Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kwa mujibu wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Jackson Saikadau,
ratiba ya awali inaonesha kuwa Dumba anatarajiwa kuzikwa kesho nyumbani
kwake eneo la Mbutu Mwembe Mdogo Kigamboni na msiba wake utafanyika
Kigamboni nyumbani kwa baba yake mzazi eneo la Ferry Midizini.
Saikadau alisema ratiba hiyo inaonesha kuwa mwili wa marehemu ambao
baada ya mauti ulihifadhiwa katika Hospitali ya Ilembula, utawasili
mjini Njombe saa nne asubuhi kwa ajili ya ibada na baadaye kuagwa na
wananchi.
“Tunatarajia kuanza safari majira saa 10 jioni kutoka Njombe kwenda
Dar es Salaam na maiti itawasili jijini humo alfajiri siku ya Alhamisi
(kesho) kwa ajili ya taratibu za msiba na mazishi,” alisema Saikadau.
Alisema Dumba alifariki ghafla juzi baada ya kusumbuliwa na tatizo la
shinikizo la damu.
Alisema kabla ya mauti, alilalamika kusumbuliwa na kichwa na hivyo
kukimbizwa katika Hospitali ya Kibena, lakini pamoja na jitihada za
madaktari za kuokoa maisha yake, alifariki dunia majira ya saa moja na
nusu usiku.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Makete, Daudi Yassin alisema mkoa umepata pigo
kwa kuondokewa na Dumba ambaye katika uhai wake ndiye aliyekuwa
Mwenyekiti wa Wakuu wa Wilaya wa mkoa huo wa Njombe.
“Kwa kweli huu msiba umetushtua sana, kwani Jumamosi iliyopita
tulikuwa na Dumba katika sherehe za kumpokea Mkuu wetu wa Mkoa, Rehema
Nchimbi baada ya kuapishwa, kwa kweli mchango wake utakumbukwa sana,”
alisema Yassin.
Kitaaluma Dumba ni Mwandishi wa Habari aliyekuwa mtangazaji wa
iliyokuwa Radio Tanzania ambao kwa sasa inajulikana kama Shirika la
Utangazaji Tanzania (TBC).
Aidha, alishika nyadhifa mbalimbali za ukuu wa wilaya katika maeneo
tofauti zikiwemo wilaya za Kilindi na Njombe alikofikwa na mauti.
Katika hatua nyingine, Rais John Magufuli amemtumia salamu za
rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk Rehema Nchimbi kutokana na kifo
cha ghafla cha Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sara Dumba.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment