SERIKALI
imewataka waajiri wote kuhakikisha wanaanzisha mifumo bora mahali pa
kazi itakayohakikisha wafanyakazi wao wana usalama na wenye afya bora.
Alisema
suala hilo si jambo la hiari kwani linagusa uhai na maisha ya
watu.Akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya afya na usalama mahali pa
kazi Duniani, Makamu wa Rais, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, aliwataka
waajiri wasikwepe wala kuogopa gharama katika hilo.
"Zingatieni kuwa hakuna kitu chenye thamani kuzidi uhai na maisha ya watu," alisema.
Alisema
takwimu za Shirika la Afya Duniani (ILO) zinaonesha kuwa Kila mwaka
duniani takriban watu milioni 337 hupata ajali kazini na kati yao
wafanyakazi milioni 2.3 hufariki kutokana na ajali na magonjwa
yatokanayo na kazi wanazofanya.
"Takwimu zinatuonesha kuwa watu
wanaofariki kutokana na magonjwa ya ajali kazini ni wengi kuliko wale
wanaofariki vitani, ni wazi kuwa ajali nyingi na magonjwa kazini
hutokana na wafanyakazi kutozingatia kanuni za usalama na afya kazini na
waajiri kutochukua hatua za kupunguza ajali na magonjwa hayo," alisema
Dkt. Bilal.
Alisema kila mfanyakazi anastahili kufanya kazi yenye
ujira wa kutosha kukidhi mahitaji ya msingi katika mazingira salama bila
kuhatarisha afya yake, kinyume na hapo kazi hiyo haitakuwa ya staha na
haipaswi kufanywa na binadamu yeyote, inayostahili kupigwa marufuku.
Hata
hivyo, alisema siku ya usalama na afya mahali pa kazi duniani ni siku
muhimu kimataifa ambapo nchi zote wanachama wa Shirika la Kazi Duniani
(ILO) tangu mwaka 2001 zilitakiwa kuadhimisha siku hiyo.
Pia alisema
maadhimisho hayo yanatoa fursa ya kubainisha njia mbalimbali za kuzuia
magonjwa na ajali zinazotokea kazini na kuimarisha kampeni za kuboresha
usalama afya na ustawi wa wafanyakazi wakiwa kazini.
Alisema
Serikali inafanya juhudi kubwa kuhakikisha inadhibiti matumizi yasiyofaa
ya kemikali sehemu za kazi na maeneo mengine kwa manufaa ya afya na
wananchi wake.
"Pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali madhara ya
kemikali yameendelea kuathiri jamii yetu kwa njia moja au nyingine na
haya yanachangiwa na tabia za baadhi ya watu wasio waungwana miongoni
mwa jamii," alisema Dkt. Bilal. Alisema Serikali itaendelea kusimamia na
kudhibiti matumizi mabaya ya kemikali kwa kutoa elimu kwa watumiaji na
wananchi kuhusu matumizi sahihi na madhara yatokanayo na matumizi mabaya
ya kemikali.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment