DOLA BILIONI 3 ZA KIMAREKANI KUTUMIKA KUTEKELEZA MRADI WA LIGANGA NA MCHUCHUMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Na Benedict Liwenga, MAELEZO
 
JUMLA ya dola Bilioni 3 za Kimarekani zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa  Mgodi wa Makaa ya  Mawe na Chuma wa Liganga na Mchuchuma.
 
Kauli hiyo imetolewa  na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage wakati akiongea na Waandishi wa habari mini Dodoma.
 
Amesema mradi huo unaojengwa kwa ubia kati ya Tanzania Kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Kampuni ya China ya Sichuan Hongda Group unatarajia kuanza mwaka huu.
 
Mhe. Mwijage amesema kuwa fedha za kuwalipa fidia wananchi wanaozunguka maeneo ya mradi huo ziko tayari ambapo zinatarajiwa kutumika zaidi ya bilioni 13 kwa ajili ya fidia na makazi.
 
Alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasadia kuzalisha umeme Megawati 600 ambapo 250 zitatumika katika Kiwanda cha Chuma na nyingine 350 zitapelekwa kwenye Gridi ya Taifa kwa ajili ya kuongeza nguvu katika nishati ya umeme.
 
‘’Pamoja na kuchimba chuma, Mradi wa Mchuchuma na Liganga utahusisha ujenzi wa Kinu cha Umeme chenye uwezo wa Megawati 600”, alisema Mhe. Mwijage.
 
Ameongeza kuwa, Tanzania kwa sasa itakuwa na umeme wa gesi, maji na umeme wa makaa ya mawe ambapo umeme wa makaa ya mawe utakuwa msaada mkubwa kwa nchi kwani hautegemei tabianchi kama ilivyo vyanzo vingine vya umeme.
 
Mhe. Mwijage amesema kuwa katika mradi huo, Tanzania itakuwa na hisa asilimia 20 na Mwekezaji kutoka China atakuwa na asilimia 80, lakini hisa za Tanzania zinaweza kuongezeka hadi kufikia 45.
 
Chini ya mradi huo, Mwekezaji huyo anatakiwa kutoa elimu kwa Vijana katika ngazi zote za teknolojia zitakazohusika kutengeneza mgodi huo.
 
‘’Tutafundisha vijana wetu kwa ngazi tofauti kwani kampuni hii ni ya ubia kati ya Tanzania na China, tuna mamlaka sawa, tuna Wakurugenzi wetu wa Tanzania ndani ya hiyo kampuni, kwahiyo tutashiriki na hatutakuwa watazamaji”, alisema Mhe. Mwijage.
 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayosimamia Viwanda, Biashara na Uwekezaji ambaye pia ni Mtaalam katika masuala ya madini, Mhe. Dkt. Dalaly Kafumu amesema kuwa, lengo la kuwajengea makazi wakazi wa maeneo ya mradi huo ni kuwawezesha wakazi hao kuwa na uhusiano mzuri na mgodi unaotarajiwa kujengwa.
 
‘’Serikali imeamua kuwajengea makazi wananchi ambao wanazunguka mradi Ili kuepusha wakazi hao kutumia pesa watakayolipwa kama fidia kwa matumizi mengine na kukosa makazi baadaye kuja kuilaumu Serikali kwamba imewadhulumu kwa kutowapa pesa za kutosha za kujenga nyumba”, alisema Dkt. Kafumu.
 

Halmashauri ya Mji Njombe yapongezwa kwa miradi

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Njombe wakifuatana na wataalamu kutoka Halmashauri ya Mji Njombe wakikagua ujenzi wa mradi wa kituo kipya cha mabasi, unaoendelea katika eneo la Mji Mwema jana. Wa pili kushoto ni Mhandisi Mshauri kutoka Masasi Construction akionesha ujenzi wa njia za kutokea mabasi. (Na Mpigapicha Maalumu).
KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Njombe, imepongeza jitihada zinazofanywa na Halmashauri ya Mji wa Njombe katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwenye ujenzi wa miradi mbalimbali.
Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi hiyo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Edward Mgaya alisema amefurahishwa na jinsi Halmashauri kupitia mapato ya ndani imekuwa ikitoa fedha kusaidia uendelezaji wa miradi hiyo.
“Mkurugenzi na Mwenyekiti napenda niwapongeze kwa jitihada nzuri mnazofanya. Miradi yenu ni mizuri na wakandarasi wenu wapo vizuri. Miradi ipo imara, thamani ya hela iliyotumika inaonekana na ninaamini mpaka kufikia mwaka 2020 Halmashauri itakuwa imepiga hatua kubwa sana kimaendeleo kwani miradi mingi itakuwa imekamilika na imeanza kutumika,” alisema Mgaya na kuongeza:
“Napenda pia niwapongeze wataalamu wa Halmashauri ya Mji Njombe kwa kazi nzuri ya usimamizi wa miradi hii. Kazi inaridhisha.” Aliongeza, “Nimefurahishwa zaidi pia na wananchi ambao wamekuwa hawaisubiri serikali kufanya kila kitu.
Tumeona kuna baadhi ya miradi ambayo imejengwa kwa nguvu za wananchi wenyewe na Halmashauri nayo inaongezea fedha ili kukamilisha miradi hiyo.” Alisema hilo ni jambo jema na angependa wananchi katika maeneo mengine ya Njombe, waige mfano huu, na inasikitisha pale unapopita na kuona miradi mingine imesimama kutokana na ukosefu wa fedha na wananchi wa eneo husika hawaoneshi ushirikiano wa aina yoyote ile na badala yake wanatupia lawama serikali na kusahau kuwa miradi hiyo inapokamilika inakuwa ni kwa manufaa yao zaidi.
Jumla ya miradi yenye thamani ya zaidi ya Sh 6,905,588,815 imekaguliwa, ikihusisha miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na vyoo katika shule za msingi na sekondari, ujenzi wa zahanati, ujenzi wa mradi wa maji, kituo cha kukusanyia maziwa, ujenzi wa kituo kipya cha mabasi, ujenzi wa vyumba vya maduka, ujenzi wa mabweni na ujenzi wa nyumba za walimu katika shule za sekondari.

Chanzo Gazeti la Habari Leo

Mtihani wa Kidato cha Sita unaendelea vizuri

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 



Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako

BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA) limesema Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita na ule wa Ualimu, umeanza vizuri katika maeneo yote nchini. Akizungumza jana ikiwa ni siku ya pili tangu kuanza kwa mtihani wa taifa, Ofisa Habari wa Necta, John Nchimbi alisema mtihani huo umeanza kwa wakati uliopangwa na umefanyika katika hali ya utulivu na na amani.
“Taarifa za kanda zote zinaonesha kuwa mtihani umeanza vizuri maeneo yote, kwa wakati na umefanyika katika mazingira ya utulivu kama taratibu za mtihani zinavyotaka,” alisema Nchimbi. Mtihani wa Kidato cha Sita ulianza Jumatatu na utafanyika hadi Mei 19, mwaka huu wakati ule wa Ualimu utafikia tamati Mei 13, mwaka huu.
Jumla ya watahiniwa 74,920 wanafanya mtihani wa kuhitimu Kidato cha Sita katika shule mbalimbali nchini huku watahiniwa 11,597 wakifanya mtahini wa ualimu. Kati ya watahiniwa hao waliosajiliwa, watahiniwa 65,610 ni watahiniwa wa shule huku watahiniwa wa kujitegemea wakiwa 9,310.
Kati ya watahiniwa wa shule 65, 610, wasichana ni 24,549 na wavulana ni 41,061 huku watahiniwa wa kujitegemea wasichana wakiwa ni 3,176 na wavulana ni 6,134. Kwa upande wa mtihani wa ualimu, watahiniwa 11,597 wanafanya mtihani wa Ualimu.
Kati ya hao watahiniwa 10,942 wanafanya mtihani wa Ualimu daraja A na watahiniwa 654 wanafanya mtihani wa Diploma ya sekondari na mmoja anafanya mtihani wa Ualimu wa Diploma ya Ufundi.
Chanzo Gazeti la Habari leo
 
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa