Home » » CWT,TGNP,WATAKA BAJETI KUZINGATIA MAENEO MUHIMU

CWT,TGNP,WATAKA BAJETI KUZINGATIA MAENEO MUHIMU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Rais wa CWT, Gratian Mukoba
Chama cha Walimu  nchini (CWT) kimesema wananchi wanahitaji bajeti itakayowapatia mahitaji muhimu kama elimu, afya, maji na ulinzi.
Rais wa CWT, Gratian Mukoba (pichani) , alisema bajeti ya elimu inatakiwa kuwa asilimia sita ya pato la taifa, lakini hadi sasa bajeti inayotengwa na serikali ni asilimia moja.

Mukoba alisema bajeti nzuri ni ile ambayo inampatia mwananchi mahitaji ya vitu muhimu ambavyo wananchi wanatarajia kuvipata.

“Vitu kama elimu, afya, maji na ulinzi ni muhimu, watu wanahitaji, afya bora ili waweze kufanya kazi na kupata kipato, ulinzi ni muhimu kwani kuna makundi yameibuka kama ‘Panya wa Rwanda’ na ‘Mbwa mwitu’ ambayo yanahatarisha usalama wa wananchi, hivyo wananchi wanahitaji kusikia ulinzi unaimarishwa,” alisema Mukoba.

Alisema ili taifa hili liweze kuendelea na kukuza uchumi wake ni vyema serikali ikazingatia vipaumbele hivyo ili kuendelea  kuinua uchumi wa wananchi wake.

Nao Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), umesema   kama bajeti itakayosomwa leo haitazingatia  na kuweka vipaumbele muhimu kama afya na maji bado haitamsaidia mwananchi wa kawaida.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi, alisema katika mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), Wizara ya Afya haijahusishwa, suala ambalo ni hatari kwani jamii inahitaji kuwa na afya bora ili kufanya shughuli za maendeleo.

“Bajeti ya serikali bado haijaweza kumnufaisha mwananchi wa kawaida kama vile ambavyo wananchi wanatarajia, mfano masuala muhimu kama afya na maji ni miongozi mwa mambo ambayo bado yanawaumiza wanawake na vijana walioko pembezoni,” alisema Liundi.

Alisema kipaumbele cha sekta binafsi ambayo serikali imeboresha na kukuza uchumi wa nchi bado hakijaweza kumnufaisha mwananchi wa kawaida.

Alifafanua kuwa ukuaji wa uchumi bado haujawafikia au kuwanufaisha wananchi ambao wako pembezoni hasa wanawake na watoto.

Alisema kwa upande wa sekta ya usafirishaji bado pia haijaweza kuwanufaisha wananchi wa kawaida ambao ni wakulima wa mazao mbalimbali ambao wanatarajia kutumia barabara ili kusafirisha mazao yao.

CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa