Home » » UJENZI WA VYOO SHULE YA MSINGI UWALE MAKETE BALAA TUPU

UJENZI WA VYOO SHULE YA MSINGI UWALE MAKETE BALAA TUPU

 Mojawapo ya chemba ya vyoo hivyo.
 Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Makete Francis Chaula akizungumzia hali hiyo.
 Mwenyekiti wa shule Hussen Mwalyoyo akizungumzia hali ya ujenzi huo.
 Choo hicho kikiwa hakina sakafu kwenye korido.
======
Na Edwin Moshi wa EDDY BLOG
Inawezekana ikawa ni mara ya kwanza kwa wilaya ya Makete kushuhudia kituko cha mwaka ambapo vyoo vya shule ya msingi Iwale wilayani hapo kujengwa bila ramani na BOQ, hali iliyopelekea mdari huo kutekelezwa chini ya kiwango

Wakizungumza na mtandao huu kwa masikitiko makubwa wananchi wa kijiji hicho wamesema mradi huo ulianzwa kutekelezwa tangu mwaka 2009 ambapo hadi leo hii mradi huo haujakamilika kiasi cha kuanza kutumika

Kutokana na maagizo yaliyotolewa na Bwana afya wa wilaya Bw Boniphace Sanga kuwa vyoo hivyo vianze kutumika kuanzia leo Septemba 26, hali hiyo imepelekea kamati ya ujenzi pamoja na mwenyekiti wa shule kugoma kuupokea mradi huo kwa madai kuwa umetekelezwa chini ya kiwango na hawako tayari kuruhusu uanze kufanya kazi licha ya maagizo ya maafisa wa wilaya ya kutaka uanze kutumika

Hali hiyo imewalazimu mwenyekiti wa CCM wilaya ya Makete Francis Chaula na viongozi wengine wa chama chake, pamoja na kaimu afisa elimu msingi Bw Fredrick Mkadange kufika shuleni hapo kujionea hali halisi ya vyoo hivyo pamoja na sababu za mradi huo kukataa kupokelewa

Akizungumza kwa masikitiko makubwa mwenyekiti wa shule hiyo Bw. Hussen Mwalyoyo amesema sababu za mradi huo kutekelezwa chini ya kiwango ni pamoja na kukosekana kwa ramani pamoja na mchanganuo wa mradi huo (BOQ) hivyo kudai kuwa walishindwa kuhoji wakati wa ujenzi huo kwa kuwa hawafahamu namna vyoo hivyo vilitakiwa viwe

'kila tukidai BOQ tunaambiwa mara ipo kijijini, mara wilayani yaani ni longolongo tu na kazi inaendelea hivyo hatukuweza kuhoji chochote kwa kuwa hatuna hiyo BOQ wala ramani ya vyoo hivi" alisema Mwalyoyo

Afisa afya wa tarafa hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Chengula ambaye alikuwa mshauri wa ujenzi huo amesema hakukabidhiwa vifaa wala hakuna aliposaini yeye kupokea vifaa vya ujenzi huo badala yake aliambiwa awe mshauri wa ujenzi huo ambapo alikiri kufika eneo la ujenzi na kuwaelekeza mafundi hao.Mtaalamu huyo alikwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa hata mkandarasi aaliyekuwa akijenga vyoo hivyo yeye hamfahamu

Hali hiyo iliwalazimu wajumbe wote kufika kujionea vyoo hivyo, ambapo walishuhudia mapungufu mengi ikiwemo milango kutofunga, bati kuwa za geji 30 badala ya 20, vyoo havina madirisha, sehemu ya kujisaidia haja ndogo kwa wavulana kukosa sakafu laini, korido kutowekwa sakafu pamoja na chemba ndogondogo za kupitishia uchafu kutotengenezwa kwa kiwango

Kufuatia hali hiyo mwenyekiti wa CCM Francis Chaula alitamka kutoafiki vyoo hivyo vianze kutumika kama vilivyo na kusema vitaanza kutumika pale tu vitakapofanyiwa marekebisho waliyoyagundua ili kutosababisha madhara zaidi, jambo lililoungwa mkono na wajumbe wote wa kikao hicho ambapo pia wameagiza mchanganuo wa vifaa vyote vilivyoletwa kwa ajili ya ujenzi huo itolewe pamoja na BOQ

Mwenyekiti aliahidi kufika ofisini kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Makete kwa ajili ya kupewa orodha hiyo na taarifa ataitoa kwa wananchi hao

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa