Tangu teknolojia ya mawasiliano ya simu za mkononi ilipoingia
nchini, mambo mengi katika jamii, ukiwamo mfumo mzima wa maendeleo na
namna ya kuishi, yamebadilika.
Teknolojia hiyo imeondoa usumbufu uliokuwapo
awali, mtu alikuwa analazimika kukaa muda mrefu kusubiri kuunganishiwa
simu posta na baadaye katika Kampuni ya Mawasiliano ya Simu Tanzania
(TTCL). Hata baada ya kupata mawasiliano bado usikivu ulikuwa hafifu
licha ya kupiga kelele sana.
Si hivyo tu, watu walikuwa wanalazimika kufika
mjini au miji maarufu kwa ajili ya kusaka mawasiliano ya simu. Pia,
wengi walikosa.
Kutokana na gharama kubwa ya simu wakati ule,
haikuwa rahisi kwa wanafunzi kuzifikia. Wale waliomudu kupiga walikuwa
watoto wa viongozi au wenye uwezo mkubwa.
Leo ni tofauti. Simu za mkononi zimeondoa
ukiritimba huo kiasi kwamba watu wengi mjini na vijijini wanamiliki na
kufanya mawasiliano wakati wowote na bila kuzuiwa. Ubora wa teknolojia
hiyo, ambayo vijana wanaita mtandao, ni kwamba mtu anaweza kuzungumza
kwa sauti ya chini hata jirani yake asisikie.
Teknolojia hiyo ina faida kadhaa; imerahisisha
muda wa mawasiliano, imeongeza ufanisi katika biashara na kazi. Lakini
pia imechangia uvunjifu wa maadili hasa upande wa wanafunzi.
Uchunguzi unaonyesha kwamba japokuwa hakuna sheria
iliyotungwa kuwabana wanafunzi kumiliki na kutumia simu katika
mazingira ya shule, baadhi ya shule zimeweka taratibu za kuwabana.
Mwanya huo ndio unatumiwa na baadhi ya wazazi
kuwapa simu watoto wao kwa madai watumie kuwajulisha wazazi ikiwa
wamepata matatizo.
Lengo hilo ni zuri, lakini uchunguzi unaonyesha
wengi wao hutumia katika mawasiliano ya hovyo na kupanga miadi ya utovu
wa maadili na wavulana au wanaowaita wapenzi wao. Waathirika wakubwa
katika mlolongo wote ni wasichana.
Pia, uchunguzi unaonyesha wanafunzi wasichana
ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuwanunulia simu hupata vishawishi vya
kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi na wavulana ili wanunuliwe
simu. Madhara yake huwa ni mimba na kisha kufukuzwa shule.
Udhibiti mdogo
Udhibiti mdogo wa wazazi kuhusu mienendo ya watoto wao ndio
umesababisha kubaki wakishuhudia simu za thamani ya hadi Sh200,000
zikimilikiwa na mabinti wao badala ya zile za Sh15,000 ambazo hazina
mvuto.
Baadhi ya shule za sekondari kama Ndwika ya Lindi,
Mara na Benjamin Mkapa zimeweka sheria kuzuia umiliki wa simu.
Aliyekuwa kiranja mkuu wa Mara Sekondari aliadhibiwa kwa kukiuka sheria
hizo na alipokataa kikawa chanzo cha vurugu na uharibifu shuleni,
akafukuzwa shule.
Uongozi wa Jitegemee Sekondari umeweka sheria kuwa
mwanafunzi yeyote atakayekutwa na simu eneo la shule atanyanganywa na
mwisho wa muhula simu zote huuzwa kwa mnada mbali ya adhabu nyingine.
Utaratibu huo wa adhabu kali umesaidia kupunguza
tatizo hilo na uongozi unaamini umechangia kuzuia wanafunzi wa kike
kufanya mawasiliano ya kimapenzi.
Viongozi wa shule wanaamini hatua hizo inawazuia
wanafunzi wa kike kujiingiza katika ngono zembe na wengine kupata mimba
pamoja na magonjwa ya zinaa kwa lengo tu la kupata simu.
Maoni ya wazazi, walimu na hata wanafunzi ni
kwamba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iweke sheria kwa shule zote
wanafunzi wasiruhusiwe kumiliki simu pindi wanapokuwa shuleni.
Kuwapo kwa sheria hiyo kutatoa uwiano sawa wa kosa
hilo kwa wanafunzi wa shule zote za Serikali na za binafsi ambazo zaidi
ya asilimia 80 ya wanafunzi wanamiliki simu tena za thamani.
Katika shule za Serikali mwenye simu hata ya Sh45,000 au Sh35,000 anaonekana wa tabaka la juu.
Kwa hiyo, japokuwa mtandao umekuwa moja ya nyanja
kuu za mawasiliano katika maisha ya leo, pale unapotumiwa vibaya na
wanafunzi, matokeo yake huwa mabaya kama kujiingiza katika biashara
haramu ili wapate pesa za kununulia na wengine kujiingiza katika
vishawishi vya mapenzi na wanaume kwa lengo la kununuliwa mtandao.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment