Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KITUO
maalumu cha uendelezaji kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT)
kimetoa wito kwa wakulima wadogo kuungana kwa kuunda vikundi vidogo ili
kuirahisishia Serikali kuwafikishia huduma muhimu za pembejeo na mikopo
katika kuinua sekta hiyo hapa nchini.
Wito huo ulitolewa jana
na Ofisa Mtendaji Mkuu wa kituo hicho, Geoffrey Kirenga, wakati
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mada alizotarajia
kuziwasilisha kwenye mkutano wa wadau wa Umoja wa Watendaji Wakuu wa
Kampuni (CEOrt).
"Mkiungana pamoja
inakuwa rahisi kuwapatia mafunzo na kuwawezesha kupata mikopo, kwa
sababu jukumu letu ni kuwatafutia masoko na kuwawezesha wakulima hawa
kuongeza uzalishaji," alisema kirenga.
Aidha alitoa wito kwa
wawekezaji na kampuni binafsi kuwekeza kwenye sekta ya kilimo katika
ukanda huo kwa kuwa ni ukanda ambao una hali ya hewa nzuri inayostawisha
vyema mazao mbalimbali yanayotakikana.
"Kwa mfano maeneo ya
Mkoa wa Iringa wanalima pia viazi, awali walikuwa wakivuna kuanzia tani 5
hadi 7 kwa mwaka lakini baada ya kutafuta wawekezaji na kuwasaidia
wakulima wadogo na wa kati, sasa wanavuna tani 25 hadi 30 za viazi.
Alisema ukanda huu
unazalisha mazao ya chakula na biashara kwa asilimia 65 nchini, sasa
iwapo zikitumiwa ipasavyo fursa zilizopo katika ukanda huu hawawezi
kuhangaika hata kidogo.
"Kwa sababu tulijaribu
katika shamba la mpunga hapo Kilombero kwa kutafuta mwekezaji ambaye
aliwasaidia wakulima, na sasa matunda yanaonekana kwani wanavuna tani
5.6 za mpunga kutoka tani moja za awali walizokuwa wakivuna," alisema
Kirenga.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa CEOrt, Ali Mufuruki alisema jukwaa hilo litaendelea
kuwakutanisha wataalamu mbalimbali na maofisa watendaji wakuu wa
makampuni ambao ni wanachama ili kuisaidia serikali kujikwamua kiuchumi.
Alisema ndani ya jukwaa
hilo la CEOrt kuna kampuni zaidi ya 100 ambazo kwa hakika zikitumiwa
vyema zinaweza kuinufaisha jamii inayowazunguka
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment