Home » » KIPINDUPINDU CHAINGIA PAWAGA, 20 WALAZWA.

KIPINDUPINDU CHAINGIA PAWAGA, 20 WALAZWA.

WAKAZI wa Kijiji cha Mbolimboli Kata ya Pawaga wilayani Iringa, wamekumbwa na ugonjwa wa kipindupindu.
Hadi jana watu 20 waliripotiwa kuwekwa karantini, wakiugua ugonjwa huo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Robert Salim alisema ugonjwa huo umelipuka baada ya eneo hilo kukumbwa na mafuriko.
“Mafuriko hayo yamesababisha uchafu wa vyoo vilivyobomoka na mwingine kusambaa hadi katika visima vya maji yanayotumiwa na wakazi wa eneo hilo,” alisema Dk Salim.

Aliongeza kuwa wagonjwa hao 20, wamepokewa na kuweka katika kambi maalumu kijijini hapo wakiwa wanatapika na kuharisha mfululizo.
Alisema wengi wa waliothiriwa na ugonjwa huo ni wakazi wa Wilaya ya Kilolo, waliokwenda katika kijiji hicho kufanya kazi ya vibarua katika mashamba ya mpunga.

Alisema Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewapatia dawa na vifaa tiba kunusuru maisha ya watu hao. Dk Salim alionya wakazi wa Pawaga wasipodhibiti ugonjwa huo, utasambaa katika maeneo mengi ya mkoa wa Iringa.
“Halmashauri zote zimekwishajulishwa kuchukua tahadhari na kuelimisha jamii kuzingatia usafi, matumizi ya vyoo bora na kutokula ovyo ovyo ili kujiepusha na maambukizi ya ugonjwa huo,” alisema.

Alisema halmashauri hizo, zinatakiwa kufunga sehemu za biashara za vyakala zinazoendeshwa katika mazingira ya uchafu na wahudumu ambao hawajapima afya zao.
“Agizo hilo linatakiwa kwenda sambamba na kuudhibiti uuzaji wa vyakula na matunda yaliyomenywa katika sehemu zisizoruhusiwa,” alisema.
CHANZO: GAZETI LA HABARI LEO.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa