Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kama tulivyoona katika sehemu ya kwanza, kuna kasoro kwenye
mchakato wa Katiba Mpya unaondelea nchini lakini Tume ya jaji Warioba,
hususan Rasimu, ina uhalali mkubwa zaidi wa kisheria na hata wa kisiasa.
Kuhitimisha, ni hili la ushirikiano uliotolewa kwa
Tume ya Warioba na taasisi za kikatiba na kiserikali. Taarifa rasmi za
tume zinathibitisha kuwa kati ya taasisi tajwa zilizotoa maoni yao kwa
Tume na kwa maandishi, ni Bunge la Jamhuri, Baraza la Wawakilishi, Ofisi
ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu na mengineyo mengi.
Kifungu cha 18 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
kilitoa fursa kwa taasisi tajwa kujigeuza kuwa ‘Mabaraza ya Katiba’ na
“kutoa maoni juu ya Rasimu ya Katiba”. Ni muhimu hili likatiliwa maanani
na maoni haya yakajulikana, tukizingatia dai la mara kwa mara kuwa Tume
haikukusanya maoni ya Watanzania ‘ya kutosha’.
Tulijikwaa Wapi?
Wahenga walinena: Angalia ulipojikwaa, siyo
ulipoanguka. Ile siku baadhi ya wajumbe, hususan wale waliomo katika
kundi linalojulikana zaidi kama Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
waliposusia kikao na kutoka nje ya Bunge Maalumu, mchakato ulikuwa
umeaungukia pua, hata kama siyo ‘kifo cha mende’.
Lakini, tulijikwaa wapi? Ni nini, na vipi
tukajikuta katika mkwamo huu? Tuelewe kuwa Bunge Maalumu ndio chombo
kitakachopitisha ile Rasimu ya Katiba ambayo hatimaye itapigiwa kura ya
maoni. Hivyo ndivyo inavyosema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba katika
‘Sehemu ya Sita’.
Kwa hiyo, kisheria, hata kisiasa, Bunge Maalum ni
sehemu nyeti na muhimu katika mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya,
Katiba ambayo itarekebisha ule upungufu, uliomo katika ‘Sheria Mama’
iliyopo. Na kwa kufanya hivyo, kuhitimisha mambo mawili: Kuandika Katiba
Mpya na kusimika misingi mipya ya utawala (bora) wa Taifa letu.
Kwa mtazamo wangu, na kwa ujumla wake, tulianza
vibaya! Na hili linajidhihirisha tukikubali tathmini ifuatayo. Uzoefu
unaonyesha kuwa uongozi wa nchi ulikuwa na dhamira thabiti kukabili
upungufu sugu ya ‘Sheria Mama’ uliopo. Kwamba, badala ya kuendelea na
utaratibu wa ‘kupiga viraka’ Katiba iliyopo ya 1977, ni bora tukachanja
mbuga mpya, kwa mantiki ya mchakato mpya, na mpana zaidi, wa kupata
mustakabali mpya wa Katiba. Na ndiyo maana kila mtu aliyeisikia ile
kauli ya Rais Kikwete siku ile ya Desemba 2010, alijawa na faraja na
matumaini makubwa. Sikumbuki kusikia hata sauti moja ya kupinga wala
kuhoji kauli lile.
Lakini uzoefu umekuja kutonyesha kuwa ‘dhamira’
ilikuwa kionjo muhimu, lakini siyo pekee, katika kufanikisha zoezi la
kupatikana Katiba Mpya na iliyo bora zaidi, kwani hata safari ya kwenda
jehanamu, inapitia juu ya njia ya ‘dhamira njema’!
Tulianza vibaya pia, kwa kuchomeka kwenye Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba, Kifungu 36 (5). Kinanena: “Endapo wingi wa kura
ya maoni utakuwa ni ‘Hapana’, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ya mwaka 1977, itaendelea kutumika”
Je, huu si uchuro (nuksi)? Inakuwaje tunakiri kuwa
‘Sheria Mama’ iliyopo ina upungufu wa kimsingi, na papo hapo kuweka
uwezekano wa kisheria wa ‘kumeza matapishi yetu’? Taifa limeingia
gharama kubwa ajabu (inasemekana, ni zaidi ya Sh100 billioni), lakini
hatima ya yote, ni kujikuta pale pale tulipokuwa (‘back to square one’),
kabla ya mchakato kuanza!
Ukiachilia mbali uchuro huo, ushahidi zaidi wa
jinsi tulivyoaanza vibaya, uko pia katika mambo mawili makuu yafuatayo.
Mosi, tulikwepa kujipa nafasi ya kuijadili kwa pamoja na kwa kina,
‘Sheria Mama’ iliyopo. Kwa kujinyima fursa hiyo, tulijinyima nafasi ya
kuwa na maridhiano kuhusu ni kipi kizuri kwenye Katiba ya mwaka 1977 (na
kwa hiyo kinahitaji kulindwa, na kuendelezwa), na ni masuala gani
yamegubikwa na utata (na hivyo, yajadiliwe kinagaubaga, mwuafaka
upatikane na tusonge mbele). Hili pengine ndio lingetusukuma kujiuliza,
na kupata mwafaka wa swali nyeti: Muungano umekuja na faida gani kwetu
sote? Tuendelee kuuenzi Muungano kwa mikakati ipi?
‘Kosa siyo kufanya kosa. Kosa ni kurudia kosa’. Na wala kuanguka sio dhambi, ili mradi utafute pale ulipojikwaa. Tukifanya hivyo, tutaweza kujikwamua. ‘Kosa’ letu kubwa kwa mantiki hii, ni ‘kuanza vibaya’. Mosi, tumeingia kwenye mchakato wa kutafuta Katiba Mpya, pasi kuichambua ‘Sheria Mama’ iliyopo, ili kubaini na kukubaliana juu ya nini hasa kiwe ‘moyo’ wa hiyo Katiba mpya tuitakayo. Pili, mchakato umesimikwa kwenye Sheria (Sura ya 83) yenye utata wa kisheria na wa kisiasa. Tatu, badala ya ‘Bunge Maalum la Katiba’ tumeunda ‘Bunge Maalum la Wanasiasa’. Nne, dhamira njema ya kupata Katiba mpya, imetiwa nuksi na Kifungu 35 (6) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Chanzo;Mwananchi
‘Kosa siyo kufanya kosa. Kosa ni kurudia kosa’. Na wala kuanguka sio dhambi, ili mradi utafute pale ulipojikwaa. Tukifanya hivyo, tutaweza kujikwamua. ‘Kosa’ letu kubwa kwa mantiki hii, ni ‘kuanza vibaya’. Mosi, tumeingia kwenye mchakato wa kutafuta Katiba Mpya, pasi kuichambua ‘Sheria Mama’ iliyopo, ili kubaini na kukubaliana juu ya nini hasa kiwe ‘moyo’ wa hiyo Katiba mpya tuitakayo. Pili, mchakato umesimikwa kwenye Sheria (Sura ya 83) yenye utata wa kisheria na wa kisiasa. Tatu, badala ya ‘Bunge Maalum la Katiba’ tumeunda ‘Bunge Maalum la Wanasiasa’. Nne, dhamira njema ya kupata Katiba mpya, imetiwa nuksi na Kifungu 35 (6) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment