Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkuu wa wilaya ya Makete mwenye suti nyeusi (aliyesuka nywele) Mh. Josephine Matiro,
mkurugenzi wa kituo cha sheria na haki za binadamu Helen Kijo Bisimba
(kulia kwa mkuu wa wilaya) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya
watoto walioshiriki maadhimisho hayo.
Mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro(wa
tatu kushoto walioketi) na Mkurugenzi wa kituo cha sheria na haki za
binadamu Helen Kijo Bisimba (wa pili walioketi kushoto) wakiwa katika
picha ya pamoja na wajumbe wa shirika la wasaidizi wa kisheria Makete
Katika picha ya pamoja na wanafunzi wa sekondari ya Iwawa Makete ambao nao walishiriki
Wanafunzi wa shule ya msingi Ndulamo wakiwa katika picha ya pamoja.(Picha/habari na Edwin Moshi na Conrad Mpila, Makete.)
Imeelezwa
kuwa ni jukumu la kila mmoja kuwasaidia watoto yatima na wanaoishi
katika mazingira hatarishi, na si kuiachia serikali ama mashirika yasiyo
ya kiserikali peke yao kufanya kazi hiyo
Kauli
hiyo imetolewa leo hii Juni 16 na mkuu wa wilaya ya Makete Mh.
Josephine Matiro ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku
ya mtoto wa Afrika yaliyofanyika kitaifa (kwa asasi zisizo za
kiserikali) katika viwanja vya mabehewani kata ya Iwawa wilayani Makete
mkoani Njombe
Hata hivyo mkuu wa wilaya hiyo amekiri kuwepo kwa changamoto ya
watoto walio wengi Wilayani Makete ambao ni Yatima na waishio katika
mazingira magumu ambao wanahitaji msaada wa kila mmoja
"Ni
kweli wilaya ya Makete ina watoto ambao ni yatima na wanaoishi katika
mazingira hatarishi, wengine wanalelewa katika vituo maalum vilivyopo
wilayani mwetu, hivyo ni jukumu letu kuwasaidia kila mtu kwa kadri ya
uwezo wake, mwenye sabuni, kalamu, fedha ama chochote anaweza kufanya
hivyo kwa wakati wake" amesema Matiro
Katika risala iliyosomwa na mwanafunzi Gaudencia Malangalila wa Shule ya
msingi Ndulamo kwa niaba ya wanafunzi wenzake amesema Kuwa watoto walio
wengi wanakabiliwa na unyanyasaji kwa kufanyishwa Kazi ngumu na
hatarishi,kutopata haki katika huduma za matibabu,walezi kunyang'anya misaada
wanayopewa na wadau mbalimbali
Naye Mkurugenzi wa kituo cha sheria na haki za binadamu (LHRC) Bi. Helen Kijo Bisimba amesema Kuwa kwa Tafiti alizofanya
amebaini Kuwa kuna watoto ambao waliondoka kwenda nje ya Makete kwa
kufanya Kazi na hawarudi tena huku wazazi hawajui Kama wapo hai au
la,kwani hata mawasiliano na wazazi ama walezi wao bado ni magumu
Hivyo amewasihi wazazi/walezi Kuwa makini na watoto wao pindi wanapoitwa
kwenda kufanya Kazi maeneo ya mbali kwani mara nyingi huko wanakokwenda
wanakutana na mambo ambayo ni kinyume na walioyatarajia
Katika maadhimisho hayo kikundi cha wazazi kutoka Kijiji cha Isapulano na Ndulamo Maarufu
Kama mama mkubwa wamesema Kuwa vikundi hivyo vitaendelea Kulinda haki za
watoto na kutoa ujumbe kwa jamii kwa njia ya sanaa na kufanya uchunguzi dhidi ya watoto wanaofanyiwa unyanyasaji
na watatoa taarifa katika ngazi husika na wakigundulikaa wahusika wachukuliwe hatua za kisheria
Kauli mbiu ya mwaka huu ni "kila mtoto ana haki ya elimu bora bila vikwazo"