Home » » Waziri Mkuu awaonya viongozi Wanging’ombe

Waziri Mkuu awaonya viongozi Wanging’ombe


WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ameipa Wilaya mpya ya Wanging’ombe mkoani Njombe hadi mwisho wa mwezi huu kuhakikisha wanafunzi zaidi ya 800, waliofaulu kuingia sekondari lakini hawajafanya hivyo, wawe shuleni.
Alikuwa akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Ilemela katika siku ya kwanza ya ziara ya wiki mbili katika Mikoa ya Njombe na Ruvuma.

Ni dhambi kubwa kuwaacha wanafunzi hao wawe nje ya shule kwa kuwa wamefaulu na kwamba wenzao wengi wanaendelea na masomo na baadhi yao wanaweza kuwa viongozi wa kesho, alisema.

“Wasakeni hawa popote walipo na mhakikishe wanakuwa shuleni badala ya kuzurura mitaani. Nakuagiza DC (Mkuu wa Wilaya Esterina Kilasi) na RC (Mkuu wa Mkoa Assery Msangi) mlisimamie jambo hili na wanafunzi hao wawe shuleni ifikapo mwisho wa mwezi.

“Mtafanyaje, mtajua wenyewe, lakini wanafunzi hao hawawezi kuachwa tu, lazima wawe shuleni,” alisisitiza.

Asilimia 75 ya watahiniwa wote wa darasa la saba katika wilaya hiyo wamefaulu kuingia Ssekondari katika mtihani wa Taifa wa mwaka 2012, lakini kati ya waliofaulu 864 walikuwa hawajaripoti shuleni.

Kuna vyumba vya kutosha vya madarasa na ziada ya madawati katika wilaya hiyo yenye watu wapatao 160,000, ikiwa ni moja ya wilaya nne za mkoa mpya wa Njombe. Wilaya nyingine ni Njombe, Makete na Ludewa.

Waziri Mkuu pia aliagiza watendaji wakuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe wawe wanaishi na kufanya kazi ndani ya wilaya hiyo badala ya kuishi katika maeneo mengine.


CHANZO GAZETI LA MTANZANIA

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa