Home » » KERO YA MAJI SHULE YA MSINGI NDULAMO WILAYANI MAKETE YAMALIZWA

KERO YA MAJI SHULE YA MSINGI NDULAMO WILAYANI MAKETE YAMALIZWA

Na Edwin Moshi, Makete
 
Kero ya muda mrefu ya ukosefu wa maji katika shule ya msingi Ndulamo wilaya ya Makete mkoani Njombe hatimaye imetatuliwa baada ya idara ya maji wilayani hapo kuamua kutilia mkazo suala hilo
 
Akizungumza na mtandao huu ofisini kwake mwalimu mkuu wa shule hiyo Bw. Bosco Godigodi Malangalila (pichani) amesema maji yanapatikana kwa wingi shuleni hapo baada ya kuyakosa kwa kipindi kirefu hali iliyokuwa inaleta picha mbaya shuleni hapo.
 
Amesema tatizo hili limeondoka shuleni hapo baada ya idara ya maji kupeleka mabomba na kuyafunga kufidia yale ya awali yaliyokuwa yakivujisha maji ilihali yalikuwa mapya hali iliyosababisha kijiji cha Ndulamo kukosa maji ikiwemo na shule hiyo.Mwalimu Godigodi amesema awali walifanya maandamano hadi kwenye ofisi za serikali ya kijiji kushinikiza tatizo hilo la maji kuondolewa shuleni hapo na waliohusika na uzembe uliosababisha maji yasifike shuleni hapo wawajibishwe
 
“Hivi sasa ndugu mwandishi kuna uafadhali mkubwa kwani maji yapo, hata waalimu wanaoishi shuleni hapa wanauwezo wa kulima hata kabustani ka mbogamboga” alisema Mwalimu mkuu huyo.Mwanafunzi aliyejitambulisha kwa jina la Alexander Marko amesema kutokana na maji kutoka shuleni hapo yanawasaidia kunywa maji na kunawa mikono ukizingatia msimu huu ni wa kiangazi
 
Amesema hivi sasa ile kero ya kwenda kutafuta maji wakati wa masomo na wakati mwingine wanafunzi kuja na maji ya kunywa shuleni kwa sasa haipo kwa kuwa yapo maji ya kutosha.Naye mwanafunzi mwingine Timotheo Ibrahim amesema hivi sasa usafi wa vyoo ni mzuri tofauti na awali lakini pia hata mazingira ya shule yamekuwa masafi kwa kuwa maji hayo hutumia kupigia deki madarasani na vyooni
 
Katika hatua nyingine mwalimu Godogodi amesema ujenzi wa nyumba ya mwalimu uliokuwa ukamilike mwezi huu, hivi sasa unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba mwaka huu kwa kuwa ujenzi huo utaendelea kwa kasi baada ya maji kufika shuleni hapo
 
Amesema ujenzi huo ulisuasua kutokana na kukosekana kwa maji shuleni hapo lakini kwa kuwa kila kitu cha ujenzi hivi sasa kipo ujenzi huo utakamilika mwezi Septemba

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa