KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Njombe,
imepongeza jitihada zinazofanywa na Halmashauri ya Mji wa Njombe katika
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwenye ujenzi wa miradi
mbalimbali.
Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi hiyo, Mwenyekiti wa
CCM Wilaya, Edward Mgaya alisema amefurahishwa na jinsi Halmashauri
kupitia mapato ya ndani imekuwa ikitoa fedha kusaidia uendelezaji wa
miradi hiyo.
“Mkurugenzi na Mwenyekiti napenda niwapongeze kwa jitihada nzuri
mnazofanya. Miradi yenu ni mizuri na wakandarasi wenu wapo vizuri.
Miradi ipo imara, thamani ya hela iliyotumika inaonekana na ninaamini
mpaka kufikia mwaka 2020 Halmashauri itakuwa imepiga hatua kubwa sana
kimaendeleo kwani miradi mingi itakuwa imekamilika na imeanza kutumika,”
alisema Mgaya na kuongeza:
“Napenda pia niwapongeze wataalamu wa Halmashauri ya Mji Njombe kwa
kazi nzuri ya usimamizi wa miradi hii. Kazi inaridhisha.” Aliongeza,
“Nimefurahishwa zaidi pia na wananchi ambao wamekuwa hawaisubiri
serikali kufanya kila kitu.
Tumeona kuna baadhi ya miradi ambayo imejengwa kwa nguvu za wananchi
wenyewe na Halmashauri nayo inaongezea fedha ili kukamilisha miradi
hiyo.” Alisema hilo ni jambo jema na angependa wananchi katika maeneo
mengine ya Njombe, waige mfano huu, na inasikitisha pale unapopita na
kuona miradi mingine imesimama kutokana na ukosefu wa fedha na wananchi
wa eneo husika hawaoneshi ushirikiano wa aina yoyote ile na badala yake
wanatupia lawama serikali na kusahau kuwa miradi hiyo inapokamilika
inakuwa ni kwa manufaa yao zaidi.
Jumla ya miradi yenye thamani ya zaidi ya Sh 6,905,588,815
imekaguliwa, ikihusisha miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na vyoo
katika shule za msingi na sekondari, ujenzi wa zahanati, ujenzi wa mradi
wa maji, kituo cha kukusanyia maziwa, ujenzi wa kituo kipya cha mabasi,
ujenzi wa vyumba vya maduka, ujenzi wa mabweni na ujenzi wa nyumba za
walimu katika shule za sekondari.
Chanzo Gazeti la Habari Leo
0 comments:
Post a Comment