Home » » WANAFUNZI WA SEKONDARI YA WASICHANA MAKETE WATAKIWA KUWA MFANO BORA KIELIMU NA KITABIA‏

WANAFUNZI WA SEKONDARI YA WASICHANA MAKETE WATAKIWA KUWA MFANO BORA KIELIMU NA KITABIA‏


Wanafunzi wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Makete Mh Josephine Matiro
 Mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro akizungumza na wanafunzi wa Makete Girls Sekondari (hawapo Pichani)
Maktaba ya shule hiyo.
 Mkuu wa wilaya ya Makete Josephine Matiro akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi na walimu wa shule hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro (wa tatu kushoto) akiwa na walimu wa shule hiyo, wa kwanza kulia ni Afisa Taaluma sekondari wilaya hiyo.
===
Wanafunzi wa kike wanaosoma katika shule pekee ya wasichana iitwayo Makete girls secondary School iliyopo wilayani Makete mkoani Njombe wametakiwa kuzingatia masomo na kuwa mfano bora wa kuigwa toka shuleni hadi sehemu wanazotoka

Aidha kwa kufanya hivyo kutapelekea wafaulu vizuri masomo yao na kuhakikisha lengo la serikali kuanzisha shule hiyo linafikiwa hasa kuinua kiwango cha ufaulu kwa wasichana katika wilaya hiyo

Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro wakati alipofanya ziara katika shule hiyo hii leo kwa lengo la kujionea maendeleo na changamoto mbalimbali zinazoikabili shule hiyo ili zitafutiwe ufumbuzi ikizingatiwa shule hiyo ni mpya, ambapo akiwa shuleni hapo pamoja na mambo mengine amekula chakula cha mchana na wanafunzi hao

Akizungumza na wanafunzi hao Mh. Matiro amewataka wanafunzi hao kuepuka wanaume walaghai ambao hutumia njia mbalimbali kuwarubuni hasa wanaporudi majumbani mwao wakati wa likizo na kusema kuwa hategemei tatizo la ujauzito kuwakumba wanafunzi hao endapo watakuwa msimamo wa kuzingatia masomo tu

"Tunategemea shule hii iwe ya mfano na ninyi ndio wenye uwezo wa kuifanya hivyo, hii shule ni mpya na ninyi ndio wanafunzi wa kwanza kusoma hapa, tunategemea mfaulu vizuri, sisi tunajitahidi kwa kila namna kuboresha shule hii, ninyi kazi yenu ni kusoma tu, acheni mzaha someni kwa bidii, kila jambo na wakati wake, wakati mlio nao sasa ni wa kusoma tu na si vingine" amesema Matiro
 
Kwa upande wa wanafunzi hao akiwemo Prisila Haule, Jema Kyando na Florida Ngogo wametaja changamoto zinazowakabili ikiwemo ukosefu wa vifaa vya michezo, ukosefu wa waalimu wa sayansi, shule kukosa gari, pamoja na shule kukosa matroni.

Mkuu wa shule hiyo Bi. Sayuni Sanga amesema ni kweli shule ina wajibu wa kumuajiri matroni lakini kwa sasa haiwezi kufanya hivyo kwa kuwa shule hiyo ni changa na haina uwezo wa kumlipa ila kwa sasa mwalimu mmoja amejitolea kuwa matroni hadi hapo atakapopatikana matroni halisi

Kuhusu michezo mwalimu wa michezo shuleni hapo Bw. Japhet Mwile amesema wanashindwa kuainisha maeneo ya viwanja vya michezo kutokana na maeneo hayo kuwa na mazao ambayo hayajavunwa na kwa sasa wanasubiri yakishavunwa waanze kuandaa viwanja kwa kuwa walikubaliana na wazazi kuwa wakishavuna mazao yao hawatalima tena mashamba hayo kwa kuwa kwa sasa ni mali ya shule

Shule hiyo imeanza rasmi Aprili 22 mwaka huu na ina wanafunzi 36 na walimu wanne, huku changamoto kubwa inayoikabili shule hiyo ni ukosefu wa mabweni ambapo serikali imeahidi kupambana kuitatua changamoto hiyo kwani kwa sasa wanafunzi hao wanalala madarasani.

Habari/picha na Edwin Moshi.Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa