaga wasipodhibiti ugonjwa huo, utasambaa katika
maeneo mengi ya mkoa wa Iringa.
“Halmashauri zote zimekwishajulishwa kuchukua tahadhari na kuelimisha
jamii kuzingatia usafi, matumizi ya vyoo bora na kutokula ovyo ovyo ili
kujiepusha na maambukizi ya ugonjwa huo,” alisema.
Alisema halmashauri hizo, zinatakiwa kufunga sehemu za biashara za
vyakala zinazoendeshwa katika mazingira ya uchafu na wahudumu ambao
hawajapima afya zao.
“Agizo hilo linatakiwa kwenda sambamba na kuudhibiti uuzaji wa
vyakula na matunda yaliyomenywa katika sehemu zisizoruhusiwa,” alisema.
CHANZO: GAZETI LA HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment