Home » » Halmashauri ya Mji Njombe yapongezwa kwa miradi

Halmashauri ya Mji Njombe yapongezwa kwa miradi

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Njombe wakifuatana na wataalamu kutoka Halmashauri ya Mji Njombe wakikagua ujenzi wa mradi wa kituo kipya cha mabasi, unaoendelea katika eneo la Mji Mwema jana. Wa pili kushoto ni Mhandisi Mshauri kutoka Masasi Construction akionesha ujenzi wa njia za kutokea mabasi. (Na Mpigapicha Maalumu).
KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Njombe, imepongeza jitihada zinazofanywa na Halmashauri ya Mji wa Njombe katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwenye ujenzi wa miradi mbalimbali.
Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi hiyo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Edward Mgaya alisema amefurahishwa na jinsi Halmashauri kupitia mapato ya ndani imekuwa ikitoa fedha kusaidia uendelezaji wa miradi hiyo.
“Mkurugenzi na Mwenyekiti napenda niwapongeze kwa jitihada nzuri mnazofanya. Miradi yenu ni mizuri na wakandarasi wenu wapo vizuri. Miradi ipo imara, thamani ya hela iliyotumika inaonekana na ninaamini mpaka kufikia mwaka 2020 Halmashauri itakuwa imepiga hatua kubwa sana kimaendeleo kwani miradi mingi itakuwa imekamilika na imeanza kutumika,” alisema Mgaya na kuongeza:
“Napenda pia niwapongeze wataalamu wa Halmashauri ya Mji Njombe kwa kazi nzuri ya usimamizi wa miradi hii. Kazi inaridhisha.” Aliongeza, “Nimefurahishwa zaidi pia na wananchi ambao wamekuwa hawaisubiri serikali kufanya kila kitu.
Tumeona kuna baadhi ya miradi ambayo imejengwa kwa nguvu za wananchi wenyewe na Halmashauri nayo inaongezea fedha ili kukamilisha miradi hiyo.” Alisema hilo ni jambo jema na angependa wananchi katika maeneo mengine ya Njombe, waige mfano huu, na inasikitisha pale unapopita na kuona miradi mingine imesimama kutokana na ukosefu wa fedha na wananchi wa eneo husika hawaoneshi ushirikiano wa aina yoyote ile na badala yake wanatupia lawama serikali na kusahau kuwa miradi hiyo inapokamilika inakuwa ni kwa manufaa yao zaidi.
Jumla ya miradi yenye thamani ya zaidi ya Sh 6,905,588,815 imekaguliwa, ikihusisha miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na vyoo katika shule za msingi na sekondari, ujenzi wa zahanati, ujenzi wa mradi wa maji, kituo cha kukusanyia maziwa, ujenzi wa kituo kipya cha mabasi, ujenzi wa vyumba vya maduka, ujenzi wa mabweni na ujenzi wa nyumba za walimu katika shule za sekondari.

Chanzo Gazeti la Habari Leo

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa