SERIKALI
ya Tanzania kupitia Mamlaka ya U kanda Maalumu wa Uwekezaji nchini
(EPZA), inatarajia kuanza kupata wawekezaji wengi kutoka Jamhuri ya
Korea Kusini kwa faida ya nchi zote mbili.
Matarajio hayo yanatokana
na ziara iliyofanywa hivi karibuni na wawekezaji katika mamlaka hiyo na
kujionea maeneo maalumu ya uwekezaji na fursa zinazopatikana katika
maeneo hayo.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa
na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt. Adelhelm Meru, hatua hiyo ni
muhimu kwa nchi hizo mbili katika kuimarisha uchumi na uwekezaji
endelevu.
Ujumbe huo ulijumuisha wafanyabiashara wakubwa kutoka kampuni 22 za nchi hiyo.
"Wamekuja na ujumbe mkubwa sana na tunatarajia sasa kuanza kupata wawekezaji wengi kutoka nchi hii," alisema Dkt. Meru.
Ujumbe
wa wafanyabiashara hao uliongozwa na balozi wa nchi yao nchini
Tanzania, Chung H na ilikuwa ni mara ya kwanza kwa kundi kubwa la
wafanyabiashara wa nchi hiyo kuja nchini.
"Sisi tulitumia nafasi hii
kuwaonesha vivutio ambavyo vinarahisisha biashara na uwekezaji katika
maeneo yetu," alisema. Pia walioneshwa fursa zilizopo katika maeneo ya
mamlaka zikiwemo za kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani mazao ya
kilimo na madini kwa ajili ya masoko ya nje.
Fursa nyingine
zilizotajwa zilikuwa za ujenzi wa miundombinu ya nishati, maji na utoaji
wa huduma mbalimbali katika maeneo maalumu ya mamlaka hiyo yaliyopo
katika mikoa 20 hapa nchini.
Alisema maeneo maalumu ya vipaumbele ni pamoja na Bagamoyo, Mtwara na Kigoma ambayo yana fursa nyingi.
"Kwa
bahati nzuri tumekuwa tukifanya nao kazi kwa muda mrefu na tunajua wao
ni mabingwa wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)," alisema.
Naye
Balozi Chung H, alisema nchi yake inauhusiano mzuri na Tanzania na
ziara ya wafanyabiashara wa nchi yake inadhihirisha uhusiano huo.
"Tunahitaji kuzidi kuongeza ushiriki wa wafanyabiashara wetu kufanya biashara na nchi hii ya Tanzania," alisema.
Mkuu
wa ujumbe wa wafanyabiashara hao, Lee Kang Min, alisema wamekuja nchini
Tanzania kwa ziara ya kuangalia mazingira ya uwekezaji na wamefurahi
kuona fursa nyingi zilizopo.
"Tutarudi kuwekeza," alisema na
kuongeza kuwa wafanyabiashara hao waliridhika na hali halisi ya
mazingira ya uwekezaji na fursa zilizopo Tanzania. Wafanyabiashara hao
pia walifanya ziara katika kiwanda cha nguo kilicho katika eneo la
mamlaka hiyo cha Tanzania Tooku Garments Co. Ltd.
0 comments:
Post a Comment