Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
ya mwaka wa fedha wa 2012/13 imefichua madudu ya ajabu, ambayo bila
shaka yatakuwa yameondoa matumaini ya wananchi ya kukua kwa uchumi na
kuwaondolea umaskini uliokithiri. Ripoti za CAG za miaka ya fedha
iliyopita zilikuwa pia zinafichua madudu ya kutisha, lakini baada ya
Serikali kuahidi kwamba ingeepuka kurudia madudu hayo na kuzifanyia kazi
changamoto nyingi zilizokuwa zikiibuliwa na ripoti mbalimbali za CAG,
wananchi wengi walipata matumaini.
Inasikitisha kwamba ripoti hiyo iliyotolewa
ufafanuzi na CAG mwenyewe, Ludovick Utouh juzi, imeonyesha dhahiri
kwamba Serikali haijawa na dhamira ya kweli ya kudhibiti matumizi mabaya
ya fedha za Serikali na kupambana na vitendo vya ufisadi na ubadhirifu
wa mali ya umma. Pamoja na kuwapo kwa Bunge na mifumo mingine kadhaa ya
kuhakikisha kwamba Serikali inakuwa na nidhamu katika kusimamia mapato
na kudhibiti matumizi yake, bado hakuna mabadiliko wala dalili za
uwajibikaji katika matumizi ya fedha za Serikali.
Ripoti ya CAG inaonyesha kwamba matumizi hayo
mabaya yanaendelea pamoja na hali mbaya ya uchumi inayolikabili taifa.
Kwa mwenendo huo, inaonekana hakuna uwezekano wa kupunguza Deni la Taifa
ambalo lilifikia Sh21.20 trilioni, ambalo ni ongezeko la Sh4.23
trilioni sawa na asilimia 25, ikilinganishwa na Sh16.98 trilioni katika
mwaka wa fedha wa 2011/12. Ndani ya Serikali umekuwamo utamaduni wa
ufujaji wa fedha tunaoweza kusema ni wa mashindano, ambao umechangia
kupanda kwa deni la ndani kutoka Sh4.55 trilioni mwaka 2011/2012 hadi
Sh5.78 mwaka wa 2012/13, likiwa ni ongezeko la Sh1.23 trilioni, sawa na
asilimia 27.
Mwenendo huo ni hatari kwa uchumi na maendeleo ya
taifa letu. Baya zaidi ni pale Serikali inapoendekeza mikopo kutoka
katika benki za biashara nje ya nchi. Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania
(BoT), inasema kwamba Serikali imekuwa ikikopa wastani wa Sh360 bilioni
kwa mwezi kutoka nje. Kutokana na hali hiyo, Shirika la Fedha Duniani
(IMF) na Benki ya Dunia (WB), vimeonya dhidi ya mwenendo huo kwamba
utahatarisha uchumi, ingawa Ripoti ya CAG inasema mikopo hiyo imesaidia
miradi mikubwa ya maendeleo kama uboreshaji wa miundombinu na kadhalika.
Sisi hatudhani kama mikopo hiyo ina madhara kwa
uchumi iwapo utakuwapo uwazi na itasimamiwa kwa uadilifu, kwa maana ya
kuhakikisha kwamba siyo tu unakuwapo usimamizi katika matumizi ya fedha
hizo, bali pia zinatumika kuendesha miradi iliyokusudiwa. Miradi mingi
ya maendeleo imekuwa ikikwama kutokana na fedha zake kuingizwa katika
michepuko isiyofaa, mbali na wizi na ubadhirifu wa baadhi ya wanasiasa,
watendaji wa Serikali na taasisi zake.
Ripoti ya CAG imebaini ufisadi mkubwa katika
maeneo mengi ya mapato na matumizi ya fedha za Serikali. Kwa mfano,
magari mapya 11 yenye thamani ya mamilioni ya shilingi yalinunuliwa
lakini yaliishia katika miliki za watu binafsi. Sh1.62 zililipwa kama
mishahara kwa watumishi hewa, huku misamaha ya kodi ikilipotezea taifa
Sh1.52 trilioni ambazo zingeweza kujenga shule za sekondari za kisasa
zaidi ya 300. Ripoti ya CAG haitoi matumaini. Serikali isipopambana na
ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma, maendeleo na ustawi wa jamii
nchini utabaki kuwa ndoto za mchana.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment