Home » » SIMU ZINAVYOSHAWISHI MAPENZI KWA WANAFUNZI

SIMU ZINAVYOSHAWISHI MAPENZI KWA WANAFUNZI

Tangu teknolojia ya mawasiliano ya simu za mkononi ilipoingia nchini, mambo mengi katika jamii, ukiwamo mfumo mzima wa maendeleo na namna ya kuishi, yamebadilika.
Teknolojia hiyo imeondoa usumbufu uliokuwapo awali, mtu alikuwa analazimika kukaa muda mrefu kusubiri kuunganishiwa simu posta na baadaye katika Kampuni ya Mawasiliano ya Simu Tanzania (TTCL). Hata baada ya kupata mawasiliano bado usikivu ulikuwa hafifu licha ya kupiga kelele sana.
Si hivyo tu, watu walikuwa wanalazimika kufika mjini au miji maarufu kwa ajili ya kusaka mawasiliano ya simu. Pia, wengi walikosa.
Kutokana na gharama kubwa ya simu wakati ule, haikuwa rahisi kwa wanafunzi kuzifikia. Wale waliomudu kupiga walikuwa watoto wa viongozi au wenye uwezo mkubwa.
Leo ni tofauti. Simu za mkononi zimeondoa ukiritimba huo kiasi kwamba watu wengi mjini na vijijini wanamiliki na kufanya mawasiliano wakati wowote na bila kuzuiwa. Ubora wa teknolojia hiyo, ambayo vijana wanaita mtandao, ni kwamba mtu anaweza kuzungumza kwa sauti ya chini hata jirani yake asisikie.
Teknolojia hiyo ina faida kadhaa; imerahisisha muda wa mawasiliano, imeongeza ufanisi katika biashara na kazi. Lakini pia imechangia uvunjifu wa maadili hasa upande wa wanafunzi.
Uchunguzi unaonyesha kwamba japokuwa hakuna sheria iliyotungwa kuwabana wanafunzi kumiliki na kutumia simu katika mazingira ya shule, baadhi ya shule zimeweka taratibu za kuwabana.
Mwanya huo ndio unatumiwa na baadhi ya wazazi kuwapa simu watoto wao kwa madai watumie kuwajulisha wazazi ikiwa wamepata matatizo.
Lengo hilo ni zuri, lakini uchunguzi unaonyesha wengi wao hutumia katika mawasiliano ya hovyo na kupanga miadi ya utovu wa maadili na wavulana au wanaowaita wapenzi wao. Waathirika wakubwa katika mlolongo wote ni wasichana.
Pia, uchunguzi unaonyesha wanafunzi wasichana ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuwanunulia simu hupata vishawishi vya kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi na wavulana ili wanunuliwe simu. Madhara yake huwa ni mimba na kisha kufukuzwa shule.
Udhibiti mdogo
Udhibiti mdogo wa wazazi kuhusu mienendo ya watoto wao ndio umesababisha kubaki wakishuhudia simu za thamani ya hadi Sh200,000 zikimilikiwa na mabinti wao badala ya zile za Sh15,000 ambazo hazina mvuto.
Baadhi ya shule za sekondari kama Ndwika ya Lindi, Mara na Benjamin Mkapa zimeweka sheria kuzuia umiliki wa simu. Aliyekuwa kiranja mkuu wa Mara Sekondari aliadhibiwa kwa kukiuka sheria hizo na alipokataa kikawa chanzo cha vurugu na uharibifu shuleni, akafukuzwa shule.
Uongozi wa Jitegemee Sekondari umeweka sheria kuwa mwanafunzi yeyote atakayekutwa na simu eneo la shule atanyanganywa na mwisho wa muhula simu zote huuzwa kwa mnada mbali ya adhabu nyingine.
Utaratibu huo wa adhabu kali umesaidia kupunguza tatizo hilo na uongozi unaamini umechangia kuzuia wanafunzi wa kike kufanya mawasiliano ya kimapenzi.
Viongozi wa shule wanaamini hatua hizo inawazuia wanafunzi wa kike kujiingiza katika ngono zembe na wengine kupata mimba pamoja na magonjwa ya zinaa kwa lengo tu la kupata simu.
Maoni ya wazazi, walimu na hata wanafunzi ni kwamba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iweke sheria kwa shule zote wanafunzi wasiruhusiwe kumiliki simu pindi wanapokuwa shuleni.
Kuwapo kwa sheria hiyo kutatoa uwiano sawa wa kosa hilo kwa wanafunzi wa shule zote za Serikali na za binafsi ambazo zaidi ya asilimia 80 ya wanafunzi wanamiliki simu tena za thamani.
Katika shule za Serikali mwenye simu hata ya Sh45,000 au Sh35,000 anaonekana wa tabaka la juu.
Kwa hiyo, japokuwa mtandao umekuwa moja ya nyanja kuu za mawasiliano katika maisha ya leo, pale unapotumiwa vibaya na wanafunzi, matokeo yake huwa mabaya kama kujiingiza katika biashara haramu ili wapate pesa za kununulia na wengine kujiingiza katika vishawishi vya mapenzi na wanaume kwa lengo la kununuliwa mtandao.
 Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Njombe Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa