KITUO CHA WATOTO YATIMA NA VIKONGWE CHAZINDULIWA MAGO WILAYANI MAKETE‏

 kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa Juma Ali Simai akizindua kituo cha Eden Valley Foster Care kilichopo kijiji cha Mago wilayani Makete wakati mwenge ulipokuwa katika mbio zake wilayani humo hapo jana.ujenzi wa kituo hicho umegharimu zaidi ya milioni 714.
 
 Msimamizi wa kituo cha eden Valley Foster Care Jenet Fournier(kulia) akifurahia heshima aliyopewa na kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa Juma Ali Simai(hayupo pichani) ya kushika mwenge huo na kupiga picha ya kumbukumbu
 Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa Juma Ali Simai(wa pili kushoto) akiangalia darasa la kutoa elimu ya ufundi cherehani katika kituo hicho
Mkuu wa wilaya ya Makete Josephine Matiro akizungumza kituoni hapo kabla ya kumkaribisha kiongozi wa mbio za mwenge kuzungumza na wananchi waliofurika kumsikiliza kituoni hapo

(Picha zote na Edwin Moshi, globu ya jamii Makete)

UJENZI WA VYOO SHULE YA MSINGI UWALE MAKETE BALAA TUPU

 Mojawapo ya chemba ya vyoo hivyo.
 Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Makete Francis Chaula akizungumzia hali hiyo.
 Mwenyekiti wa shule Hussen Mwalyoyo akizungumzia hali ya ujenzi huo.
 Choo hicho kikiwa hakina sakafu kwenye korido.
======
Na Edwin Moshi wa EDDY BLOG
Inawezekana ikawa ni mara ya kwanza kwa wilaya ya Makete kushuhudia kituko cha mwaka ambapo vyoo vya shule ya msingi Iwale wilayani hapo kujengwa bila ramani na BOQ, hali iliyopelekea mdari huo kutekelezwa chini ya kiwango

Wakizungumza na mtandao huu kwa masikitiko makubwa wananchi wa kijiji hicho wamesema mradi huo ulianzwa kutekelezwa tangu mwaka 2009 ambapo hadi leo hii mradi huo haujakamilika kiasi cha kuanza kutumika

Kutokana na maagizo yaliyotolewa na Bwana afya wa wilaya Bw Boniphace Sanga kuwa vyoo hivyo vianze kutumika kuanzia leo Septemba 26, hali hiyo imepelekea kamati ya ujenzi pamoja na mwenyekiti wa shule kugoma kuupokea mradi huo kwa madai kuwa umetekelezwa chini ya kiwango na hawako tayari kuruhusu uanze kufanya kazi licha ya maagizo ya maafisa wa wilaya ya kutaka uanze kutumika

Hali hiyo imewalazimu mwenyekiti wa CCM wilaya ya Makete Francis Chaula na viongozi wengine wa chama chake, pamoja na kaimu afisa elimu msingi Bw Fredrick Mkadange kufika shuleni hapo kujionea hali halisi ya vyoo hivyo pamoja na sababu za mradi huo kukataa kupokelewa

Akizungumza kwa masikitiko makubwa mwenyekiti wa shule hiyo Bw. Hussen Mwalyoyo amesema sababu za mradi huo kutekelezwa chini ya kiwango ni pamoja na kukosekana kwa ramani pamoja na mchanganuo wa mradi huo (BOQ) hivyo kudai kuwa walishindwa kuhoji wakati wa ujenzi huo kwa kuwa hawafahamu namna vyoo hivyo vilitakiwa viwe

'kila tukidai BOQ tunaambiwa mara ipo kijijini, mara wilayani yaani ni longolongo tu na kazi inaendelea hivyo hatukuweza kuhoji chochote kwa kuwa hatuna hiyo BOQ wala ramani ya vyoo hivi" alisema Mwalyoyo

Afisa afya wa tarafa hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Chengula ambaye alikuwa mshauri wa ujenzi huo amesema hakukabidhiwa vifaa wala hakuna aliposaini yeye kupokea vifaa vya ujenzi huo badala yake aliambiwa awe mshauri wa ujenzi huo ambapo alikiri kufika eneo la ujenzi na kuwaelekeza mafundi hao.Mtaalamu huyo alikwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa hata mkandarasi aaliyekuwa akijenga vyoo hivyo yeye hamfahamu

Hali hiyo iliwalazimu wajumbe wote kufika kujionea vyoo hivyo, ambapo walishuhudia mapungufu mengi ikiwemo milango kutofunga, bati kuwa za geji 30 badala ya 20, vyoo havina madirisha, sehemu ya kujisaidia haja ndogo kwa wavulana kukosa sakafu laini, korido kutowekwa sakafu pamoja na chemba ndogondogo za kupitishia uchafu kutotengenezwa kwa kiwango

Kufuatia hali hiyo mwenyekiti wa CCM Francis Chaula alitamka kutoafiki vyoo hivyo vianze kutumika kama vilivyo na kusema vitaanza kutumika pale tu vitakapofanyiwa marekebisho waliyoyagundua ili kutosababisha madhara zaidi, jambo lililoungwa mkono na wajumbe wote wa kikao hicho ambapo pia wameagiza mchanganuo wa vifaa vyote vilivyoletwa kwa ajili ya ujenzi huo itolewe pamoja na BOQ

Mwenyekiti aliahidi kufika ofisini kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Makete kwa ajili ya kupewa orodha hiyo na taarifa ataitoa kwa wananchi hao

MSITU WA TEKETEA KWA MOTO MAKETE





Picha zikionesha moto ulivyoacha madhara makubwa kwa wenye misitu hii baada ya kuteketeza miti na mimea mingine iliyokuwa katika eneo hilo. Haijafahamika mara moja nini chanzo cha moto huo(PICHA ZOTE NA EDWIN MOSHI)

WANAOJISAIDIA OVYO MAKETE WAICHEFUA SERIKALI


Na Edwin Moshi, Makete

Serikali wilayani Makete mkoani Njombe imewataka wananchi kutoa ushirikiano wa pamoja kuwakamata ama kutoa taarifa kwa ngazi husika pindi wanapowaona watu wakijisaidia ovyo maeneo yasiyo rasmi.

Hayo yamesemwa na afisa afya wilaya ya Makete Bw Boniphace Sanga wakati akizungumza na mtandao huu na kuongeza kuwa kumekuwa na ongezako la magonjwa hasa ya kuhara ambayo yanatokana na watu wanaojisaidia ovyo na kuchafua mazingira.

Bw sanga amesema jukumu la usafi ni la kila mmoja na si la bwana ama bibi afya pekee na kwa kuwa wananchi ndio wanaoshinda maeneo mbalimbali wanawaona wale wanaojisaidia hovyo na kuomba watoe taarifa kwenye ofisi yake ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Amesema inashangaza kuona hadi sasa wapo watu ambao hawana vyoo na wanaongoza kwa kuchafua mazingira kutokana na kujisaidia ovyo, na kutoa wito kuwa msimu huu ni wa kiangazi hivyo wanatakiwa kujenga vyoo kabla mvua haijanyesha.

"Kwa kweli natoa wito nyumba bila choo haijakamilika, acheni kun***a(akimaaisha kujisaidia) maeneo ambayo si kwa ajili hiyo, unakuta mtu kavaa vizuri lakini ni namba moja kujisaidia maporini, huu si ustaarabu na watu wa namna hii ndio wanaoleta magonjwa kwenye wilaya yetu.

Katika hatua nyingine Bw. sanga amewaomba wananchi kuendelea kujijengea utaratibu wa kutupa taka maeneo yanayoruhusiwa( kwenye vizimba vya taka) na kuwaasa kuacha tabia ya kutupa chupa za soda na maji mitaani kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa watakaokamatwa.

SHULE YA MSINGI NKENJA MAKETE: INA HALI TETE!


 Majengo ya shule ya msingi Nkenja, kulia na kushoto ni vyumba vya madarasa, katikati ni ofisi ya mwalimu mkuu.
Uongozi wa CCM wilaya ya makete ukishangaa kuona jinsi wanafunzi wanavyopata tabu kusomea kwenye pagale.
Madarasa ambayo hayajakamilika lakini yanatumiaka kwa ajili ya darasa la kwanza na la pili.
Turubai likining'inia kwenye chumba ambacho wanasomea wanafuzni wa darasa la kwanza na la pili ambalo hulitumia kama bati kuzuia jua.



Mazingira magumu hasa kwa elimu ya msingi nchini bado yanazidi kuonekana baada ya shule ya msingi Nkenja iliyopo kata ya Kitulo wilayani Makete mkoani Njombe kuonekana ina vyumba viwili tu vya madarasa ambavyo vina hadhi ya kutumiwa kama madarasa

Hali hiyo si imeacha hoi mtandao huu tu bali pia viongozi mbalimbali waliofanya ziara ya kukagua shule hiyo ambayo ilijengwa kwa makusudi ya kuwapunguzia wanafunzi mwendo mrefu wa kilomita 14 wanaotembea kwenda kusoma shule ya msingi Ujuni iliyopo kijiji cha jirani cha Ujuni

Mbali na shule hiyo kuwa na vyumba viwili vya madarasa, chuma kimoja wanasomea wanafunzi wa darasa la tatu na la nne kwa kuchanganywa pamoja, na chumba kimoja wanatumia darasa la tano tu peke yao

Hayo yamebainika baada ya ziara ya mwenyekiti wa CCM wilaya ya Makete Francis Chaula kufanya ziara katika shule hiyo kukagua hali ya ujenzi na maendeleo kwa ujumla katika shule hiyo ikiwa ni muendelezo wa ziara yake katika kata mbalimbali wilayani hapo

Viongozi hao wa CCM wamezidi kushuhudia maajabu katika shule hiyo kwa kujionea chumba ambacho wanasomea wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili kikiwa hakina paa, bati wala sakafu ambapo wakati mwingine waalimu hukifunika kwa turubai ili kuwakinga na jua na wakati wa mvua havitumiki

"kama mnavyojionea ndugu viongozi wa CCM hali ni ngumu kwa kweli, tunaupungufu wa vyumba vitano vya madarasa, watoto wa darasa la kwana na la pili wanasomea kwenye chumba hiki ambacho hakina bati muda wote, wakati wa mvua hakitumiki kabisa, na wote tunawachanganya kwenye chumba hiki kimoja" alisema mwalimu mkuu Hester Mahenge

Viongozi hao ambao walikagua vyumba vyote vya shule hiyo pia waligundua shule hiyo ina upungufu wa madawati 50

Akizungumza shuleni hapo katibu wa CCM wilaya ya Makete Miraji Mtaturu amewapongeza wananchi wa Nkenja kwa kujitoa kwa gharama zao hadi hapo madarasa mawili yanayojengwa yalipofikia, na kuwaomba kushirikiana na kutilia mkazo suala hilo ili ujenzi huo ukamilike ndani ya mwaka huu

Amesema pamoja na wananchi hao kukabiliwa na michango mingi lakini watoe kipaumbele kwa ujenzi huo ili wanafunzi hao wasome kwa raha ukizingatia wanafunzi wanaosomea pagalani ni wa darasa la kwanza na pili ambao ndio wachanga wanaohitaji msaada kwa ukaribu zaidi

Naye mwenyekiti wa CCM wilayani hapo Francis Chaula amewataka kuandika bajeti ya vitu vinavyohitajika na gharama zake ili kukamilisha miradi hiyo na waipeleke kwa mkurugenzi mtendaji wa wilaya na nakala kwa chama chake ili kutilia mkazo zaidi namna ya kuboresha mazingira ya shule hiyo

Diwani wa kata ya Kitulo ilipo shule hiyo Mbosa Tweve amesema serikali kupitia halmashauri ya wilaya kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2013/2014 imetoa sh. milioni 8 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo na muda wowote kuanzia sasa zitapelekwa shuleni hapo na kuahidi kushirikiana kukamilisha ujenzi huo

baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wamelalamikia michango ya ujenzi huo kuchangwa na kitongoji kimoja tu ilihali kijiji kina vitongoji vinne na kusema hali hiyo inachangia mradi huo kusuasua, huku hoja hiyo ikijibiwa na mwenyekiti wa kijiji hicho Zablon Chengula kuwa amesawaita wenyeviti wa vitongoji vyote kuzungumzia suala hilo na wapo wananchi ambao wameshapelekwa kwa mtendaji wa kata kushughulikiwa kutokana na kugoma kushiriki zoezi hilo

Shule hiyo ina madarasa matano (I-V) ina jumla ya wanafunzi 51 wanaofundishwa na waalimu watatu tu
 
Na Edwin Moshi, Makete

Katiba mpya: Wakulima wadai kupuuzwa maoni yako

Njombe

RASIMU ya katiba mpya imeingia doa baada ya wakulima kudai kuwa tume ya katiba ya Jaji wa Joseph Walioba imeyapuuza maoni yao.

Hoja hiyo imeibuliwa  katika mkutano  mkuu wa mwaka  wa muungano wa  vikundi vya wakulima  wadogo wadogo  nchini  (MVIWATA)  ambao umefanyika katika  mkoa wa Njombe.

Mkutano huo umehusisha   wanachama  na viongozi wa bodi Taifa wa MVIWATA kutoka  Kanda  sita  zinazojumisha mikoa yote ya Tanzania  bara , ambao ulilenga kuzungumzia maendeleo ya Mtandao kwa ujumla.

Mwenyekiti MVIWATA  Habibu Simbamkuti amesema, kuna mambo ambayo ni ya msingi yamepuuzwa katika Rasimu ya katiba mpya amabayo walianisha na kuwayawasilisha katika Tume.

Upande wao wakulima   wamesema,licha ya kuwepo vikwazo lukuki pia ushirikishwaji ni kitendawili kisichoteguka, kile kilichodaiwa kuwa mikataba ya uwekezaji katika sekta ya ardhi haihusishi maoni ya mkulima moja kwa moja na kusababisha migogoro kati yao.


Mjadala wa rasimu ya katiba mpya umehitimishwa mwishoni mwa wiki hii, ambapo maoni na mapendekezo ya kitaasisi yanawasilishwa kwenye tume ya Jaji  mstaafu  Joseph  Walioba  kabla ya kupeleka kwenye Bunge la katiba Novemba mwaka huu.
mwisho

ZIARA YA VIONGOZI WA CCM WILAYA YA MAKETE YAZIDI KUIBUA MENGI


Katibu wa CCM wilaya ya Makete Miraji Mtaturu (kulia) akizungumza katika ziara ya kukagua maendeleo ya shule ya msingi Nkenja wilayani Makete, kushoto kwake ni mwenyekiti wa chama hicho wilaya ya Makete Francis Chaula

Viongozi wa CCm wilaya ya Makete wakikagua chumba cha darasa wanachosomea wanafunzi wa darasa la tatu na la nne kwa pamoja
 Katibu wa CCM wilaya ya makete Miraji Mtaturu, mwenyekiti Francis Chaula na diwani wa kata ya Kitulo Mbosa Tweve wakisikiliza maelezo kutoka kwa mkuu wa shule ya msingi Nkenja Hester Mahenge ofisini kwake
 Viongozi wa CCM wakikagua ujenzi wa madarasa unaodaiwa kusuasua, mwenyekiti wa CCM wilaya ya makete (katikati) akizungumzia ujenzi huo
 darasa wanalotumia wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili kusomea
 Turubai linalotumika kama bati kwenye jengo hilo
 Vyumba viwili vya madarasa ambavyo vinafaa kwa matumizi shuleni hapo.
(Picha zote na Edwin Moshi)
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa